Uhuni wa mashabiki tatizo ni maofisa habari wa klabu

SOKA ni burudani. Soka ni furaha, amani na upendo. Soka na michezo kwa ujumla hujenga urafiki na kuleta suluhu ndani ya jamii.

Lakini kwa siku za karibuni kuna baadhi ya mashabiki wachache sio wastaarabu wametaka kugeuza soka kama vita, uhasama na uadui.

Ndio maana wikiendi iliyopita kwenye pambano la Simba na Asec Mimosas ya Ivory Coast lililopigwa Kwa Mkapa kuna baadhi ya mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga walifanyiwa fujo na kupigwa walipokuwa uwanjani.

Walipigwa na wanaodaiwa mashabiki wa Simba waliokerwa na wenzao hao kuwaunga mkono wageni. Baadhi waliopigwa walisikika wakilalamika kupigwa na kupoteza fedha na simu. Hilo ni tukio la aibu na lisilo la kiungwana hata kidogo.

Pia tukio hilo sio la kwanza kutokea nchini kwenye viwanja vya soka hususan vikiwahusisha mashabiki wa klabu kubwa nchini za Simba na Yanga. Ilishatokea msimu uliopita mjini Morogoro wakati Yanga ilipokuwa ikicheza na Mtibwa Sugar. Mashabiki wa Simba walishambuliwa Uwanja wa Jamhuri.

Ieleweke wazi kuwa vurugu michezoni ni suala lisilokubalika hata kwa namna yoyote na bahati mbaya kuna watu wanaoipanda mbegu hiyo ya chuki kwa kutumia nafasi zao za usemaji mara uhamasishaji na hata tamko rasmi la klabu ya Simba lililotolewa lilikuwa na umuhimu, ila lilienda nje kidogo kinyume kabisa na taaluma ya uhusiano ya umma.

Wakati pia mjadala ukihanikizwa kuhusu taarifa hiyo ukaibuka utetezi kuwa sio lazima kutumia maneno magumu kutoa karipio.

Ikafuatiwa na taarifa rasmi ya klabu ya Yanga kulaani tukio hilo na ilikuwa imejitosheleza kabisa kwenye kuelezea msimamo wao na wakatoa mapendekezo ya dhahiri kuwataka wanachama wao na mashabiki kutofanya vurugu zozote za kulipiza kisasi. Ilikuwa imeshiba na ilionyesha udhaifu wa kitengo cha mawasiliano cha watani zao ambao walisema wanatumia maneno laini. Unatumiaje maneno laini kwa mtu asiye muungwana? Ikiwa ameshindwa tu kustahamili kwa mwenzake ataelewa hayo maneno laini? Ni ajabu na kweli.

Msemaji wa klabu husika na mambo yanayohusu klabu yako kuzungumzia klabu isiyo yako kwa timu nyingine kuwa msifanye hivi na vile kwa kuwapa michongo ili timu ya nyumbani ifungwe ni kukosa maadili. Ni kinyume na taaluma. Ni kuweka chuki kati ya mashabiki nando jambo tunalopitia kwa sasa. Hivi pilipili usiyoila yakuwashia nini? Izungumzie timu yako bila kuwachombeza watani wako. Ndivyo wasemaji wa timu hizi wanavyofanya ama kuja uwanjani kushangilia si vibaya ila maneno ya kejeli na matusi wanapokutana mashabiki hawa uso kwa uso ndo huleta shida maana wengine sio wavumilivu.

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa)limekuwa na kampeni nyingi za kuhamasisha uhusiano mwema michezoni na walikuja na kampeni kama ‘football for all’ na ‘inclusive football’ ambazo zote zilikusudia kusema mchezo wa mpira wa miguu ni wa watu wote duniani wala hakuna anayestahili kuamini ana uhalali sana wa mpira kuliko mwingine. Hii tabia ya kuwapiga watu tunaotofautiana nao kimtazamo ama kishabiki ni ya ovyo inayopaswa kujibiwa na hawa wanaoitwa wasemaji.

Juzijuzi tu kwenye mchezo baina ya klabu ya Leicester City dhidi ya Nottingham kule England kuna mchezaji alipigwa na chupa na mashabiki wote waliohusika na tukio hilo wamefungiwa maisha na klabu yao kuingia viwanjani kwa kutozingatia usalama wa wanamichezo wengine. Sisi bado tunapozana tu wakati huu ambao timu zetu hazioni thamani ya shabiki uwanjani wenzetu wanalilia mashabiki kurudi uwanjani na bado tumeendelea kuwapuuza wanaolipa viingilio vyao kwa kuwapiga.

Tukiwafukuza hawa mashabiki ni kwa faida ya nani? Kwa nini tusiwaruhusu wakae kwa amani kisha tuzifunge timu zao na tuwazomee kimchezo? Wakiondoka uwanjani faida ni ipi? Wakati ambao kuna kundi kubwa la kinadada na wanawake viwanjani leo tunapigana? Kwa wasivyopenda bugudha mnadhani watakuja tena? Tutawakumbusha kazi zenu mpaka lini?

Muungwana hubadilika. Maofisa uhusiano kwa umma hapaswi kuwa sehemu ya vurugu. Acheni mzaha wa kucheza na roho za watu. Tusisubiri mpaka watu wapoteze maisha uwanjani ndo tuanze kulaani kwa lugha kali ama kuwadhibiti wanaoieneza hii chuki kwenye mpira wetu.

Kama utani wa jadi umewashinda achaneni nao ila msipandikize uadui kwa kivuli cha utani wa jadi.

Ni aibu tupu! Naamini mamlaka za soka nchini zitachukua hatua stahiki mapema na ukimya wao kwenye hili naamini sio kuwa wamelipuuza labda bado wanatafakari njia sahihi ya kuja nayo ingali walipaswa kutoa taarifa rasmi ya kulaani suala hili kama ambavyo klabu ya Yanga angalau ilitoa taarifa yenye weledi mkubwa na yenye kuzingatia uhitaji wa taaluma.