Wanaiaga Derby

Muktasari:

WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi ikizidi kupanda kwa mashabiki wa soka nchini pia kwa upande mwingine kuna wachezaji watakuwa wanaaga kabisa kwani ndio itakuwa nafasi yao ya mwisho kushiriki mchezo huo ndani ya timu hizo.

WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi ikizidi kupanda kwa mashabiki wa soka nchini pia kwa upande mwingine kuna wachezaji watakuwa wanaaga kabisa kwani ndio itakuwa nafasi yao ya mwisho kushiriki mchezo huo ndani ya timu hizo.

Leo Jumamosi, Simba na Yanga wanakutana katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara pale uwanja wa Mkapa.

Wachezaji hao wamemaliza mikataba na wengine bado wana mikataba lakini viwango vyao vinawapa nafasi finyu ya kuendelea kusalia katika vikosi hivyo.


SARPONG- YANGA

Michael Sarpong raia wa Ghana mpaka sasa ameifungia Yanga mabao manne kwenye ligi lakini bado hajawashawishi mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuwa na imani naye.

Ujio wake uliwafurahisha mashabiki na kuona kama timu hiyo imepata mtambo wa mabao lakini mambo yamekuwa tofauti kwani kila wakati amekuwa akiingia katika lawama kubwa ya kukosa mabao katika mechi za ligi.

Amewahi kuifunga Simba bao moja kwa penalti katika mchezo wa watani wa jadi uliofanyika Novemba 7 mwaka jana na mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hii inaweza kuwa Derby yake ya mwisho kwani ana nafasi ndogo ya kuendelea kuwepo kwenye kikosi hicho.


NCHIMBI - YANGA

Mchezaji mwingine ambaye naye Mei 8 inaweza kuwa Derby yake ya mwisho kwani hapana shaka msimu ujao ataonyeshwa mlango wa kutokea ni Ditram Nchimbi.

Nchimbi alisajiliwa Yanga wakati Desemba 2019 wakati wa dirisha dogo la usajili lakini ameshindwa kuonyesha kiwango ambacho wengi walikitarajia.

Ameifungia Yanga bao moja tu msimu huu timu yake ilipoibamiza Gwambina mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika April 20, 2021. Bao hilo alifunga na kumaliza ukame wake wa mabao aliokuwa nao kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuanza kunyooshewa vidole na mashabiki wa klabu hiyo kwa kuona kuwa timu yao ilisajili galasa.


NIYONZIMA-YANGA

Kabla ya msimu huu kuanza alimanusura aonyeshwe mlango wa kutokea lakini uongozi ukaamua kumbakisha na kumpa mkataba wa miezi sita.

Uongozi wa klabu hiyo umeampa mkataba mfupi ili kufuatilia maendeleo yake ingawa bado hajaweza kuonyesha ubora wake kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma hivyo naye inaweza kuwa Derby ya mwisho kwani anatajwa kuwa anaweza akaachwa.

Amekuwa hapati nafasi ya kuanza mara kwa mara msimu huu kutokana na ubora wa viungo waliopo ambao ni Mukoko Tonombe naFeisal Salum ‘Fei Toto’.


FISTON-YANGA

Fiston Abdurazack ni kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, mpaka sasa ameifungia Yanga bao moja tu kwenye ligi tangu ajiunge na timu hiyo Januari mwaka huu.

Alifunga bao hilo Machi 7 , Yaga ilipotoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania, bado ule ubora ambao mashabiki wao waliambiwa kuhusu mchezaji huyu haujaonekana mbele ya macho yao na hivyo kuwa katika nafasi ndogo ya kuendelea kuwa ndani ya kikosi hicho msimu ujao.

Yanga hivi sasa inataka kutengeneze timu bora itakayokuwa na wachezaji wenye mchango mkubwa na watakaoipa matokeo na ubingwa msimu ujao kwani kwa msimu wa nne huu timu hiyo inakosa ubingwa wa ligi, labda kama atafunga bao litakaloibeba timu hiyo inaweza kuwa salama yake


MIRAJI-SIMBA

Miraji Athuman ni miongoni mwa washambuliaji hatari anayelijua goli kama akiwa katika ubora wake lakini majeruhi yameonekana kumgharimu kwani hajatumika mara nyingi msimu huu.

Inadaiwa ana nafasi kubwa ya kutemwa kutokana na ubora wa kikosi cha Simba kwa sasa kilichosheheni mastaa wenye viwango vikubwa na inaonyesha kama akiendelea kuwepo anaweza akaua kipaji chake.

Anamaliza mkataba mwisho wa msimu na Derby hii kama atakuwepo kati ya wachezaji watakaoshiriki mchezo huo inaweza kuwa ni ya mwisho kwake kwa kipindi hiki ingawa uongozi una nafasi ya kumfikiria kumpa mkataba mpya.


WAZIRI JR-YANGA

Baada ya msimu uliopita kumaliza ligi akiwa amefunga mabao 13 wakati huo akiichezea Mbao, Yanga ilimsajili ikiamini atakwenda kutibu tatizo la ufungaji akishirikiana na washambuliaji wengine.

Hata hivyo mambo yamekuwa tofauti kwani mchezaji huyo ameifungia Yanga bao moja tu msimu huu alilofunga katika mchezo dhidi ya KMC uliofanyika kwenye uwanja CCM Kirumba Mwanza Oktoba 25 mwaka jana na kumaliza kwa Yanga kushinda mabao 2-1.

Kwa siku za karibuni hata nafasi ya wachezaji wanaokaa benchi hayumo jambo ambalo linampa tiketi kubwa ya kutemwa msimu ujao na kama kesho atakuwemo itakuwa ni mchezo wake wa mwisho wa watani wa jadi kushiriki.