Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sura nyingine tofauti kwa Fei Toto na Simon Msuva

JICHO Pict

Muktasari:

Nilimshangaa Tshabalala kidogo. Alikuwa mpole kama alivyo. Kando yake alikuwa amezungukwa na vijana wengi wasio na majina. 

NINI kinambadili mwanadamu? Vitu vitatu. Pesa, umaarufu na madaraka. Wapo wachache ambao wanaendelea kuwa kama walivyo. Nilisafiri na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenda Indonesia Februari mwaka jana na kikosi cha timu ya taifa. Haikuwa kalenda ya FIFA. Ulikuwa mwaliko tu wa wenyeji.

Nilimshangaa Tshabalala kidogo. Alikuwa mpole kama alivyo. Kando yake alikuwa amezungukwa na vijana wengi wasio na majina. Mastaa wakubwa walikuwa wametoa visingizio kibao vya kutosafiri. Kibu Dennis alidai kuwa amechoka na alisema anaenda Marekani kupumzika. Pesa bwana. Hata hivyo, Tshabalala ndo alikuwa mchezaji pekee mwenye jina kubwa na hakuchoka kusafiri.

Nimekumbuka tena kilichotokea juzi. Kwa sasa nipo Afrika Kusini na timu ya taifa. Ijumaa jioni kulikuwa na mechi ya kimataifa ya kalenda ya FIFA dhidi ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ katika dimba la Peter Mokaba pale Polokwane. Kilomita 300 kutoka jijini Johannesburg.

Mechi ilikuwa ngumu kama ilivyoonekana katika televisheni huko nyumbani. Pambano lilipomalizika wachezaji wa Yanga na Simba waliruhusiwa kulala ili asubuhi warudi Johannesburg ili kurudi nyumbani kwa kile kinachodaiwa kuwahi dabi yao ambayo mpaka sasa ni kama hadithi ya ndotoni. Hatujui kama ipo wala haipo.

Wachezaji wengine walipaswa kula, kuoga na kuanza safari ya usiku huo huo, saa tano usiku, kutoka Polokwane kwenda Bloemfotein. Safari ya kilomita 720. Walitakiwa kufika saa moja asubuhi na kucheza pambano jingine jioni yake dhidi ya Madagascar ikiwa ni pambano lao la kwanza la michuano ya COSAFA.

JICH 01

Kikosi hiki hakina majina makubwa lakini katika kundi hili kulikuwa na sura mbili zenye majina makubwa. Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Simon Msuva. Na wao walilazimika kukunja magoti wakiwa wamelala katika basi kutoka Polokwane mpaka Bloemfotein. Walinitafakarisha sana. Nawajua wachezaji ambao walijitoa kijanja katika pambano dhidi ya Afrika Kusini, lakini wapo na klabu zao wanafanya mazoezi kama kawaida.

Kwangu ilikuwa kitu cha msingi kuwaona Fei na Msuva wakiwa wamekunja magoti kwenye basi njiani kwenda Bloemfotein. Ni utii kwa taifa. Ingekuwa rahisi kuweka visingizio. Ama wasiwepo Polokwane au wasiwepo Bloemfotein. Hata hivyo, walitii ombi la kuitwa. Haikunishangaza sana kwenda Polokwane, lakini ilinishangaza kidogo kuwaona Bloemfotein. Tena katika michuano ya COSAFA.

Wote walianza katika pambano hili ingawa walikuwa hoi. Fei hakuweza hata kumaliza kipindi cha kwanza na alitolewa nafasi yake ikaenda kwa Shekhan. Msuva naye hakuweza kumaliza dakika 90 za pambano hilo na alitolewa ingawa Stars walikuwa wanahitaji kusawazisha.

Wachezaji wa siku hizi wanasumbua. Hawa wenye vipaji wa siku hizi wana mambo mawili. Wana umaarufu na wana pesa. Ni rahisi kuwa na viburi. Kuanzia Afrika hadi Ulaya wachezaji wa kizazi kipya ni jeuri. Katika mechi kama hizi ni rahisi kwao ‘kujiumiza’ na kutosafiri au kutocheza. Mfano, hata baada ya pambano dhidi ya Afrika Kusini ambalo liliwaweka sokoni Fei na Msuva ilikuwa rahisi kwao kudai wameumia na wasingeweza kusafiri kwenda Bloemfotein.

JICH 02

Vijana wadogo wengine kina Pascal Msindo bado wana ari. Bado wanasaka majina kwa nguvu. Bado hawajateseka na safari hizi. Lakini kwa kina Fei ingekuwa jambo rahisi tu kutoa visingizio na kurudi nyumbani. Wangeweza kurudi nyumbani hata kwa nauli zao. Wana pesa na kama tunavyojua pesa inaongea.

Ukiona hivyo ujue mchezaji ana nidhamu. Nidhamu na kazi yake na nidhamu kwa taifa lake. Ni jambo kubwa katika maisha ya kazi yao na haishangazi kuona hata wanafanikiwa katika maisha yao ya mpira. Hawa sio wachezaji masela ambao tunaona wamekwama. Wale wachezaji ambao tuliwasifu kuwa na vipaji vikubwa lakini sasa hivi wamekosa mwelekeo.

Hawa kina Fei pia wamenikumbusha namna ambavyo mashabiki wa Tanzania hatuna fadhila. Licha ya kujitoa huku lakini mara nyingi huwa wanaishia kutukanwa tu wanapokosea uwanjani wakiwa wamevaa jezi ya timu ya taifa. Imetokea mara nyingi na tunasahau tabu wanazopitia mpaka kuvaa jezi.

Mfano ni Mbwana Samatta. Huwa anakunja magoti katika ndege kutoka Ulaya mpaka Tanzania. Safari ya usiku, futi nyingi juu ya usawa wa bahari huku unapigwa na baridi. Anapocheza na asipofunga bao mashabiki wanamshutumu kwamba hajitumi. Wanasahau kwamba Samatta wa Ulaya anacheza na wachezaji wazuri kuliko Samatta wa Taifa Stars. Hili hatuliangalii.

JICH 03

Wanasahau kwamba Samatta wa Taifa Stars kwa sababu mipira mingi haimfikii akisimama pale mbele basi analazimika kurudi mpaka katikati ya uwanja kwa ajili ya kupokea mipira na kuchezesha timu zaidi kuliko kusubiri kupelekewa mipira. Haya yote tunayaweka kando na tunachosubiri ni kumshutumu tu kwamba hajitumi.

Tunasahau kwamba hata katika mechi hizi ngumu za Stars bado yeye ndiye mchezaji ambaye wageni huwa wanamtazama zaidi kwa sababu ya jina lake. Hii inatoa nafasi kwa Msuva au mchezaji mwingine kufunga. Hilo jambo aliwahi kuniambia Msuva mwenyewe akikiri umuhimu wa Samatta kuwepo uwanjani.

Na sasa nimezijua sura nyingine za Fei na Msuva. Mtu mwingine anaweza kudhani ni wajibu wao kufanya walichofanya. Ni kweli. Lakini hata wasingetimiza wajibu wao bado hatuna tunachoweza kuwafanya. Zaidi ni kwamba makocha pia wanapata wakati mgumu kuwawajibisha wachezaji hawa kwa sababu hata kama wakikosea mashabiki tunatoa shinikizo kwao wawepo vikosini.

JICH 04

Ni rahisi kwa mchezaji wa Tanzania kukosa nidhamu kwa sababu mara zote ambazo atakosa nidhamu bado mashabiki watasimama nyuma yake na kumgeuzia kibao kocha au uongozi. Ukiona mchezaji anafanya hiki anachofanya basi ni kwa sababu ana nidhamu ya asili kutoka kwao. Hajabadilishwa na pesa wala umaarufu.

Vinginevyo kuhusu pambano la Stars dhidi ya Afrika Kusini vyombo vya habari vya hapa vimevutiwa na uwezo wa Pascal Msindo pamoja na Fei mwenyewe. Na ni kweli, Pascal Msindo anakuja juu. Anacheza bila ya wasiwasi hata sekunde moja. Anatulia na mpira. Akili nyingi kichwani na mguuni. Sidhani kama atatoka salama.

Wakati pengo la Shomari Kapombe na walinzi wengine wa upande wa kulia likionekana kuwa kubwa, pengo la Tshabalala na Msindo halionekani kuwa kubwa. Shavu la kushoto lipo salama na litaendelea kuwa salama kwa sababu hata Tshabalala mwenyewe bado yupo fomu. Ni vile tu Tanzania tunapenda kuzeesha wachezaji ambao wametamba kwa muda mrefu.

Kwa Fei ameendelea kujitengenezea soko lake Afrika Kusini. Alikuwa na mechi nzuri hasa katika kipindi cha pili. Yusuf Kagoma alikuwa anapiga nyundo kwa nyuma wakati Fei alikuwa anahaha kwa mbele akionyesha uwezo wake binafsi. Wasauzi wanampenda na wanamtupia jicho la karibu kwa sababu amekuwa akitajwa katika vyombo vya habari vya huku kama mchezaji nyota zaidi kikosini.