Ibenge kasukuma kete za ushindi Azam
Muktasari:
- Baada ya wiki mbili za kusambaa kwa taarifa za Ibenge kukaribia kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Mali, Azam wamezika rasmi tetesi hizo kwa kufichua kocha huyo atakuwepo hadi 2028.
ZILE tetesi za Florent Ibenge kuondoka Azam FC sasa zimezikwa rasmi na hatimaye Kocha huyo raia wa DR Congo sasa atabakia rasmi klabuni hapo.
Baada ya wiki mbili za kusambaa kwa taarifa za Ibenge kukaribia kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Mali, Azam wamezika rasmi tetesi hizo kwa kufichua kocha huyo atakuwepo hadi 2028.
Kwa sisi tuliosoma Cuba hapa kijiweni, tunaona kama taarifa za Ibenge kukaribia kujiunga na timu ya taifa ya Mali hazikuibuka kwa bahati mbaya na wala siyo jambo hilo halikuwa na ukweli.
Inavyoonekana ni kweli Ibenge aliomba kazi ya kuinoa Mali na ndiyo maana baada habari ya kuongeza mkataba wa kuitumikia Azam FC inaonekana kuwavuruga sana mabosi wa chama cha soka Mali.
Hapo kwenye kuomba, tunahisi kuna sababu moja hivi ya msingi ambayo imepelekea kocha wa mpira Ibenge kufanya jambo kimyakimya kwa kutuma maombi ya kazi kuinoa Mali pasipo kuwajuza waajiri wake.
Sababu hiyo ni kutengeneza mazingira ya kupata ongezeko la fedha katika mkataba wake kama ambavyo tunahisi bila kufanya hivyo pengine mambo yanakuwa hayaendi vyema.
Kama kusingekuwa na hiyo hali ya kuviziwa na chama cha soka Mali, pengine Azam FC wasingeona haja ya kumuongezea mkataba mpya kocha huyo kwa sasa kama ambavyo tayari wamefanya.
Pia imemsaidia Ibenge kufahamu nafasi na hadhi yake ndani ya klabu hiyo. Kuona maofisa wa Azam FC hawapati nafasi ya kupumua ili kuhakikisha suala la kocha huyo kutimkia Mali halizai matunda.