Ushirika Moshi iliupiga sana mwingi balaa!

KWA sasa mashabiki wa Simba wamekuwa wakipagawa na soka tamu linalopigwa na kina Luis Miquissone, Clatous Chama na Larry Bwalya, lakini asikuambie mtu kuna timu ilikuwa balaa enzi hizo, iliitwa Ushirika Moshi.

Baadhi ya mashabiki bila shaka wanaikumbuka. Timu moja matata iliyowahi kutikisa nchini kwa soka la kampa kampa tena, iliyokuwa ikimilikiwa na Chuo cha Ushirika Moshi.

Asikuambie mtu timu hii ilikuwa moto na iliupiga mwingi sana uwanjani, kiasi hizo Simba na Yanga zilisubiri kwao. Hata hivyo, bahati mbaya timu hiyo imepotea kwenye ramani, huku baadhi wakishindwa kuelewa kilichoiponza hata ikashuka daraja.

Mwanaspoti lilifunga safari ya zaidi ya kilomita 85 kutoka jijini Arusha hadi Chuo cha Ushirika, Moshi mkoani Kilimanjaro na kufanikiwa kuwakuta baadhi ya nyota wa zamani wa timu hiyo kipindi ikipanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu Bara).

Athuman Shunda, Kusiaga Kiata, Ruben Mwandambo na Jafar Kiango ni baadhi ya wachezaji walioipandisha timu hiyo na wamefichua kila kitu juu ya soka tamu kabla ya kushuka daraja na kupotea kwenye ramani ya soka nchini.


HISTORIA YA TIMU

Ushirika Moshi ilianzishwa mwaka 1982 ikiwa ni moja ya kuendeleza michezo kwa wafanyakazi wa chuo hicho na sio kushiriki ligi kubwakubwa kama ilivyofika na kuandika historia.

“Wakati huo mkuu wa chuo alikuwa Tasilo Mahuwi, baadaye akaja Suleiman Chambo na Raymond Kimaro akiwa mkuu wa utawala wote wakiwa mashabiki wakubwa wa michezo chuoni hapo na ndio walikuwa chachu ya timu kufika mbali,” anasema Shunda.


KASHFA UPANGAJI MATOKEO

“Baada ya kushiriki mashindano mengi na kupata jina sehemu mbalimbali, ndipo viongozi wa chuo wakaona vyema timu iwe rasmi kwenye michezo ili kushiriki ligi ya wilaya na hatimaye mkoani, hapo ndipo safari yetu ilianza rasmi,” anasema Kiata.

Baada ya kusota miaka mitatu ligi ya mkoa bila kupata mafanikio kwenda Daraja la Kwanza, ilifuzu michuano ya ligi ya kanda ambayo ingewapa tiketi ya Ligi Kuu, lakini likawakumba balaa.

Wakiwa kwenye michuano hiyo na harakati za kuipandisha timu, mwaka 1987 ilikumbwa na kashfa ya upangaji matokeo dhidi ya Ndovu ya Arusha, jambo lililokifanya Chama cha Soka Tanzania (FAT) kutopandisha timu yoyote kutoka kundi hilo.

Kundi hilo lilijumuisha timu za RTC Kigoma, Ndovu Arusha, Ushirika Moshi na Bandari Mtwara, jambo lililowakatisha tamaa wachezaji wengi wa timu hizo waliokuwa na kiu ya kuandika historia mbalimbali.


DARAJA LA KWANZA

Baada ya zengwe la 1987 lilowashutumu kupanga matokeo viongozi, wachezaji na benchi zima la ufundi la timu hiyo waliamua wasifanye kosa.

Mwaka 1988 wakiwa kwenye Ligi ya Kanda iliyofanyika Uwanja wa Sokoine - Mbeya sambamba na timu ya Mecco, Lidico, CDA, RTC Shinyanga na Sua, Ushirika ilipanda daraja sambamba na Mecco na kuuwasha moto mkali katika ligi hiyo ambayo kwa sasa ni Ligi Kuu Bara.

“Mecco iliongoza kundi letu, ila tulikuwa tumelingana pointi japo waliongoza kwa mabao, hapo ndipo ikawa mwanzo wa Ushirika kuwa na jina kutokana na soka safi lililowashangaza wengi nchini,” anakumbuka Kiango.


KIKOSI KAZI

Kwa mujibu wa kina Kiango, wachezaji walioandika historia isiyofutika Ushirika Moshi kucheza Daraja la Kwanza na kuupaisha Mkoa wa Kilimanjaro ni pamoja na Fanuel Singano, Bahatisha Ndulute na Nathaniel Haule wote wakiwa makipa. Mabeki ni Shaffih Nyangasa, Athuman Shunda, Kusiaga Kiata, Reuben Mwandambo, Juma Mahimbo, Said John, David Rogers, Emmanuel Sawala na Pascal Maingu ilhali viungo walikuwa John Haule, Poisant Moyo, Michael John, Nurdin Hussein ‘Mido’ na Andrew Kabisama.

Safu ya ushambuliaji iliundwa na Jafar Kiango, Omary Abbas, Julius Kalambo, Venance Mwakalukwa, Said Ngobe, Ally Maliva, Wazir Ally, Nico Ungani, Ernest Mponzi na John Makelele ‘Zigzag’. Benchi la ufundi lilikuwa chini ya mmoja wa makocha wa kwanza Tanzania kufundisha nje ya nchi, Dan Korosso akisaidiana na David Mwamwaja. Dan baadaye alitimkia zake Botswana kufundisha soka la kulipwa.

Baadaye timu hiyo iliwasajili wakali wengine kama kina Offen Martin, Willy Martin, Jimmy Mhango, Abdallah Seleman ‘Kaburu’, Humphrey Mgaza, Abuu Juma, Patrick Betwel, Charles Daffa, Wassi Kiango, Ally Bushiri, Shaaban Juma, Simon Masange, Rashid Kondo, Abdul Abbas na wengineo walioifanya izitetemeshe Simba na Yanga.


KILICHOISHUSHA

Baada ya kudumu Ligi Daraja kwa miaka saba tangu 1989 timu hiyo ilishuka daraja 1995 na kuanza kupotea taratibu kwenye ramani ya soka. “Timu ya Ushirika ilishuka baada ya kuja kwa sera ya mabadiliko ya kiuchumi mwaka 1992 ambapo mashirika ya umma yalianza kujitegemea, huku timu hiyo ilikuwa ikipata ruzuku kutoka serikalini na bajeti yetu ilikuwa zaidi ya Sh38 milioni kwa mwaka enzi hizo.”

“Baada ya kuona sera hiyo inawakaba huku timu haikuwa na kitega uchumi chochote ndipo Chuo kikaamua kuikabidhi Chama cha Soka mkoani Kilimanjaro (KRFA), ili iwe ya wananchi na hapo ndipo mambo yalipozidi kwenda mrama na hatimaye ilishuka daraja.

“Timu haziwezi kuendeshwa kwa mapato ya mlangoni, lazima kuwe na bajeti inayojulikana maana kuendesha timu ni gharama sio kama watu wanavyofikiria miaka ya sasa na kuanza kugombania madaraka.”


NINI KIFANYIKE

Wakizungumzia faida waliyotapa, Kiango anasema: “Michezo ina ushawishi mkubwa kwenye kila jambo na asilimia kubwa ya chuo ilitangazwa na timu ile, maana hata sasa tukienda mahali watu wanapoona gari limeandikwa jina la ushirika mtu anaanza kuulizia timu ipo wapi.

Mkongwe huyo anashauri mfumo wa zamani wa uendeshaji timu urejeshwe. “Mfumo wa zamani unatakiwa urudishwe wa kuhakikisha mashirika, shule, jeshi na kampuni wawe na timu za michezo, hilo ndilo litaweza kurudisha soka nchini maana timu nyingi za wanachama sasa hazina uwezo wa kujiendesha.

“Kuwe na mfumo wa kupandisha timu pamoja na namna ya kuendesha sio watu wachache wanajimilikisha timu ndio maana hata timu zinashindwa kufanya vizuri na hatimaye kufa.”