VPL SPESHO: Wana zali kinoma

Muktasari:

LIGI Kuu Bara imemalizika jana Jumapili huku Simba ikitwaa ubingwa mara ya nne mfululizo, lakini kubwa ikiwa ni kwa baadhi ya makocha kupata zali la kufundisha timu zaidi ya moja msimu huu.

LIGI Kuu Bara imemalizika jana Jumapili huku Simba ikitwaa ubingwa mara ya nne mfululizo, lakini kubwa ikiwa ni kwa baadhi ya makocha kupata zali la kufundisha timu zaidi ya moja msimu huu.

Wakati msimu wa ligi 2020/2021 ukimalizika kuna makocha walikuwa na zali la kupata kazi katika timu tofauti licha ya wengine kupata misukosuko ya kutimuliwa kutoka timu walizokuwa wakizifundisha awali.


Amir Said-Mbeya City

Beki huyu wa zamani wa Simba msimu uliopita aliinoa Mbeya City iliyomaliza vibaya msimu kabla ya kuponea mechi ya mtoano ( Paly Off) baada ya kuichapa bao 1-0 Geita Gold FC.

Kocha huyo alianza msimu huu na timu hiyo lakini Oktoba 20 mwaka jana akatimuliwa baada ya Mbeya City kucheza michezo saba ikivuna pointi mbili tu ilizopata baada ya kutoka suluhu na Prisons na Dodoma Jiji huku ikiwa mkiani kwenye msimamo wa ligi.

Baada ya kukaa kwa muda bila timu, Amri akapata zali la kuifundisha Mwadui ya Shinyanga ambayo kipindi hicho iliachana na kocha wake wa muda mrefu Khalid Adam.

Amri alijiunga na Mwadui, Januari Mosi mwaka huu lakini aliingoza michezo sita na kupoteza mitano huku akitoka sare mchezo mmoja na wakati akijipanga kuendelea na harakati za kuinusuru timu na janga la kushuka daraja, ukaibuka mgomo wa wachezaji ambao waligoma kurejea kambini wakidai kwanza walipwe malimbikizo ya pesa zao.

Wakati sekeseke hilo likiendelea inadaiwa Amri nae akaamua kubwaga manyanga kwa madai hawezi kufanya kazi katika mazingira kama hayo.


Hitimana Thierry -Namungo FC

Mrundi huyu aliajiriwa Namungo Fc mwaka 2019 na kuisaidia timu hiyo kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu uliopita

Hitimana alifanya vizuri Namungo kwani aliiwezesha kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kuiwezesha kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Hata hivyo aliondolewa Novemba mwaka jana ikiwa ni mwanzoni tu mwa msimu huu wa ligi baada ya kuwachana mabosi wake kwa kufanya usajili ambao haukuwa mapendekezo yake.

Hitimana alikaa bila timu kwa mwezi mmoja kabla ya Desemba mwaka jana kupata dili la kuinoa Mtibwa Sugar akisaini mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo alidumu ndani ya kikosi hicho kwa miezi minne tu baada ya April mwaka huu alitangaza kutimka chanzo ni kutokuwa na maelewano mazuri na aliyekuwa kocha msaidizi Vincent Barnabas.


Zubery Katwila -Mtibwa

Kocha huyu amekuwa na zali msimu huu kwani baada kuingoza Mtibwa Sugar muda mrefu huku timu hiyo ikipata matokeo yasiyoridhisha, akachungulia akaona bora abadilishe upepo hivyo Oktoba 18 mwaka jana wakati ligi ikiwa ndio kwanza imeanza akabwaga manyanga baada ya kuingoza mechi sita, akishinda moja, akipoteza michezo mitatu na kutoka sare mechi mbili.

Siku moja baadae akaibukia Ihefu ya Mbarali Mbeya jambo ambalo lilileta mshangao kwa wadau wengi wa soka ambao waliona kama amejipeleka mahali pagumu zaidi kutokana na ugeni wa timu aliyoenda.

Hata hivyo mwenyewe alisema hayo ni maamuzi yake na yaheshimiwe kwani ameona ni bora atafute changamoto sehemu nyingine baada ya kukaa Mtibwa Sugar muda mrefu akiwa mchezaji na kocha pia.


Francis Baraza-Biashara united

Kocha huyu Mkenya naye amekuwa mwenye bahati msimu huu huku uwezo wake wa kuijenga timu ukiwa ndio silaha kubwa.

Alitua nchini Novemba 2019 kujiunga na Biashara United na kuiwezesha timu hiyo kumaliza msimu wa 2019/20 ikiwa nafasi ya tisa kwenye msmamo wa ligi.

Aliendelea kuinoa timu hiyo msimu huu hadi alipoamua kuondoka Machi mwaka huu, alijiunga Kagera Sugar ambayo ilikuwa ikipambana na janga la kushuka daraja.

Hata hivyo taarifa zilidai kocha huyo aliamua kuondoka Biashara baada ya timu hiyo kuwa katika ukata ikiwa baada ya kuiongoza katika michezo 22 ya TPL msimu huu.


Mohammed Badru

-GWAMBINA FC

Kocha huyu anafahamika kwa maneno mengi hasa timu yake inapomaliza mechi na usiombe awe ameshinda wapinzani wataomba poo.

Mzanzibar huyu alianza kuinoa Gwambina Februari mwaka huu na kuingoza michezo 10, alishinda minne, sare moja huku akipoteza mitano.

Mei 16 kocha huyo akaibukia Mtibwa Sugar na kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo ambayo ilikuwa ikipumulia mashine kwenye msimamo wa ligi huku akitamba kuwa ataibakisha ligi msimu ujao.