Prime
Washambuliaji wanaiogopa mipira ya TPLB
Muktasari:
- Shujaa huyo amekuwa Mosi Ndumumwe wa Singida Black Stars aliyefunga hat-trick katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
MSIMU wa Ligi Kuu Bara (TPLB) 2025-2026 unakaribia ukingoni ukiwa umeacha maswali mengi kuhusu kiwango cha ufungaji wa mabao.
Tofauti na misimu ya nyuma, mashabiki walizoea kuona washambuliaji wakitamba kwa mabao mengi na hat-trick zikitokea mara kwa mara, safari hii hali imekuwa tofauti kabisa. Imechukua hadi mzunguko wa 27 ndipo tukashuhudia mchezaji wa kwanza akiondoka na mpira wa mechi baada ya kufunga mabao matatu.
Shujaa huyo amekuwa Mosi Ndumumwe wa Singida Black Stars aliyefunga hat-trick katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Tukio hilo lilikuwa la kipekee kiasi cha kuwafanya wengi kujiuliza ni nini hasa kimewakumba washambuliaji wa ligi yetu. Kwa nini imekuwa vigumu kwao kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja? Je, ni uimara wa safu za ulinzi au ni kupungua kwa ubora wa washambuliaji wenyewe?
Sababu ya kwanza inaweza kuwa ni maendeleo ya kiufundi na kimkakati yaliyofikiwa na timu nyingi za ligi kuu. Makocha wengi wamewekeza muda mwingi katika maandalizi ya timu zao, wakihakikisha kila mchezaji anaelewa wajibu wake kulingana na aina ya mpinzani anayekutana naye. Timu zimekuwa bora zaidi katika kusoma mchezo, kufunga nafasi za wapinzani na kudhibiti maeneo hatari ya uwanja.
Matokeo yake ni kupungua kwa ushindi wa mabao mengi na nafasi za washambuliaji kutamba kama ilivyokuwa zamani. Safu za ulinzi zimeimarika, huku viungo wakipewa majukumu makubwa ya kusaidia katika kukaba na kulinda eneo la hatari. Hali hii imefanya kazi ya washambuliaji kuwa ngumu zaidi kuliko misimu iliyopita.
Sababu nyingine ni mgawanyo wa majukumu ya ufungaji ndani ya timu. Siku hizi timu nyingi hazimtegemei mshambuliaji mmoja pekee kufunga mabao. Viungo na hata mabeki wa pembeni wanashiriki kwa kiasi kikubwa katika mashambulizi na ufungaji. Ni jambo la kawaida kuona timu ikifunga mabao manne au matano huku wafungaji wakiwa wachezaji watatu au zaidi.
Mfano mzuri ni ushindi wa Yanga wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa. Licha ya idadi kubwa ya mabao, hakuna mchezaji aliyeffunga hat-trick. Mabao yaligawanywa kwa wachezaji tofauti, jambo linaloonyesha namna majukumu ya kufunga yalivyosambazwa ndani ya timu. Hii ni ishara ya maendeleo ya kimfumo, pia ni sababu inayopunguza uwezekano wa washambuliaji kuondoka na mpira wa mechi.
Pamoja na maendeleo hayo ya kimkakati, bado hatuwezi kupuuza ukweli, washambuliaji wengi wa ligi yetu wamekuwa na matatizo ya kutumia nafasi wanazozipata. Ukiangalia idadi ya nafasi zinazotengenezwa na timu pamoja na mabao yanayofungwa, utaona wazi kuwa kuna changamoto kubwa ya umaliziaji.
Takwimu za mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu zinathibitisha hali hiyo. Kwa muda mrefu msimu huu, nafasi za juu zimekuwa zikishikiliwa na viungo badala ya washambuliaji wa kati. Feisal Salum wa Azam FC anaongoza mbio hizo akiwa na mabao 14, idadi inayozidi mabao yote yaliyofungwa na Mashujaa FC kama timu. Pia ana mabao sawa na timu nzima ya KMC katika kipindi hicho cha msimu.
Takwimu hizi zinaonyesha wazi ukubwa wa tatizo lililopo kwa washambuliaji. Ikiwa kiungo mmoja anaweza kufunga mabao mengi kuliko timu nzima ya ligi kuu, basi kuna jambo linalohitaji kutazamwa kwa umakini katika eneo la ushambuliaji.
Kwa jumla, kiwango cha mabao katika ligi pia kimepungua. Msimu uliopita ulimalizika kwa jumla ya mabao 569, lakini hadi kufikia mzunguko wa 27 wa msimu huu yalikuwa yamefungwa mabao 458 pekee. Hiyo ni tofauti ya mabao 111. Ingawa bado kuna mizunguko michache iliyobaki, ni vigumu kuona pengo hilo likifutwa ndani ya muda huo mfupi.
Nusu ya timu za ligi bado hazijafikia wastani wa kufunga angalau bao moja kwa kila mchezo. Hii ni dalili changamoto si kwa washambuliaji pekee, bali pia katika ubunifu wa mashambulizi na uwezo wa kubadilisha nafasi kuwa mabao.
Mwisho wa yote, kuna pande mbili za kuangalia suala hili. Kwa upande mmoja tunaweza kupongeza maendeleo ya kimkakati na uimara wa safu za ulinzi ulioongeza ushindani wa ligi. Kwa upande mwingine, washambuliaji wanapaswa kubeba lawama kwa kushindwa kuonyesha ukatili unaohitajika mbele ya lango. Kama ligi yetu inataka kuendelea kuvutia mashabiki na kuzalisha washambuliaji wa kiwango cha juu, basi eneo la umaliziaji linahitaji kupewa kipaumbele kikubwa zaidi katika mazoezi na usajili wa wachezaji.
Hat-trick ya Mosi Ndumumwe inaweza kuwa kumbukumbu ya kipekee msimu huu, lakini pia imeibua mjadala muhimu kuhusu kiwango cha washambuliaji wa Ligi Kuu Bara na uwezo wao wa kugeuza nafasi kuwa mabao.