Prime
Yanga, Simba chaka lao liko hapa!
SIMBA na Yanga zinarudi nyumbani baada ya kila moja kutoka kupokea kichapo katika mechi za ugenini za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya vigogo, Al Ahly ya Misri na Esperance ya Tunisia.
Yanga ilianza kucheza mechi ya raundi ya tatu ya Kundi B dhidi ya Al Ahly Ijumaa na kupasuka mabao 2-0 ya Mahmoud Hassan 'Trezeguet' aliyefunga dakika ya 45+3 na 75, kisha siku inayofuata Simba ikavaana na Esperance katika mechi ya Kundi D na kulala bao 1-0 jijini Tunis la Jack Diarra dakika ya 21.
Kupoteza mechi hizo kumetokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiufundi na kiuzoefu kutokana na wapinzani waliokutana nao, lakini timu zote zikiwa na dakika nyingine 90 kila moja ya kulipa kisasi nyumbani na kufufua tumaini la kuisaka tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo kwa makundi yaliyopo.
AL AHLY 2-0 YANGA
Mechi hii ya Kundi B, ilidhihirisha uzoefu wa Al Ahly muda wake wa kuamua mechi kwani kabla ya kukutana na Yanga, ilikuwa na rekodi nzuri ya kutumia dakika 15 za mwisho kipindi cha kwanza na 15 za mwisho kipindi cha pili katika kufunga mabao. Pia dakika 15 za kwanza kipindi cha pili.
Hata Yanga, nayo imekuwa na uwezo huo wa kutumia muda huo kufunga katika mechi zake za kimataifa msimu huu kwa mujibu wa rekodi zilivyo.
Al Ahly ilitumia vizuri uzoefu wake kupata ushindi huo uliowaweka kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi saba, ikiiacha Yanga nafasi ya pili na pointi nne. JS Kabylie na AS FAR Rabat zinafuatia kila moja na pointi mbili.
Matokeo ya 0-0 waliyoyapata JS Kabylie na AS FARR Rabat, imekuwa faida kwa Yanga kuelekea mechi tatu zilizobaki zikiwamo mbili za nyumbani dhidi ya Al Ahly na JS Kabylie, pia ile ya ugenini ikiifuata AS FAR Rabat.
Kwa hesabu zilivyo sasa, Yanga ikikusanya pointi tano pekee katika mechi tatu zijazo, ina nafasi kubwa ya kufuzu robo fainali kwani itafikisha tisa ambazo zitaiweka sehemu nzuri.
Hiyo inatokana na namna nafasi ya pili iliyopo Yanga sasa na pointi zake zinaibeba dhidi ya AS FAR Rabat na JS Kabylie.
Ili timu hizo mbili zikate tiketi ya kufuzu robo fainali, lazima kila moja ishinde mechi zote tatu kitendo ambacho ni kigumu. Kumbuka zinakutana zenyewe, hapo kikwazo cha kwanza, pia zinakwenda kukutana na kinara wa kundi, Al Ahly inayohitaji ushindi wa mechi moja pekee kati ya tatu kujihakikisha tiketi ya robo fainali.
Hesabu za Yanga zinaweza kutimia mapema endapo Januari 31, 2026 ikikataa unyonge mbele ya Al Ahly itakapoikaribisha pale New Amaan Complex, Unguja.
Kama ilivyofanya msimu wa 2023-2024 ilipoikazia Al Ahly jijini Dar na kutoka sare ya bao 1-1 iliyokuwa na faida baadaye ikafuzu robo fainali, safari hii karata muhimu ipo hapo.
Hata hivyo, inaweza kutumia mechi zingine mbili zitakazofuatia kukusanya angalau pointi nne dhidi ya AS FAR Rabat ugenini na JS Kabylie nyumbani.
Kuwadhoofisha wapinzani wake kwa kulazimisha sare au kushinda, itakuwa faida kwa Yanga.
Kilichobaki ni kocha Pedro Goncalves wa Yanga kuchanga karata zake vizuri kumalizia vizuri kazi aliyoianza hatua ya makundi tangu akabidhiwe kikosi.
Maingizo mapya ya Yanga kupitia dirisha dogo la usajili kwa kiasi fulani yameonyesha kiu ya upambanaji. Licha ya kupoteza dhidi ya Al Ahly, lakini wapya waliopata nafasi ya kucheza, Mohamed Damaro, Allan Okello na Laurindo Dilson Maria Aurélio 'Depu' walioanza kikosi cha kwanza, namba zao zilitoa matumaini.
Kwa mujibu wa flashscore, Damaro amepewa alama 6.7 kutokana na kiwango alichoonyesha dakika 57 alizocheza na kuambulia kadi ya njano, kabla ya kumpisha Mudathir Yahya, huku Okello akiokota 6.0 kwa dakika 75, akaja kumpisha Prince Dube. Wakati Depu aliyemaliza dakika tisini, ameambulia 5.9.
ESPERANCE 1-0 SIMBA
Yalikuwa matokeo mazuri sana kwa Esperance iliyoanza hatua ya makundi kwa sare mfululizo, huku hali ikiwa mbaya upande wa Simba iliyopokea vipigo vitatu hadi sasa.
Katika kundi D, Simba haina kitu, si hilo tu, bali imefunga bao moja pekee huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nnae hali iliyofanya Wanasimba kupoteza matumaino ya kufuzu robo fainali kama kawaida yao.
Hii ni mara ya kwanza Simba inapoteza mechi tatu mfululizo hatua ya makundi katika michuano ya CAF.
Mwaka 2003, Simba ilicheza makundi ya Ligi ya Mabingwa, haikufuzu robo fainali lakini haikupoteza mechi tatu mfululizo za makundi.
Ilianza kufungwa 3-0 na Enyimba, ikaja kuichapa ASEC Mimosas 1-0, kisha ikatoka 0-0 na Ismaily. Mechi tatu za kwanza ilikuwa na pointi nne.
Baada ya hapo ikafungwa 2-1 na Ismaily, ikaja kushinda 2-1 dhidi ya Enyimba, ikamaliza na kichapo cha 4-3 mbele ya ASEC. Ikashika nafasi ya tatu na pointi saba.
Kidogo msimu wa 2022-2023 ilianza vibaya lakini haikupoteza mechi tatu mfululizo, badala yake ni mbili. ilianza kufungwa bao 1-0 na Horoya ugenini, kisha ikapokea kichapo cha 3–0 nyumbani dhidi ya Raja Athletic.
Baada ya hapo, Simba ikashinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Vipers (1-0) ugenini na nyumbani, kisha ikaichapa Horoya 7-0 nyumbani. Ikaenda Morocco kuhitimisha ratiba kwa kufungwa 3-1 na Raja Athletic, ikafuzu kwa pointi tisa ikiizidi Horoya iliyokuwa na saba na Vipers (2), wakati Raja ikiwa kinara na 16.
Hesabu za Wanamsimbazi sasa ni kupata pointi tisa katika mechi tatu zijazo ambapo inahitajika kazi ya ziada kufanikisha hilo kutokana na kundi lilivyokaa kimtego.
Matumaini ya kufuzu robo fainali ya michuano ya CAF kwa mara ya nane katika misimu tisa tangu 2018, yamefifia kutokana na kipigo cha jana, huku matokeo ya leo kati ya Petro Atletico na Stade Malien yakipigilia msumari zaidi.
Kabla ya wawili hao kukutana, kila mmoja alikuwa na pointi nne ambazo wameiacha Simba mbali, hivyo kuongezeka kwa gepu la pointi, inazidi kupoteza nafasi ya Simba kucheza robo fainali.
Miujiza inahitajika ili Simba icheze robo fainali msimu huu na itatakiwa kuzifunga Esperance (nyumbani), Petro Atletico (ugenini) na Stade Malien (nyumbani). Kumbuka ilipokutana na timu hizo zote, Simba imepoteza ikifungwa 1-0 dhidi ya Petro Atletico, Stade Malien (2-1) na Esperance (1-0).
Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kufuzu robo fainali michuano ya CAF mara saba katika kipindi cha kuanzia 2018 kila inapoingia makundi, haijawahi kucheza makundi na kukwama, huku 2024-2025 ikienda hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikapoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane. Safari hii mlima mrefu.
Kocha Steve Barker amekuwa na mguu mbaya ndani ya Simba, hii ikiwa ni mechi yake ya tano katika mashindano tofauti, ameshuhudia akikosa ushindi mara tatu mfululizo akifungwa 1-0 nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, akatoka 1-1 na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara na kichapo cha 1-0 mbele ya Esperance kwenye Ligi ya Mabingwa. Kabla ya hapo, ameshinda mechi mbili za Kombe la Mapinduzi dhidi ya Muembe Makumbi (1-0) na Fufuni (2-1).
Tatizo la Simba hadi sasa linaonekana katika kujilinda na kushambulia ambalo Barker anapaswa kulishughulikia kabla ya mambo hayajawa mabaya zaidi.
Katika mechi tano chini ya Barker, Simba imeondoka na clean sheet moja pekee iliposhinda 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi, huku ikiruhusu bao mechi nne mfululizo.
Pia timu hiyo imefunga mabao manne katika mechi tano ambapo wastani ni 0.8 kwa mechi ikiwa ndogo zaidi.
Mechi dhidi ya Esperance, Simba ilikuwa na uwezo wa kufunga kwa wastani wa 0.38 ikipiga shuti moja pekee lililolenga lango la wapinzani kati ya matano huku ikishindwa kutengeneza nafasi kubwa ya kufunga, wakati Esperance ikilenga manne kati ya sita, ikitengeneza nafasi moja kubwa ya kupata bao.
NAFASI BADO
Kwa kuyaangalia matokeo ya Kundi B ambapo ilishuhudiwa pia FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria zikishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu, kumetoa nafasi kwa Yanga kuendelea kusalia nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo, nyuma ya Al Ahly yenye pointi saba baada ya kila moja kucheza mechi tatu.
Yanga ina pointi nne, wakati FAR Rabat Kabylie kila moja ikiwa na pointi mbili na zitarudiana zenyewe kwa kwenye wikiendi hii kama ambayo vijana wa Jangwani watakavyoipokea Al Ahly visiwani Zanzibar ambapo inahitaji ushindi kisha kupambana mechi mbili za mwisho kukusanya pointi za kuipeleka robo fainali.
Kwa Simba mtihani ni mkubwa, kwani sasa inahitaji kushinda mechi zote tatu zilizosalia, ikianza na Esperance kisha ile y Petro Atletico ya Angola ya ugenini kabla ya kumalizana na Stade Malien ya Mali Februari 13, ili kufikisha pointi tisa zitakazoweza kuibeba kulingana na matokeo ya wapinzani wengine wa kundi hilo.
Kinyume cha hapo Simba itakuwa imeaga rasmi hatua hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu 2018-2019 ilipocheza hatua hiyo ya makundi, kwani kila iliposhiriki kuanzia Ligi ya Mabingwa hadi Kombe la Shirikisho Afrika ilikuwa ikivuka kwenda robo fainali na sio kuishia hapo.
Bahati mbaya ni kwamba Simba kwa msimu huu haijapata ushindi wowote nyumbani katika michuano ya CAF
kwani katika raundi ya kwanza ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Gaborone United, kisha kutoka suluhu na Nsingizini Hotspurs ya eSwatini kisha kupoteza kwa bao 1-0 mbele ya Petro Atletico katika hatua ya makundi.