Wafungaji bora Championship wanavyoteseka Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Tangu msimu wa 2017-2018, ilikuwa ni mchezaji mmoja mmoja aliyeshinda tuzo ya mfungaji bora katika Ligi ya Championship, japo mambo yalikuwa ni tofauti msimu wa 2024-2025, baada ya kushuhudia wachezaji watatu wakifunga idadi sawa ya mabao.
MSIMU wa 2024-2025, uliingia katika rekodi mpya ya kushuhudia wachezaji watatu wakifunga idadi sawa ya mabao katika Ligi ya Championship, ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo yenye mvuto hapa Tanzania tangu msimu wa 2017-2018.
Tangu msimu wa 2017-2018, ilikuwa ni mchezaji mmoja mmoja aliyeshinda tuzo ya mfungaji bora katika Ligi ya Championship, japo mambo yalikuwa ni tofauti msimu wa 2024-2025, baada ya kushuhudia wachezaji watatu wakifunga idadi sawa ya mabao.
Msimu wa 2024-2025, nyota waliofunga idadi sawa ni Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar, Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold na Abdulaziz Shahame wa TMA ya jijini, Arusha, ambao kila mmoja alifunga mabao 18, ikiwa ni rekodi mpya ya Championship.
Licha ya ubora wa washambuliaji wote watatu, ila walishindwa kuvunja rekodi ya ufungaji bora inayoshikiliwa na aliyekuwa mshambuliaji wa KenGold, Edgar William anayeichezea Dodoma Jiji kwa sasa, ambaye msimu wa 2023-2024, alifunga mabao 21.
Idadi ya mabao ya Edgar William ni mengi zaidi kwa mshambuliaji kufunga katika Ligi ya Championship, kwani tangu msimu wa 2017-2018, hakuna aliyefunga kama yeye, jambo linalosubiriwa kuona mwingine atakayefikia au kuivunja pia rekodi hiyo.
Msimu wa 2017-2018, mfungaji bora alikuwa ni Hassan Mwaterema wa JKT Tanzania ambaye kwa sasa anaichezea Kagera Sugar, aliyefunga mabao 16, ambapo idadi hiyo ni sawa na iliyofungwa na Reliants Lusajo, msimu wa 2018-2019, akiwa Namungo FC.
Msimu wa 2019-2020, mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir aliibuka mfungaji bora baada ya kukifungia kikosi hicho mabao 10, huku Edgar William aliyeichezea Mbeya Kwanza kwa msimu wa 2020-2021, akishinda tuzo hiyo kufuatia kufunga 13.
Mshambuliaji wa maafande wa JKT Tanzania, Edward Songo akaibuka kidedea kwa kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo akiwa na kikosi hicho, akianza msimu wa 2021-2022, alipotupia kambani mabao 16, kisha msimu wa 2022-2023, akafunga 18.
Msimu wa 2023-2024, ndipo akaibuka Edgar William akiwa na KenGold aliyoipandisha Ligi Kuu Bara, baada ya kutupia mabao 21, ikiwa ni rekodi mpya kwa nyota aliyefunga idadi kubwa katika Ligi ya Championship, tangu kuanza msimu wa 2017-2018.
Baada ya kufunga mabao hayo 18, mashabiki na wadau wengi wa soka walitarajia kuwaona nyota hao wakiendeleza ubora wao katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, japo mambo yamekuwa ni tofauti, baada ya wote kupitia kipindi kigumu pia.
ANDREW SIMCHIMBA
Simchimba amejiunga na Mtibwa kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, aliyojiunga nayo, Julai 14, 2025, ingawa, kiwango chake hadi sasa kimekuwa cha kupanda na kushuka, licha ya rekodi bora alizokuwa nazo katika karia yake ya soka kiujumla.
Kama utakuwa umesahau pia, Simchimba ni miongoni wa nyota waliowahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2022-2023, alipofunga mabao yake saba, akiwa na kikosi cha Ihefu kwa sasa Singida Black Stars.
Tangu michuano hiyo iliporejea tena kwa msimu wa 2015-2016, Simchimba anashika nafasi ya tatu kwa nyota waliofunga idadi kubwa zaidi ya mabao, ambapo wa kwanza ni Omari Yassin wa Panama FC msimu wa 2019-2020, alipofunga tisa na kikosi hicho.
Idadi hiyo ya mabao tisa ya Omari Yassin, ni sawa na iliyofungwa pia na aliyekuwa mshambuliaji wa Coastal Union, Abdul Suleiman ‘Sopu’, msimu wa 2021-2022, ingawa kwa sasa anakichezea kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
Msimu wa 2024-2025, Simchimba aliiwezesha Geita Gold kumaliza nafasi ya nne katika Ligi ya Championship, baada ya kikosi hicho kumaliza na pointi 56, jambo lililoiwezesha kucheza mechi za ‘Play-Off’, kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya timu hiyo ilishindwa kutamba, baada ya kuchapwa jumla ya mabao 4-2, dhidi ya Stand United, ambapo kikosi hicho cha ‘Chama la Wana’, kilimaliza kwa msimu huo kikishika nafasi ya tatu na pointi 61, katika msimamo.
Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Licha ya rekodi bora kwa mshambuliaji huyo, ila amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Mtibwa Sugar msimu huu, akiwekwa benchi zaidi na nyota mwenzake, Kassim Shaibu ‘Mayele’ aliyeifungia timu hiyo mabao mawili ya Ligi Kuu Bara.
Tangu amejiunga na Mtibwa, Simchimba amefunga bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, Septemba 28, 2025, alilofunga dakika ya 16, huku pia, Lamela Maneno akijifunga mwenyewe dakika ya 47.
RAIZIN HAFIDH
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Dodoma Jiji, Gwambina na Coastal Union, baada ya kuonyesha kiwango bora msimu wa 2024-2025, akiwa na Mtibwa Sugar, mashabiki walitarajia angefanya vizuri zaidi, japo mambo yamekuwa magumu kwake hadi sasa.
Msimu huu wa 2025-2026, mshambuliaji huyo amefunga bao moja la Ligi Kuu Bara, wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Februari 22, 2026.
Katika mechi hiyo, Raizin alifunga bao hilo moja la kufutia machozi kwa Mtibwa Sugar dakika ya 88, huku mabao ya Singida yakifungwa na Mossi Nduwumwe dakika ya 5, Malanga Horso Mwaku dakika ya 17 na beki wa kati, Kennedy Juma dakika ya 59.
ABDULAZIZ SHAHAME
Abdulaziz Shahame anayefananishwa na mshambuliaji nyota wa Manchester City ya England, Erling Braut Haaland baada pia ya kuonyesha kiwango bora msimu wa 2024-2025, akiwa TMA FC ya Arusha, alijiunga na Namungo FC, ili kuongeza nguvu kikosini.
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na TMA msimu wa 2024-2025, Shahame alisajiliwa na Namungo FC ili kuongezea nguvu katika eneo la ushambuliaji, ingawa, tangu amejiunga na kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, amefunga bao moja tu.
Bao hilo la Shahame aliifungia Namungo FC dakika ya 90+4, likiwa ni la kuchomoa kwa kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, katika mechi kali na ya kuvutia ya Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya kufungana 1-1, dhidi ya Pamba Jiji, Septemba 18, 2025.
Kabla ya msimu wa 2025-2026, kuanza, Shahame alikuwa mfungaji bora wa mashindano ya Tanzanite Pre-Season International, baada ya kufunga mabao manne akiwa na Namungo FC, kiwango kilichoashiria huenda angeendelea kufanya vizuri hadi sasa.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Klabu ya Fountain Gate kuanzia Agosti 31, 2025 hadi Septemba 7, 2025, yalishirikisha timu 10, zikiwemo sita za Ligi Kuu, ambazo ni Dodoma Jiji, Namungo FC, TRA United, Tanzania Prisons na Coastal Union.
Nyingine ni waandaaji, Fountain Gate, JKU ya Zanzibar, City FC Abuja kutoka Nigeria, TDS iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi na Eagle FC kutoka mkoani Manyara.
WASIKIE WENYEWE
Akizungumzia kiwango chake hadi sasa, Shahame anasema sababu kubwa ya kutokuwa na mwenendo mzuri kama msimu uliopita wa 2024-2025, ni kutokana na ushindani wa nafasi katika eneo la ushambuliaji, japo anaendelea kujifunza kwa waliomtangulia.
“Unapozungumzia Championship na Ligi Kuu ni vitu viwili tofauti, timu niliyokuwa mwanzo nilikuwa nacheza mara kwa mara, ila kwa Namungo FC nimekutana na wachezaji wazuri na wazoefu zaidi yangu, bado najifunza kutoka kwao,” anasema Shahame.
Kwa upande wa Raizin anasema licha ya ugumu wa Championship ila ni ngumu kuifananisha na Ligi Kuu kutokana na aina ya timu, wachezaji na ushindani ulivyo, ingawa malengo ya kila mchezaji ni kufanya vizuri bila kujali aina ya mashindano.
“Muda mwingine unaweza kutamani kitu na usifanikiwe, ndivyo ilivyo pia katika mpira wa miguu, ni kweli msimu huu umekuwa ni mgumu kwangu, ila nimezigeuza changamoto hizo kama fursa ya kunikuza kwenye maisha yangu kiujumla,” anasema Raizin.