Wakali rekodi za Simba CAF balaa!

Muktasari:

  • SIMBA imetinga hatua ya robo fainali kibabe, baada ya kumaliza hatua ya makundi ikiwa na mabao tisa, nane yakifungwa na maproo na moja na mzawa, ikipata bao moja ugenini na wamefungwa kwenye mechi moja ya ugenini kati ya tatu.

SIMBA imetinga hatua ya robo fainali kibabe, baada ya kumaliza hatua ya makundi ikiwa na mabao tisa, nane yakifungwa na maproo na moja na mzawa, ikipata bao moja ugenini na wamefungwa kwenye mechi moja ya ugenini kati ya tatu.

Katika mechi tano za hatua ya makundi kabla ya kuingia robo fainali na kabla ya mchezo wa juzi Ijumaa ugenini Misri dhidi ya Al Ahly mechi ya mwisho ya makundi uliokuwa wa marudiano baada ya awali Waarabu hao kuchapwa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, safu ya ulinzi ya timu hiyo ikiongozwa na Aishi Manula ilikuwa imeruhusu bao moja tu dhidi ya As Vita, ikishinda mabao 4-1.

Katika makala haya, Mwanaspoti linakuletea namna Simba ilivyotinga robo fainali, huku mastaa wa kigeni wakionekana kuibeba zaidi timu hiyo na winga wao Luis Miquissone akiongoza kwa mabao matatu.


AS Vita vs Simba 1-0

Baada ya Simba kutinga hatua ya makundi, ilianza vyema mchezo wake wa kwanza dhidi ya AS Vita nchini DR Congo na ilishinda bao 1-0, kupitia Chriss Mugalu aliyefunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 61, ushindi huo uliipa nguvu timu hiyo, kuamini inawezekana kufika mbali zaidi.


Simba vs Al Ahly -1-0

Iliichapa Al Ahly bao 1-0 Uwanja wa Mkapa, haikuwa kazi rahisi kutokana na rekodi ya wapinzani wao kuwekeza katika soka kwa muda mrefu, Luis ndiye aliyewapa heshima ya kutembea kifua mbele mashabiki wao baada ya kupiga shuti nje ya 18 dakika ya 31 na mpira kutua nyavuni.


Simba vs Al-Merrikh 3-0

Kabla ya kucheza Dar es Salaam, ilipoichapa Al Merrikh mabao 3-0, walianzia Sudan ambako walitoka suluhu, wafungaji wa mabao ya mechi ya nyumbani ni Luis dakika ya 18, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dakika 39 na Mugalu dakika 50.


Simba vs As Vita 4-1

AS Vita imepigwa ndani na nje, Uwanja wa Mkapa ilichapwa bao 4-1, mabao hayo yalifungwa na Luis dakika ya 30, Clatous Chama dakika 45+1, 84 na bao la nne lilipigwa na Larry Bwalya dakika 66.

Ukiachana na rekodi hiyo, kuna wachezaji ambao wametamba kwenye michuano hiyo, kama beki Joash Onyango (Mkenya) na nahodha msaidizi Tshabalala, Luis na Chama ambao walikuwa kwenye kikosi bora cha Caf.


NENO LA WADAU

Staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel analiona hilo, lakini anamkingia kifua John Bocco kwamba anaamini angefunga mabao mengi kama isingekuwa majeraha yalikuwa yanamwandama.

“Safu ya mbele kuna Bocco, Meddie Kagere, Mugalu na mawinga ambao wanatoa pasi na kufunga, ndio maana unaona hao wengine wana mabao mengi, pia kazi yao ni kufunga hivyo wamefanya wajibu wao, unaowezeshwa na ubora wa timu nzima,” anasema.

Kauli yake iliungwa mkono na staa mwenzake wa zamani wa kikosi hicho, William Martin anaeleza kwamba licha ya mapro kuonekana wamefunga mengi lakini anaamini ni ushirikiano wa timu nzima kuhakikisha wanafika mbali kwenye michuano hiyo.

“Kikosi kizima kipo vizuri kuanzia anayeanza hadi anayekaa benchi, kila mmoja ana mchango wake mkubwa, sidhani kama kikosi kingekuwa kibaya wangeweza kufunga mabao hayo, hayo ni mafanikio ya timu nzima, wanafanya kazi kwa kushirikiana bila kuweka ubinafsi mbele na wanatakiwa kuendelea hivyo hivyo hadi dakika ya mwisho,” anasema.