Vitengo vya habari Simba, Yanga na TFF vinapwaya

Muktasari:

Kitendo cha mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp, Instagram na mingine kuwa na mamilioni ya wafuasi ni ishara tosha kitengo cha habari na mawasiliano kinapaswa kupewa kipaumbele.

DUNIA nzima inafahamu umuhimu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano katika taasisi binafsi na za umma. Ni wazi kitengo hiki ndiyo msingi wa mawasiliano yote ya ndani na nje ya taasisi.

Umuhimu wa mawasiliano ndiyo unasababisha hata kitengo hicho kuwa taaluma ambayo inasomewa mpaka ngazi ya udaktari ili kurahisisha utendaji wake.

Taasisi zimekuwa zikiajiri watu wa mawasiliano na hao mara nyingi kazi yao imekuwa kubwa na yenye mashiko miongoni mwa umma.

Kwenye soka pia, kumekuwa na kitengo cha mawasiliano. Timu za soka pamoja na taasisi zinazosimamia mchezo huo zimekuwa zikiajiri watu wa mawasiliano ambao kazi yao kubwa ni kuhakikisha umma una taarifa zote muhimu kuhusu taasisi yao.

Kwa vipindi tofauti klabu za Simba na Yanga pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimekuwa zikiimarisha vitengo hivyo ili wadau wa michezo nchini wapate kufahamu ni kitu gani kinaendelea.

Katika dunia ya sasa suala la kitengo cha mawasiliano haliishii tu katika kutoa habari kwa vyombo vya habari, bali kujenga taswira chanya ya taasisi pamoja na kutoa taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Kitendo cha mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp, Instagram na mingine kuwa na mamilioni ya wafuasi ni ishara tosha kitengo cha habari na mawasiliano kinapaswa kupewa kipaumbele.

Kuwa na vitengo imara vya habari, ni moja ya mafanikio kwa taasisi kwani kwa kufanya hivyo, wanakuwa wamejihakikishia ulinzi wa taasisi yao pamoja na kupata sapoti kubwa ya umma.

Habari zinakuwa zikitoka kwa wakati, zinakuwa zimepangika na zenye kuleta ushawishi kwa jamii husika. Ikitokea hata taasisi imepata matatizo ni rahisi kwa vitengo hivi kutoa habari za uhakika ambazo zitasaidia kuondoa migogoro.

Baada ya kuona umuhimu huo wa kitengo cha habari na mawasiliano, turejee katika klabu za Simba na Yanga pamoja na TFF.

Kwanza, klabu ya Yanga mpaka sasa haina Ofisa Habari anayefahamika. Kitengo hicho tangu ameondoka Jerry Muro kimekuwa wazi na hakuna mtu aliyeajiriwa kurithi nafasi yake.

Kitendo cha Yanga kushindwa kuziba nafasi hiyo kwa mwaka mzima sasa ni wazi hawakipi kipaumbele kitengo hicho muhimu. Tangu Muro alipofungiwa mwaka jana taarifa za Yanga zimekuwa zikitolewa tu kiholela na mzigo mkubwa kuwa kwa Katibu Mkuu, Charles Mkwasa jambo ambalo siyo sahihi.

Yanga kama taasisi imekuwa ikichafuliwa huku na kule lakini kwa kuwa haina mtu wa habari, mambo yanakwenda tu yanavyokwenda.

Yanga imeshindwa kutambua kuwa hata Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limekuwa likisisitiza uwepo wa kitengo cha habari na limeweka katika moja ya masharti yake ya kupata leseni.

Ni jambo linalotia aibu kwa taasisi kubwa kama hiyo kukosa kitengo imara cha mawasiliano.

Kwa upande wa Simba, tangu alipofungiwa aliyekuwa Ofisa Habari wake, Haji Manara mwezi Mei mwaka huu, hakuna mtu ambaye ameteuliwa kurithi mikoba yake.

Manara amefungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja kutokana na kutoa lugha za kuudhi kwa vigogo hao wa TFF jambo ambalo limeacha kitengo hicho wazi.

Kutokana na Katibu Mkuu wa Simba, Hamis Kisiwa naye kuwa kama mtendaji baridi, kitengo cha habari cha klabu hiyo ni kama kimekufa.

Kwa wakati huu Rais wa klabu, Evans Aveva, pamoja na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wapo rumande, hali ya klabu inaweza isiwe tulivu kama kitengo cha habari hakipo.

Ni wazi nyakati hizi za matatizo ndizo zinahitaji zaidi uwepo wa kitengo imara cha habari hasa kwa kutolea ufafanuzi mambo ambayo yanaendelea pamoja na kutengeneza mkakati sahihi wa mawasiliano ili kulinda taswira ya taasisi.

Kwa upande wa TFF, kitengo cha Habari kipo lakini bado kinapwaya. Ofisa Habari aliyepo sasa, Alfred Lucas bado amekuwa hana mkakati sahihi wa mawasiliano hasa katika kipindi cha matatizo.

Mfano tangu kushikiliwa kwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na katibu wake, Celestine Mwesigwa, Alfred hajatoa taarifa zozote juu ya kukamatwa kwao pamoja na hali ya shirikisho kwa jumla.

Kitengo hiki kinapaswa kujitambua na kutambua majukumu yake, kuliko kusikitika tu pindi matatizo yanapotokea.

Kama watashindwa kusimama imara wakati huu wa matatizo, ni wazi wataiacha taasisi hiyo ikiwa imechafuka na isiyotamanika tena.

Alfred Lucas anapaswa kuamka na kufahamu TFF ni zaidi ya Malinzi ama watu wengine, bali ni taasisi ambayo inapaswa kulindwa na kusimamiwa imara.