VIALLI: Simba na Yanga wala siziwazii kivile

VIALLI: Simba na Yanga wala siziwazii kivile

MAISHA yana changamoto nyingi na kubwa ambazo zinaweza kukufanya mtu ushindwe kutimiza malengo na kujiona mkosaji, lakini bila ya kumtanguliza Mungu haiwezekani.”

Hayo ni maneno ya nyota wa Dodoma Jiji, Khamis Mcha ‘Vialli’ anayekiri bila kuwa na roho ngumu na kumuomba Mungu angeachana na soka kutokana na maisha aliyoyapitia miaka kadhaa iliyopita.

Anasema alikumbana na matukio makubwa na magumu, lakini alijitahidi kukaza roho na kupiga moyo konde na hadi sasa yuko kwenye ramani ya mpira anaendelea kucheza.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuichezea Azam FC alifunguka mambo mbalimbali kwenye maisha ya soka.


MAISHA AZAM USIPIME

Mcha anasema kila mchezaji aliyepita Azam FC hawezi kujutia maisha ndani ya klabu hiyo.

“Kiukweli kabisa Azam niliishi maisha mazuri sana. Ukiwa unapenda kucheza mpira ukienda Azam lazima utafurahia sana maisha ya soka kwa sababu wana kila kitu kinachohusiana na mambo ya mpira, labda ushindwe mwenyewe tu,” anasema.

“Niliondoka Azam baada ya kuumia na ule msiba wa baba yangu Mzee Mcha Khamis, bibi yangu mzaa mama na mume wa shangazi yangu iliambatana pamoja. Kipindi hicho nilipitia wakati mgumu sana kwakweli.

“Ni tukio ambalo siwezi kulisahau maishani mwangu kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa naumwa, nimeweka hogo (POP), nilikuwa nasumbuliwa na majeraha ya mguu hata kutembea nilikuwa siwezi.”

“Nilivyopona mguu, nakumbuka likaja suala lingine la kubana matumizi ndani ya Azam. Upande wangu jambo hilo sikukubaliana nalo kwa sababu walitaka wapunguze mshahara pamoja fedha ya kusaini mkataba mpya, nikaondoka zangu,” anasema Vialli.

Anasema kwa sasa anafurahia maisha ya Dodoma Jiji kutokana na namna ambavyo wanaishi kama familia moja kwa sababu ya muda mwingi kuwa pamoja kambini.

Mcha anasema kwenye maisha ya binadamu ili kufikia ndoto inabidi kukabiliana nazo kwa kuzipiga kumbo na kuangalia ulipoangukia na kunyanyuka.

“Sikuwahi kutamani kuacha soka kwa ajili ya changamoto kwa sababu napenda kucheza mpira, kushinda kitu chochote kile maishani mwangu. Changamoto nilizokuwa nakutana nazo nilikuwa naona ni mambo ya kawaida tu,” anasema Mcha ambaye anatamani kufikia mafanikio ya nyota kama Simon Msuva, Mbwana Samatta, Himid Mao na Thomas Ulimwengu wanaokipiga nje ya nchi.


KWA NINI SOKA

Vialli anasema ameamua kuchagua kucheza soka kwasababu ni mchezo ambao anaupenda toka utoto wake na ndio maana anautumikia hadi hivi sasa.

“Niliishia kidato cha nne, nikaamua kuwa bize na soka ambalo naendelea kucheza hadi nitakapoamua kustaafu, lakini kwa sasa bado sana,” anasema Mcha.

Kama asingekuwa mchezaji soka anasema basi angekuwa mpishi kwenye hoteli kubwa ndani na hata nje ya nchi kwa kuwa suala la kupika pia analijua vizuri.


TIMU YA TAIFA

Anasema kwa kipindi alichocheza soka ametoa mchango wake kwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na kukiri kutokuwa na deni hadi sasa. “Kiukweli kabisa kwa sasa sina deni na Taifa Stars, mechi ambayo sitoisahau nilivyocheza Stars mwaka 2014, ilikuwa mechi kati ya Tanzania na Msumbiji iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, nilitokea benchi nikaenda kufunga mabao mawili ambayo yaliipatia timu yangu ushindi,” anasema.

Anasema mchezo huo ulikuwa wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika, hivyo hawezi kuusahau mchango wake kwani kila aingiapo uwanjani humtanguliza Mungu ili kutimiza majukumu yake.


SIMBA, YANGA HAPANA

Mcha anasema hakuna asiyejua wala kufahamu ukubwa wa Simba na Yanga nchini kwa kuwa ndizo zilizobeba taswira ya soka la nchi, lakini hakuwahi kutamani kucheza moja kati ya timu hizo.

“Kiukweli kabisa kutoka ndani ya moyo wangu sikuwahi kutamani kucheza hizo timu. Kwanza zina mambo mengi sana, hata utulivu wa mchezaji kucheza ni kazi. Ndio maana niliamua kucheza timu nyingine,” anasema.


USHINDANI WA LIGI

Msimu huu wa 2021/22 ambao Yanga imekuwa bingwa ikiwa na mechi tatu mkononi umekuwa na ushindani mkubwa ambao unaifanya kila timu kupambana ili kupata matokeo mazuri.

“Kiukweli ligi ya msimu huu ngumu sana na ina tofauti kubwa na ligi ya msimu uliopita. Nahisi ni kwa sababu ya maboresho yaliyofanywa na wadhamini wakiwemo Azam Tv na wengine,” anasema.

“Hakuna mtu anayependa fedheha au kufedheheshwa mbele za watu, kwa kawaida ukicheza mechi na Yanga au Simba ni lazima ukamie kweli kweli la sivyo utadhalilika, hizo timu huwa zina wachezaji wenye ubora mkubwa tofauti na hizi timu zetu ndogo ndogo”


MAPORO LIGI KUU

Mcha anaunga mkono hoja ya wachezaji kutoka nje ya nchi wawepo nchini, lakini wakidhi vigezo wawe na uwezo mkubwa kuzidi wazawa ili kuongeza chachu na ushindani.

“Yanga na Simba ni timu kubwa lazima tuziheshimu. Kwa upande wangu napenda maproo wawepo kwenye ligi yetu wasizidi watano na hao watano wawe ni maproo kwelikweli wametimiza vigezo vyote,” anasema


ALIKOTOKA

Vialli ni mchezaji aliyezaliwa kwenye familia ya wanamichezo wawili baba marehemu Mcha Khamis na mama yake Wahida Seif Visiwani Zanzibar.

Alianza kucheza timu za mtaani kwao Zanzibar, baadaye alijiunga na timu ya Kwahani, Mbuyuni, Ras-el-kheimah, Miembeni, Azam, Ruvu Shooting na Dodoma anakocheza hadi sasa.

“Safari ya maisha yangu ya mpira ilianzia katika hizo timu na sikuwahi kujutia timu yoyote kwamba nilipita kwa makosa hapana, kila sehemu ni kwa uwezo wa Mungu mie kucheza.”