Prime
Unazikumbuka dabi hizi tano ziliopigwa Zanzibar?
Muktasari:
- Hii itakuwa mara ya sita kwa watani hawa kukutana kwenye fainali kwenye ardhi ya Zanzibar. Tunakuletea fainali zote zilizotangulia, na namna mambo yalivyokuwa.
WAKATI wa jadi wa soka la Tanzania, Yanga na Simba, wanakutana leo, Alhamisi, Unguja, Zanzibar kuwania Kombe la Muungano.
Hii itakuwa mara ya sita kwa watani hawa kukutana kwenye fainali kwenye ardhi ya Zanzibar. Tunakuletea fainali zote zilizotangulia, na namna mambo yalivyokuwa.
YANGA 2-0 SIMBA - 1975
Hii ilikuwa fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame), iliyofanyika Januari 13, 1975 kwenye Uwanja wa Amaan ambao ulitoka kuzinduliwa mwaka 1972. Simba waliingia kwenye mashindano hayo kama mabingwa watetezi baada ya kutwaa Kombe mwaka 1974 kwenye mashindano ya kwanza kabisa yaliyofanyika Dar es Salaam.
Mechi hii iliyoanza saa mbili na robo usiku, ilikuwa ya kwanza kwa Yanga na Simba kuchezwa usiku. Yanga ilishinda 2-0 kwa mabao ya Sunday Manara na Gibson Sembuli. Baada ya hii mechi, mgogoro mkubwa ukaibuka ndani ya klabu ya Simba kwa wanachama kumlaumu mwenyekiti wao, Hassan Haji, kwamba alitoa siri kwa Sunday Manara ili awafunge.
Sunday Manara, ambaye ni baba yake Haji Manara, alikuwa nyota wa Yanga aliyeoa binti wa Hassan Haji. Kabla ya fainali hii, Yanga na Simba walikutana kwenye fainali ya klabu bingwa ya taifa mwaka 1974 mjini Mwanza. Simba walifungwa 2-1, wafungaji walikuwa Sunday Manara na Gibson Sembuli.
Kwa hiyo Sunday alipofunga tena Zanzibar, wanachama wa Simba wakasema mwenyekiti wao amempa siri mkwewe...kwanini alikuwa hatufungi kabla hajaoa binti yako? Walihoji. Hassan Haji alipotoka Simba, akaenda kuanzisha Klabu ya Nyota Nyekundu.
SIMBA 1-1 YANGA (penati 6-5)
Watani wakakutana tena 1992 kisiwani Unguja kwenye Uwanja wa Amaan kuwania Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati. Kama ilivyokuwa fainali 1975, Simba waliingia kwenye mashindano hayo kama mabingwa watetezi kwa kushinda Kombe mwaka 1991 Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga, Syllersaid Mziray, alionyeshwa kadi nyekundu, akipinga kutolewa kwa kadi nyekundu beki wake wa kushoto, Kenneth Mkapa.
Simba walifunga bao la kuongoza kupitia Hussein Marsha, kabla Said Mwamba Kizota hajasawazisha. Matokeo yakabaki 1-1 hadi dakika 120 ndipo changamoto ya mikwaju ya penati ilipohusika. Simba wakashinda kwa penalti 5-4 baada ya David Mwakalebela wa Yanga kupoteza penati yake.
Katika mechi hiyo Joseph Lazaro wa Yanga alikataa kupiga penalti yake ndipo Mwakalebela alipotakiwa kuchukua nafasi yake. Wakati Mwakalebela anasimama, kipa wa Simba, Mohamed Mwameja, akaanza kushangilia na kuwahamasisha mashabiki wao washangilie pia.
Mwakalebela kuona hivyo, akaingia hofu, akakaa chini...akasimama na kukaa tena...akawa tayari ameshapoteza kujiamini. Alipopiga, Mwameja akaokoa... Simba wakawa mabingwa.
YANGA 0-1 SIMBA
Ilikuwa fainali ya Ligi Kuu ya Muungano. Hii ilikuwa mara ya pili kwa ligi hiyo iliyokuwa kuu Tanzania, kuchezwa kwa mtindo wa mtoano, baada ya 1990 pale Pamba ya Mwanza ilipocheza na Small Simba ya Zanzibar kwenye uwanja huohuo wa Amaan. Bao la tik tak la winga mfupi wa Simba mwenye asili ya Burundi, Damien Kimti likaitosha Simba kutwaa ubingwa.
SIMBA 2-0 YANGA
Ilikuwa Januari 12, 2011 pale watani wa jadi walipokutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi. Yanga waliingia kwenye mechi hii wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kwenye ligi kuu, kama ilivyo mwaka huu...na Simba walikuwa wamepoteza mechi moja tu, kama mwaka huu.
Dakika 90 za fainali, Simba wakashinda 2-0 kwa mabao ya Mussa Hassan Mgosi na mzambia Felix Sunzu.
SIMBA 0-0 YANGA (penalti 3-4)
Hii ilikuwa mechi iliyoanzisha safari ya makombe kurudi Jangwani baada ya kupotea kwa muda mrefu. Utawala wa GSM ulikuwa na mwaka mmoja klabuni Yanga na msimu mmoja uliotangulia, Engineer Hersi Said alitamba kwamba Yanga lazima watakuwa mabingwa wa ligi kuu, wasipokuwa basi aulizwe yeye. Ubingwa wakaukosa na maswali yakarudi kwake...akajificha kuyajibu. Hamad ndio ikaja fainali hii, Yanga wakataka kuitumia kuficha kilichotokea msimu uliopita. Wakashinda kwa penati 4-3 baada ya sare tasa ya dakika 120. Yanga wakalifanyia gwaride la heshima (parade) kombe lao kwenye mitaa ya Dar es Salaam waliporudi nalo.
KOMBE LA MUUNGANO 2026
Sasa wanakutana tena, nani kuibuka mshindi?