Uofisa habari wa timu si mipasho, vijembe

Uofisa habari wa timu si mipasho, vijembe

KIATIKA nchi zilizoendelea Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika klabu huambatanishwa na Idara ya Masoko.

Lengo kuu likiwa ni kujenga taswira ya uhusiano mwema na taasisi za kibiashara na kuleta mapato katika taasisi ya mchezo wa mpira wa miguu.

Pamoja na kutakiwa kujikita katika kuwekeza kwenye teknolojia na maendeleo chanya katika mitandao ya kijamii na kuongeza wigo na mapato kupitia ‘applications’ za klabu, ofisa habari anatakiwa kuielezea, kuizungumzia klabu kwa umakini ili walengwa washibishwe matarajio chanya na mustakabali mwema.

Ni lazima awe mwepesi wa kujenga taswira njema na wanahabari, vituo vya habari, klabu nyingine, taasisi za kibiashara na kusambaza habari zisizo na mawaa kwa jamii.

Pia moja ya kazi kubwa ni kuilinda klabu kwa zile habari zenye mrengo wa kutaka kuvuruga, kuchafua na kupeleka katika njia isiyo sahihi. Yeye ndiye mtetezi wa kwanza kwa kutumia hoja zenye mshiko zisizo za kuungaunga na aaminike katika yale anayoyaeleza.

Hata wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) enzi za Rais Leodegar Tenga kupitia Azimio la Bagamoyo lilipoamua hivyo, ilikuwa ni lengo zuri la kujenga taasisi ya soka yenye kuheshimika mbele ya wadau na jamii kwa ujumla.

Azimio la Bagamoyo lilitaka klabu kuajiri makatibu Wakuu badala ya kuendelea kutegemea wanaochaguliwa kupitia sanduku la kura.

Walitaka maofisa habari nao waajiriwe na kuachana na makatibu wenezi na pia walitaka weka hazina wapigwe chini na badala yake waajiriwe watu wenye taaluma zao ili kuepuka migororo na ubabaishaji uliokuwapo zamani.

Waliokuwa wakichaguliwa kwenye nafasi hizo hawakuzifanya kazi zao kwa ufanisi kwa vile walikuwa wakijitolea zaidi, licha ya majukumu makubwa ambayo kiasi kikubwa yalichangia kuzaa migogoro na baadhi kukosa uaminifu na uadilifu.

Maofisa habari, makatibu wakuu na wahasibu walituma maombi yao na pale wanapokidhi sifa kitaaluma kwa nafasi walizoomba waliajiriwa na kuanza kazi kwa kutegemea mkataba wa ajira na malipo yake kimasilahi. Kwa bahati mbaya ile dhima na lengo la Azimio la Bagamoyo ni kama imesahaulika hasa kwa upande wa maofisa habari wa klabu za soka.

Baadhi yao kama sio wengi wao wametoka katika maadili, weledi na taaluma za kazi zao (professionalism) na kuishia kutupiana mipasho na vijembe vya rejareja.

Hata mashabiki, wapenzi wa timu hizo ‘wanawatia ndimu’ ili kuweza kushindana baina yao. Katika hili la ushindani usio na tija wamekuwa wakiongopa katika baadhi ya taarifa zao ili kuwaridhisha wapenzi na mashabiki wa timu.

Kwa kufanya hivyo, mashabiki na wapenzi wamekuwa nao wakilishwa matango pori bila kujua na kufurahia hata kama wanachoelezwa sio cha kweli na pengine hakijawahi kutokea ndani ya klabu na kwamba ni vinginevyo.

Niwaombe viongozi wanaosaka maofisa habari watafute watu makini, weledi, walio na taaluma, na pia wafuatilie historia zao katika kazi kama hawakuwahi kuwa na mawaa.

Sio lazima mwandishi awe ofisa habari kwani vyuo vikuu vyetu vimetoa watu wengi wako mitaani wenye taaluma hiyo na sio mipasho.

Vingenvyo kwa jinsi inavyoonekana ipo siku malumbano au mipasho yao italeta dhahama kwa timu zao au mashabiki ama wao kwa wao, na natabiri anguko la mmojawao hivi karibuni kutokubalika katika maudhui na kujenga taswira mbaya kwa taasisi yake.

Hakuna asiyekumbuka miaka michache ya nyuma baadhi ya wasemaji wa klabu walifikia hadi kupopoana juu ya dosari zao za maumbile na kadhalika, kitu ambacho hakipo ndani ya soka ambalo ni mchezo wa kiungwana. Nimefikisha.

Tukutane wikiendi ijayo tutakapoangalia kwa kina fainali za Afcon 2021.