UCHAMBUZI: Uchaguzi Mkuu TFF na umakini wa wajumbe kuchagua

Friday June 11 2021
tff pic
By Mwanahiba Richard

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika Agosti 7 mwaka huu na utakwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo.

Hivyo matukio hayo yote mawili yatafanyika jijini Tanga ambapo mara ya mwisho ilikuwa jijini Dodoma ambako Wallace Karia alichaguliwa kuwa rais wa shirikisho hilo.

Hivi sasa wagombea wameanza kuchukuwa fomu na Karia alikuwa mgombea wa kwanza kuchukuliwa fomu na Swedy Mkwabi kwani yeye alikuwa kwenye majukumu mengine huko Kanda ya Ziwa.

Karia hajarudisha fomu na tunatarajia kwamba atarudisha mwenyewe tofauti na alivyochukuliwa na wapambe wake, lakini tayari amepata wapinzani wa nafasi hiyo anayoitetea kwa miaka minne mingine ijayo.

Sitaki kuelezea zaidi nini Karia amekifanya kwa kipindi cha miaka minne anayomaliza, ila mambo yapo wazi kwenye mafanikio na changamoto zote zilizotokea kwa kipindi chake.

Kwa kipindi hiki ambacho wagombea wameanza kuchukuwa fomu kuna mambo mengi yatafanywa na Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo ikiwamo urudishaji, usaili, pingamizi hadi kufikia hatua ya kuanza kampeni ambayo inakuwa hatua ya mwisho kabisa.

Advertisement

TFF hii inalalamikiwa sana kutokana na utendaji wao wa kazi lakini hata TFF iliyopita chini ya Jamal Malinzi nayo ilikuwa ikilalamikiwa pia isipokuwa ile ya Leodegar Tenga ambayo hata kama kulikuwa na malalamiko yalikuwa machache si kama hizi awamu mbili, Malinzi na Karia.

Hawa wanalalamikiwa mno kwa madai kwamba utendaji wao unaonyesha waziwazi kuzibeba timu ambazo wanazishabikia, yawezekana ama isiwezekane maana hayo ni maono ya wadau wa soka hasa wale wanaoguswa moja kwa moja na shirikisho hilo.

Wanakwenda kwenye uchaguzi, kampeni zitafanyika, kila atakayeingia kwenye mkutano mkuu atakuwa na nafasi ya kupiga kura sasa ni juu yao kuchagua kiongozi atakayelalamikiwa tena ama kuchaguwa kiongozi mwenye sifa kama za Tenga.

Tenga alipita na sifa zake bora, hata atakayechaguliwa awamu hii hata kama hatakuwa Karia sijui kama ataweza kufanana moja kwa moja na utendaji kazi wa Tenga, maana si jambo jepesi katika miaka ya sasa kupata mtu wa hivyo. Hivi sasa wengi wana mapenzi yao ambayo hawawezi kuyaficha hadi watu kutambua moja kwa moja walivyo.

Wapiga kura siku zote ndiyo wanaochagua nani awaongeze, sasa ni juu yenu maana mnachagua kwa uoga halafu mnakuja kulalamikia koridoni, hicho kitu ni kibaya sana kwani tayari mnakuwa mmefanya uamuzi ambao utadumu kwa miaka minne ijayo.

Umakini, msimamo wenu ndiyo utawapa kiongozi bora na si bora kiongozi ambaye mnaona kabisa hatatenda haki juu yenu ila mnamchagua kwasababu tu labda mnamuonea aibu au kuogopa urafiki kuvunjika.

Kama hamtamhitaji Karia arudi madarakani basi ni kuamua sasa na sio mnamchagua halafu baadaye mnalalamika, fanyeni uamuzi sahihi sasa ili mkitoka hapo lawama zisiwepo, kwani Karia ni binadamu ana udhaifu wake na hata nyie mnaochagua mna udhaifu wenu, hivyo udhaifu huo usijekuleta tatizo la lawama hapo baadaye.

Ni tahadhari tu pia kama itazingatiwa kwamba hata wakati wa kampeni za wagombea, kila mmoja atajinadi basi sikilizeni angalieni kama ahadi zake kweli zitaweza kutekelezeka kwa miaka minne ijayo maana sio kuwa kampeni za kupiga porojo tu.

Waweke mipango ambayo inatekelezeka na endelevu katika soka, sio kutoa ahadi za kuwarubuni tu wanachama wao, hili wanachama na wapiga kura mnapaswa kulikataa. Porojo hazikubaliki kwenye soka maana soka sio siasa, mwenye porojo afyekwe tu bila kuoneana aibu.

Wagombea pia wafanye kampeni zenye tija na sio kupakana matope, propaganda zitupwe kule huku iwe vitendo tu, kupakana matope ndiko huko kunakotengeneza chuki ambazo zinawafanya wengine wasionekane viongozi bora.

Advertisement