Wanayanga wawili kutikisa Bondeni msimu huu

Muktasari:

Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Papic kuushuhudia akiwa kama meneja au kocha mpya wa Chippa United maarufu kama ‘Chilli Boyz’, timu ambayo imerejea Ligi Kuu Bondeni na kumnyakua Papic kama kocha mkuu mpya akitokea Black Leopards ya Polokwane nchini humo.

JUMAPILI iliyopita, kocha wa zamani wa Yanga, Kosta Papic alikuwa katika benchi la timu ya Chippa United katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Port Elizabeth, akishuhudia timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) ikichapwa na Kaizer Chiefs mabao 4-2 katika mchezo wa kirafiki.

Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Papic kuushuhudia akiwa kama meneja au kocha mpya wa Chippa United maarufu kama ‘Chilli Boyz’, timu ambayo imerejea Ligi Kuu Bondeni na kumnyakua Papic kama kocha mkuu mpya akitokea Black Leopards ya Polokwane nchini humo.

Akiwa na Black Leopards tangu Agosti mwaka jana, Papic alishindwa kuipandisha daraja timu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa Afrika Kusini baada ya kuporomoka kutoka Ligi Kuu mwaka juzi.

Aidha kuchukuliwa kwa Papic kujiunga na Chippa United, kulitokana na timu hiyo kumkosa Kocha, Steve Komphela ambaye aliamua kubaki na timu yake ya Maritzburg United licha ya kupewa ofa ya kujiunga na Chilli Boyz.

Kwa Bondeni, Papic ana historia kubwa. Amewahi kuzifundisha timu kubwa mbili za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, timu ambazo zina upinzani wa jadi. Lakini kama unadhani Papic pekee ndiye ‘MwanaYanga’ anayepeperusha bendera ya Yanga katika Ligi ya PSL hapo Bondeni, basi umekosea.

Free State Stars ni timu yenye maskani yake katika Mji wa Bloemfontein katika jimbo la Free State. Timu hii ndiyo iliyokusudia kumnyakua Mrisho Ngasa ili ajiunge nayo, lakini uongozi wa Yanga ‘kama kawaida’ umemwekea kauzibe mchezaji huyu.

Pamoja na kumzibia Ngassa, bado Yanga ndani ya Free State inae kipenzi mwingine ambaye ni Kocha, Tom Saintfiet.

Saintfiet amejiunga Free State Stars akitokea Malawi alikokuwa akiifundisha timu ya taifa. Kabla ya hapo, Saintfiet aliifundisha Yanga kwa siku themanini na kuisaidia kutwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati Julai 2012 kisha kutimuliwa miezi miwili baadaye yaani Septemba mwaka huohuo baada ya kucheza mechi tatu pekee za Ligi Kuu.

Kisa na mkasa wa kufukuzwa wanaujua viongozi wa Yanga (wa wakati huo).

Msimu uliopita, Free State Stars ilikuwa na mwendo wa kusuasua ambapo al-manusra ishuke daraja. Hii ilikuwa ni baada ya kuwauza wachezaji wake nyota wengi ikiwa ni pamoja na Kipa wa Zambia, Kennedy Mweene aliyehamia Mamelodi Sundowns.

Matumaini ya Free State Stars kwa Kocha Saintfiet ni makubwa sana msimu huu kwani wanaamini kuwa atarejesha makali yao ya msimu wa mwaka juzi.

Makocha hawa wawili, Saintfiet na Papic, walibezwa na kutimuliwa ndani ya Yanga, lakini leo wamekuwa lulu katika moja ya ligi ngumu Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ligi ya PSL.

Naamini Wanayanga na wapenda soka wengine Tanzania, watafuatilia kwa karibu sana maendeleo ya ‘Wanayanga’ hawa wawili (Saintfiet na Papic) katika Ligi kuu ya Bondeni na kujua watavuna nini.

Kufanya kwao vyema katika Ligi hiyo ama kufanya kwao vibaya, bado litakuwa ni fundisho kubwa kwenye timu ya Yanga ambapo makocha wote hawa wawili wamepitia.

Mwisho, nawasihi Wanayanga wasikose kuangalia mchezo wa PSL Novemba 26, mwaka huu utakaofanyika katika Uwanja wa Fezile Dabi mjini Parys katika Jimbo la Free State, ambapo Kocha ‘Mwana-Yanga’ Kosta Papic atakuwa akiingoza Chippa United katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Free State Stars ambayo pia itakuwa chini ya Kocha ‘Mwana-Yanga’ Tom Saintfiet. Siyo mechi ya kukosa hata kidogo!