Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayosubiriwa Championship ikikaribia ukingoni

Muktasari:

  • Kwa upande wa timu nyingine zinahitaji kuongeza nguvu zaidi ili kujinasua na nafasi za hatari, kama ambavyo Mwanaspoti linaelezea mambo yanayotarajiwa wakati ligi itakaporejea, hususani kutokana na mechi tisa tu zilizobakia kumaliza msimu.

BAADA ya Ligi ya Championship kusimama mwezi mzima, hatimaye uhondo huo unarejea Ijumaa hii ya Aprili 17, huku vita mpya ikishika kasi kwa timu hasa zinazowania nafasi mbili ya kupanda Ligi Kuu moja kwa moja na zile zitakazocheza 'Play-Off'.

Kwa upande wa timu nyingine zinahitaji kuongeza nguvu zaidi ili kujinasua na nafasi za hatari, kama ambavyo Mwanaspoti linaelezea mambo yanayotarajiwa wakati ligi itakaporejea, hususani kutokana na mechi tisa tu zilizobakia kumaliza msimu.


VITA YA TOP FOUR

Katika sehemu ya kuvutia kwa sasa ni katika nafasi nne za juu, ambazo zitatoa timu mbili za moja kwa moja kupanda daraja kwa maana ya kutoka Championship na kwenda kushiriki Ligi Kuu Bara, huku zitakazomaliza ya tatu na nne zikicheza mtoano.

Hadi sasa, Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, ikitokea Ligi Kuu hadi Championship, kwa msimu huu inaongoza Ligi ikiwa na pointi zake 52, baada ya kikosi hicho kucheza mechi 21 na kimeshinda 16, sare nne na kupoteza moja.

Msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship, Geita ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya timu hiyo ya mjini, Geita, kufeli mechi zake za 'Play-Off'.

Timu hiyo ilicheza 'Play-Off' ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Stand United 'Chama la Wana' iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

Kagera Sugar iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki mwaka 2005, msimu huu inapambana ili kurejea pia, baada ya kushika nafasi ya pili na pointi 49, ikishinda mechi 15, sare nne na kupoteza mbili tu kati ya 21.

Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyecheza pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, msimu huu imekuwa mshindani mkubwa wa Geita Gold, inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila.

Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, msimu huu inashika nafasi ya tatu na pointi 45, ikishinda mechi 14, sare tatu na kupoteza nne, huku Transit Camp ikiwa nafasi ya nne na pointi 43, ikishinda 13, sare nne na kupoteza nne.

Kwa upande wa maafande wa Polisi Tanzania ya mjini Moshi, msimu huu iko nafasi ya tano na pointi 42, baada ya kushinda mechi 12, sare sita na kupoteza tatu kati ya 21, ikipambana kurejea Ligi Kuu Bara, kufuatia kushuka msimu wa 2022-2023.


SPORTS, BARBERIAN MTEGONI

Timu za African Sports na Barberian, hadi sasa ziko katika nafasi ya kushuka daraja moja kwa moja kutokana na mwenendo usioridhisha msimu huu katika Ligi ya Championship, zikisubiria miujiza ya kujinasua na mtego huo kwa mechi tisa zijazo.

Sports maarufu kwa jina la utani la 'Wanakimanumanu', iko nafasi ya 15 na pointi 11, baada ya kikosi hicho kutoka mjini Tanga, kushinda mechi tatu tu, sare mbili na kupoteza 16 kati ya 21, iliyocheza, huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu 41.

Kwa upande wa Barberian FC zamani ikifahamika kwa jina la Kiluvya United, msimu huu iko nafasi ya 16, ikiburuza mkiani na pointi 10, ikishinda mechi moja, sare saba na kupoteza 13, kati ya 21, iliyocheza, ikifunga mabao 11 na kuruhusu 32.

African Sports iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship msimu wa 2015-2016, ilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 26, ina kazi kubwa ya kujinasua kushuka zaidi, sawa na Barberian FC, ambayo imekuwa na kiwango kisichoridhisha.


KAZI IPO HUKU!

Vita nyingine itakayovuta hisia za mashabiki ni kwa zile zitakazozikutanisha timu zilizomaliza nafasi ya 11, 12, 13 na 14, ili kusaka tiketi ya kubakia kwa msimu ujao katika ligi zitakapopambana zenyewe, kisha kukutana na za First League.

Hadi sasa timu zenye hatari hiyo ni TMA iliyokuwa nafasi ya 11 na pointi 21, ambazo ni sawa na za B19 FC, iliyokuwa ya 12, ila zikitofautiana kwa mabao, ikifuatiwa na Stand United 'Chama la Wana' inayoshika nafasi ya 13 na pointi zake 20.

Hausung FC ya Njombe iliyopanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi ya Championship, inashika nafasi ya 14 na pointi 11, baada ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza 16, ikihitaji kupambana zaidi ili kukwepa mtego wa kucheza mtoano.

Timu mbili zitakazoshinda kati ya 11, 12, 13 na 14, zitabakia Ligi ya Championship msimu ujao, huku mbili zitakazopoteza zitakuwa na kibarua cha kujitetea, kwa kucheza mechi nyingine za mtoano na za First League, ili kusaka tiketi ya kubaki.


VITA YA UFUNGAJI BORA

Sehemu inayovutia ni ya vita ya ufungaji bora, ambapo mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa, anaongoza kwa sasa akifunga mabao 14, akifuatiwa na Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp na Ramadhan Hashim wa B19 FC waliofunga 11, kila mmoja.

Kiwango hicho kizuri kwa Uledi, kiliwafanya mabosi wa KMC FC kumsajili mshambuliaji huyo katika dirisha dogo la Januari 2026, ili kuongezea nguvu eneo hilo la ushambuliaji, huku nyota wa Mbeya Kwanza, Boniface Mwanjonde, akifunga mabao 10.

Abrahaman Mussa aliyeanza msimu huu wa Ligi ya Championship akiwa na Gunners FC ya Dodoma, kisha dirisha dogo la Januari 2026, akajiunga na maafande wa Transit Camp na Samson Albert anayeichezea KenGold, kila mmoja wao amefunga mabao tisa.

Maulid Shaban wa Geita Gold, amefunga pia mabao tisa, huku, Joseph Ambokege na Seif Adam wanaoichezea Mbeya Kwanza na Emmanuel Mpuka wa maafande wa Polisi Tanzania, kila mmoja wao amefunga nane, wakizidi kukoleza vita ya ufungaji bora.