UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna matajiri wengi, halafu kuna Bakhresa mmoja tu

Muktasari:

KAMA tunatakiwa kutengeneza sanamu ya heshima kwa watu wenye mchango mkubwa kwenye kukuza soka la Tanzania, mimi nampendekeza Said Salim Bakhresa.

KAMA tunatakiwa kutengeneza sanamu ya heshima kwa watu wenye mchango mkubwa kwenye kukuza soka la Tanzania, mimi nampendekeza Said Salim Bakhresa.

Huyu mzee kiboko sana, ni moja kati ya matajiri wachache ambao wanalipa heshima kubwa sana soka letu, ni moja kati ya watu wachache sana wanaoongeza thamani ya soka letu kila kukicha.

Ni kweli anafanya biashara lakini analisaidia pia, thamani ya ligi yetu inazidi kupanda ni kwa sababu ya Bakhresa.

Tunapata pesa nyingi sana sio kwa sababu ligi yetu ni bora kihivyo, ni kwa sababu yupo Mzee Bakressa, bado nazikumbuka Bilioni 225.6 alizoweka kwenye udhamini wa haki za matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu Bara.

Unadhani ligi yetu ina thamani hiyo? Labda jibu ni ndiyo, labda jibu ni siyo, lakini, tunaye Bakressa, hakuna tunachokosa, hakuna tunachopungukiwa. Bilioni 225.6 sio pesa ya kawaida, sio pesa ya mchezo kuweka kwenye soka letu huu ambao hata ratiba bado inakosewa kila siku.

Sio pesa ya kitoto kwenye ligi ambayo Waamuzi wanashindana kufanya makosa kila wikendi, ukipanga urefu wa sifuri za Bilioni 225.6, zinaweza kutoka Dar es Salaam mpaka nyumbani kwetu Kaliua, ni pesa nyingi mno kwenye ligi ambayo mshika kibendera anainua tu pale anapojisikia kufunya hivyo uwanjani.

Siku chache zilizopita, Yanga na Mzee Bakhresa wameingia tena mkataba wa Bilioni 41, huu ni ushindi mwingi sana kwa Yanga, huu ni ushindi mwingi sana kwa Azam Media.

Siku hizi bilioni ni rahisi sana kuisikia kwenye soka letu kwa sababu ya uwepo wa Bakhresa, unadhani Yanga wana thamani hiyo kwenye maudhui? Labda jibu ni ndiyo, labda jibu ni siyo, lakini, Bakhresa ameweka mzigo.

Kuweka bilioni 41 kwa timu ambayo inakwenda mwaka wa nne bila Kombe la Ligi Kuu sio jambo dogo, kuweka Bilioni 41 kwa timu ambayo haina uhakika wakufika hata hatua ya makundi kwenye michuano ya Afrika, sio jambo rahisi.

Uwepo wa Mzee Bakhresa ni faida kubwa sana kwenye soka letu, ni kweli Yanga wana watu wetu sana nchini lakini, ni kweli pia hawafanyi vizuri uwanjani katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni.

Bilioni 41 inapaswa kwenda kuibadilisha Yanga, Bilioni 41 inakwenda kuwasaidia sana viongozi na hasa kwenye gharama za uendeshaji wa Klabu.

Ni kweli wapo matajiri wengi waliowahi kuusaidia mpira wetu, ni kweli wapo watu wengi wanaostahili heshima kubwa sana kwenye kukuza soka letu lakini kwa zama hizi, Bakhresa anastahili kupewa heshima, ameongeza thamani kubwa sana ya soka letu.

Tuko kwenye kipindi ambacho mikataba ya biashara ikiisha, watu wanajishauri kuongeza kutokana na Janga la Covid-19 lakini Mzee Bakhresa anazidi kumimina tu pesa tu kwenye soka letu.

Tuko kwenye kipindi ambacho biashara nyingi ndiyo zinaanza kurejea baada ya mtikisiko wa Covid-19, lakini Bakhresa anatujaza tu mapesa. Sio jambo Dogo, sio jambo rahisi.

Zamani Bilioni 23 ilitosha kununua haki za matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu Bara kwa miaka mitano, leo Yanga peke yake inauza maudhui yake kwa Bilioni 41.

Huyu Mzee anatupa heshima kubwa sana kwenye soka, tuna deni bado anatudai, kuna deni kubwa inabidi tumlipe, umefika wakati sasa wa kuonyesha thamani ya Bilioni 225.6 za udhamini wa haki ya matangazo ya Televisheni ionekane uwanjani.

Umefika wakati thamani ya Bilioni 41 za udhamini wa Yanga tuione uwanjani, ligi yetu inapaswa sasa kuimarika ili tuione nguvu ya Bilioni 225.6 uwanjani.

Ni muda wa kuona miundombinu yetu ya soka inafanana na pesa hizo, ni muda wa kuona aina ya wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu Bara nao wanafanana na Bilioni 225.6.

Tabia ya kuleta wachezaji wa kigeni waliochoka, inabidi ifike mwisho, tabia ya kuleta wachezaji wa kigeni kuja kustaafia soka Tanzania, inabidi ikome mara moja kwa sababu tuna Bilioni 225.6 za Bakhresa.

Ni kweli Simba na Yanga wana mashabiki wengi wa asili yetu kila kona ya nchi lakini, klabu zingine zinatakiwa kuiona hii fursa ya dili la Yanga.

Coastal Union pamoja na kusua sua kwenye ligi lakini wana watu, ni moja kati ya klabu zenye ushawishi mkubwa mno pale mkoani Tanga.

Ni muda wa kuongeza thamani ya maudhui yao na kumfuata Mzee Bakhresa, Mbeya City pamoja na wao kusuasua uwanjani lakini wana mashabiki wengi sana pale mkoani Mbeya.

Ni muda wa kuongeza thamani ya timu yao na kwenda kumwona Mzee Bakhresa, uzuri wa Dunia ya leo kila kitu kinaweza kugeuzwa na kuwa pesa, ni wewe tu, kila Klabu inaweza kutajirika.

Mapinduzi ya Teknolojia yasituache nyuma, kila kitu ni pesa, ni kweli kuna matajiri wengi kwenye mpira wetu, nawaheshimu sana.

Ni kweli watu wengi sana wamewahi kumwaga pesa kuongeza thamani ya ligi yetu. Kuongoza thamani ya klabu zetu lakini, achana na mtu anaitwa Bakhresa, ni hatari.

Hizi pesa anazotoa, zikalete utofauti uwanjani, hizi pesa anazomwaga, zikatuletee wachezaji wa kigeni wa ukweli.

Imeandikwa na  OSCAR OSCAR maoni: 0789 784 858