Prime
Usiyoyajua kuhusu uwanja wa Yanga utakaojengwa
YANGA imetangaza kuanza mchakato wa ujenzi wa uwanja wa mechi kupitia hafla ya kusaini makubaliano kati ya klabu hiyo na Kampuni ya GSM ambayo ndiyo iliyoshinda zabuni ya kujenga uwanja huo.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Yanga kumiliki uwanja, kwani awali klabu hiyo iliwahi kumiliki uwanja katika eneo hilo la Jangwani, Dar es Salaam yaliyopo makao makuu ulioitwa Uwanja wa Kaunda ambao miaka ya nyuma ulitumika kwa baadhi ya mechi za mashindano lakini kwa sasa utakuwa wa kisasa zaidi.
Uwanja wa Kaunda ulipotea kutokana na kuibuka kwa mafuriko ya mara kwa mara eneo la Jangwani kutokana na kufurika kwa maji ya Mto Msimbazi, na baada ya hapo zilipita ahadi mbalimbali za kujengwa kwa uwanja huo, lakini zilikwama huku viongozi waliopita wakionyesha ramani kadhaa.
Hivi sasa chini ya uongozi wa Hersi Said inaonyesha kwenda kutimia kutokana na hatua ambazo zimepigwa zikiakisi uhalisia wa kukamilika kwa ahadi hiyo ambayo ilikuwa ni moja ya ajenda ya uongozi wake wakati akiomba ridhaa ya kuiongoza klabu hiyo.
Yapo mengi umeyasikia kuhusu ujenzi wa uwanja huo ambao unatarajiwa kujengwa chini ya usimamizi wa GSM utakaochukua mashabiki 20,000, lakini haya ni mambo saba ambayo unapaswa kuyajua.
MUUNDO, JINA LA UWANJA
Jina la uwanja huo halitakuwa maalumu kwa klabu hiyo pekee, bali litaakisi makubaliano ya pande hizo mbili yaani Klabu ya Yanga na GSM kutokana na makubaliano ambayo wameingia.
Hii haitakuwa mara ya kwanza duniani ambapo klabu mbalimbali zimekuwa zikifanya hivyo, ikiwemo Atletico Madrid ambayo uwanja wake wa sasa unajulikana kwa jina la Riyadh Air Metropolitano ukiwa ni ubia na Shirika la Ndege la Riyadh, Saudi Arabia.
Hapo kabla uwanja huo ulikuwa ukibeba jina la Wanda Metropolitano, ambapo tena jina la Wanda lilikuwa la kampuni moja ya ujenzi iliyojenga uwanja huo kabla ya baadaye kubadilishwa na kupewa jina jipya kufuatia muda wake wa kimkataba kumalizika.
MARAIS SEHEMU YAO
Katika ramani ya uwanja huo hakutakuwa na eneo la VIP kama ambavyo imekuwa kwenye viwanja vingi, lakini Yanga imetaka kuwepo kwa majukwaa zaidi yakiwemo VVIP lakini ikaenda mbali zaidi kwa kuwa na chumba maalumu kitakachotoa huduma kwa ugeni wa marais uwanjani hapo.
KILA SHABIKI KITI CHAKE
Kwa mujibu wa Hersi ni kwamba, wakati mashabiki watakapokuwa wanaingia uwanjani kila tiketi itaonyesha kiti ambacho atakwenda kuketi na hakutakuwa na mwingiliano kama ambavyo imekuwa kwenye viwanja vingi hapa nchini.
Hii maana yake kuna uwezekano shabiki akanunua tiketi ya msimu mzima kwa mechi za nyumbani, lakini sio shabiki mmoja pekee, bali hata taasisi kununua tiketi kadhaa kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi au wateja wao.
UWANJA MMOJA
Katika eneo hilo utajengwa uwanja mmoja pekee wa mchezo na hakutakuwa na nafasi ya kujengwa mwingine hata mdogo wa mazoezi kulingana na ukubwa wa eneo hilo. Hii maana yake ni kwamba Yanga itatua hapo kwa ajili ya kucheza mechi na itakuwa na uwanja mwingine kwa ajili ya mazoezi, hatua ambayo itaupunguzia majukumu uwanja huo utakaochukua ukubwa wa eneo la mita za mraba 37,200.
NYASI ZA BERNABEU, SAN SIRO
Uwanja huo utakuwa na nyasi za kisasa zaidi ambapo zitawekwa aina ya ‘hybrid natural’ ambazo kwa sasa duniani zimekuwa zikitumika kwenye viwanja vikubwa zinazovutia kwa wachezaji na mwonekano kwa picha.
Nyasi hizo ni mchanganyiko wa nyasi asilia ambazo ndizo zinakuwa nyingi na bandia chache. Klabu mbalimbali duniani zimetumia kwenye viwanja vikiwemo vya Santiago Bernabeu unaotumiwa na Real Madrid ya Hispania, Camp Nou wa Barcelona ya Hispania na hata ule wa San Siro unaotumiwa na AC Milan na Inter Milan ya Italia.
REKODI AFRIKA
Yanga imetangaza uwanja huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 walioketi na kama itakuwa hivyo, basi utakuwa sawa na ule wa St Mary’s unaomilikiwa na Vipers ya Uganda katika viwanja vinavyomilikiwa na klabu Afrika.
St Mary’s ulijengwa 2017 ambao pia una viti 1,000 vya VIP, lakini ukiwa na eneo la kuchezea (pitch) lenye nyasi bandia. Kabla ya huo wa Yanga kujengwa ndio ulikuwa unashikilia rekodi ya uwanja mkubwa zaidi unaomilikiwa na klabu.
Nyuma ya St Mary’s unafuata Uwanja wa TP Mazembe ya DR Congo ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki walioketi 18,000 uliojengwa 2010, lakini ukafanyiwa ukarabati 2019 ukifuatia ule wa Kimataifa wa Enyimba unaochukua mashabiki 16,000.
VIWANGO CAF
Toleo la kisasa zaidi la uwanja bora Afrika kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika CAF linajulikana kama ‘category 4’ ambapo wa Yanga ukikamilika utakuwa na ubora huo ukichanganya na ‘category 3’ ambao utaibeba klabu hiyo.
Kama Yanga itafanikisha uwanja huo kuwa katika daraja hilo maana yake itaweza kuutumia katika michezo ya kimataifa hata ya mechi za CAF kutokana na kubeba mahitaji yote muhimu yanayohitajika kwa sasa. Viwanja vya daraja hilo hapa nchini havipo, lakini vipo kwenye mchakato wa kujengwa.