Ujenzi viwanja Zanzibar unakuja na neema
Muktasari:
- Mradi huo unatekelezwa kwa viwanja 17 katika wilaya 11 na mikoa mitano ya Unguja na Pemba, kati ya viwanja hivyo vinavyojengwa, 13 vimeshakamilika na vinne vinaendelea na ujenzi.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imewekeza Dola za Marekani milioni 51 (zaidi ya Sh132.3 bilioni) kwa ujenzi wa viwanja vya michezo vya Wilaya na Mkoa.
Mradi huo unatekelezwa kwa viwanja 17 katika wilaya 11 na mikoa mitano ya Unguja na Pemba, kati ya viwanja hivyo vinavyojengwa, 13 vimeshakamilika na vinne vinaendelea na ujenzi.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, anasema wizara hiyo imefanikiwa kutekeleza vipaumbele vyake kwa ufanisi zaidi.
Anaahidi kwamba Serikali itaendelea kuwawezesha wanamichezo kupitia makundi yao, ikiwemo michezo ya asili kama vile baiskeli, bao na karata.
Waziri Pembe anasema hayo yamechangia kuendeleza michezo kama nyenzo ya afya, ajira na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
“Ujenzi wa viwanja 17 vya Wilaya na Mikoa ambavyo utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 90, kati ya hivyo, viwanja 13 vimekamilika na viwanja vinne vinaendelea na ujenzi, haya ndio mafanikio ambayo tulikuwa tukiyalilia kwa muda mrefu sasa yamepatikana,” anasema.
Anaongeza kwamba, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Waziri huyo haishii hapo, bali anasema Serikali itaendelea kuimarisha viwanja na miundombinu ya michezo nchini ili kuongeza hamasa ya wananchi kushiriki michezo mbalimbali inayoandaliwa.
Januari 13, 2026, wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, akizindua Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, alisema Serikali ya Zanzibar imepata mafanikio katika kufanikisha ujenzi wa viwanja vya michezo katika kila wilaya pamoja na ujenzi wa viwanja vya mikoa.
Katika hotuba yake, aliipongeza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa viwanja hivyo huku akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza sekta ya michezo Zanzibar.
Machi 25, 2026 Serikali ya Mapinduzi kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo iliingia mkataba wa miaka 15 na Kampuni ya Bahari Leisure kuendesha viwanja vya michezo vilivyopo Unguja na Pemba.
Katika makubaliano hayo, Serikali ilieleza dhamira yake ya kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya michezo kupitia sekta binafsi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu wa Wizara hiyo, Ali Abdulgulam Hussein anasema lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha viwanja vya michezo vinaendeshwa kwa ufanisi na vinatunzwa kuleta tija kwa taifa.
Anaeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha michezo na kuongeza ajira kwa vijana na imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa baadhi ya viwanja vilikuwa havisimamiwi ipasavyo.
Kwa upande wake, Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar, Mohammed Makame anawataka wananchi kushirikiana na mwekezaji ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na serikali kupitia uwekezaji huo.
Pia anawahimiza wadau kutoa maoni yao kwa njia sahihi ili kuboresha zaidi huduma zitakazotolewa katika viwanja hivyo.
Mkurugenzi wa Bahari Leisure, Ibrahimshah Faisal Shahbhai anasema wamejipanga kuhakikisha viwanja hivyo vinaendeshwa kwa viwango vya kisasa na vinakuwa na huduma bora kwa watumiaji wote.
Anasema kwamba, kampuni hiyo itaweka mifumo madhubuti ya usimamizi, ratiba za matumizi na uimarishaji wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya wadau wa michezo.
Anaahidi kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma, hasa vijana na watu wenye mahitaji maalumu.
WADAU WAFUNGUKA
Licha ya Serikali kuchukua jitihada hizo, baadhi ya wadau wa michezo kisiwani hapa wametoa maoni juu ya uamuzi huo wa kumpa mwekezaji miaka 15 kuendesha viwanja hivyo.
Akitoa maoni hayo, Saidi Mohammed Khamis ‘Argentina’ anasema pamoja na umuhimu wa uwekezaji huo, bado kuna haja ya kuangalia maslahi ya wananchi waliokuwa wakitumia viwanja hivyo awali.
Anasema, gharama zinazotajwa kwasasa ni kubwa kwa wananchi wa kawaida na zinaweza kuwanyima fursa vijana wengi kushiriki michezo.
“Serikali inapaswa kuweka utaratibu maalum wa kuruhusu matumizi ya viwanja hivyo kwa gharama nafuu au bure kwa shughuli za kijamii na ukuzaji wa vipaji,” anasema Argentina.
Mohammed Rashid anasema uwekezaji huo ni mzuri lakini unapaswa kuzingatia upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwani viwanja hivyo vinapaswa kubaki kuwa mali ya umma.
Anapendekeza Serikali kuweka viwango maalum vya gharama vitakavyowawezesha hata timu za vijana na ligi ndogo kutumia viwanja hivyo kwa urahisi, ili kusaidia kukuza vipaji na kuendeleza michezo nchini.
Anasema Serikali inaweka mikataba yenye uwazi, masharti ya kijamii na mifumo ya udhibiti wa bei, uwekezaji wa aina hiyo unaweza kuleta mapinduzi katika sekta ya michezo bila kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini.
Hivyo, wadau hao wameiomba Serikali kuhakikisha kunakuwepo na uwazi katika utekelezaji wa mkataba huo, ikiwemo kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mapato, matumizi na mafanikio ya uwekezaji huo.