Ubabe huko RCL ukipigwa tu umeachwa!

LIGI ya Mabingwa wa Mkoa (RCL) inafikia tamati leo hatua ya makundi ambapo timu mbili kutoka kila kundi zitapenya kwenda hatua ya nane bora ambapo huko zitaendelea kuonyeshana ubavu.

Timu mbili zitakazofika hatua ya fainali zitakuwa zimejihakikishia kucheza First League msimu ujao wakati timu nyingine mbili za First League zikishuka kwenda Ligi Daraja la Tatu ngazi ya Mkoa.

Tayari Njombe Mji imeshashushwa kutokana na kushindwa kuendelea na ligi hiyo sababu kubwa ikitajwa na mabosi wao ni ukosefu wa fedha wa kuiendesha timu.

Msimamizi wa kituo Katavi, Joel Balisija anasema kulingana na kalenda ya mashindano hayo michezo ya nane bora itaanza kuchezwa Aprili 13 huku kituo kimoja kati ya vinne vinavyotumika sasa kitachaguliwa kwaajili ya nane bora.


VITA KALI
Kocha wa Buhaya FC, Said Masoud anasema ligi imekuwa na upinzani mkubwa kwenye kundi lao sababu timu nne zipo kwenye nafasi nzuri ya kupata nafasi ya kwenda hatua inayofuata.

"Michezo ya mwisho ndio itakayotoa taswira nani atakwenda hatua ya nane bora kutokana na ushindi ambao tutakua tumeupata maana bila hivyo unaweza ukakwama dakika za mwisho.

"Tumejipanga kukabiliana na timu yeyote katika hatua hii na huko tuendako sababu maandalizi tumeyafanya vyema tangu mwanzo wa msimu na kila mmoja anajua kipi kinatakiwa kufanywa," anasema Masoud.

Mwenyekiti wa Bus Stand, Elias Mashaka anasema watapambana hadi dakika ya mwisho kupigania nafasi ya kwenda kwenye nane bora licha ya ushindani unaoonekana kwenye kundi lao.

Katibu wa timu ya Buhaya FC, Edson Charles kwa upande wao anasema moja ya vitu vinavyowafanya kuhakikisha wanafanya vyema ni mashabiki wao ambao wamekuwa sambamba kila wakati.

"Sisi ndio wenyeji wa kundi letu hivyo tunakila sababu ya kuwapa raha mashabiki wetu kwa kuendelea kupata ushindi kwenye michezo yetu iliyosalia ili kuona tunasonga mbele."


MAKUNDI
Upande wa kundi A ipo timu ya Buhaya (Kagera) ambayo itakuwa wenyeji ikiwa pamoja na timu za Shilabela (Geita), Mapinduzi (Mwanza), Nyamongo (Mara), Damali (Simiyu), Nyumbu (Pwani) na Eagle ya Dar es Salaam.

Kundi B, Aglo Sports Academy itakuwa mwenyeji mkoani Kigoma na Mambali Ushirikiano (Tabora), Singida Cluster (Singida), Arusha City (Arusha), Tanesco (Kilimanjaro), Kiluvya (Dar es Salaam) na Kilosa ya Morogoro.

Maila Boys itakuwa mwenyeji kwenye kituo cha Shinyanga ikicheza na Bus Stand (Dodoma), Aca Eagle (Manyara), Eagle Rangers (Tanga), Sharp Lion (Lindi), Mbuga (Mtwara) na Navy FC ya Dar es Salaam.

Malimao wao watakuwa nyumbani mkoani Katavi kwenye kundi D ikiwa na THB (Rukwa), Hollwood (Songwe) KFC (Mbeya), Ilula Tigers (Iringa), Zamalek (Njombe) na Mbinga United ya Ruvuma.


 

MSIMU HUU
Mbinga United ilianza kuchafua hali ya hewa kutokana na kushindwa kwenda kwenye kituo chao  sababu kubwa ni kushindwa kufanya maandalizi mazuri ya msimu.

Mbinga United ilipangwa Kundi D kituo cha Katavi pamoja na Malimao ambao ndio wenyeji, THB (Rukwa), Hollwood (Songwe) KFC (Mbeya), Ilula Tigers (Iringa) na Zamalek ya Njombe.

Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Wilaya ya Mbinga, Ahmed Mwalimu anasema timu hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo maandalizi yao hayakuwa mazuri kwaajili ya kwenda kwenye mashindano hayo.

Anaongeza pamoja na maandalizi lakini ukosefu wa fedha ndio uliosababisha mabingwa hao wa Mkoa wa Ruvuma kushindwa hata kufanya usajili wa wachezaji ndio maana haikuweza kujitokeza kituoni.

"Ninachopenda kushauri timu zetu kuwa na maandalizi hasa pale zinapokuwa na lengo lao la kupiga hatua kwenye soka sababu walifanikiwa kutwaa ubingwa lakini mwisho wa siku hakuna kilichofanyika.

"Timu zinatakiwa kuwa na watu ambao watawashika mkono katika kuendesha mambo yao kwa kuwashirikisha wadau ambao kimsingi ndio wenye mpira wao lakini pekee yako huwataweza kupiga hatua," alisema Mwalimu.

Msimamizi wa kituo hicho, Joel Balisija anasema Mbinga United ilipaswa kuanza ligi kwa kucheza na Malimao lakini wakapaswa kubadilisha ratiba dakika za mwishoni kutokana na kushindwa kufika kwa timu hiyo.


RATIBA
Michezo ya leo Kundi A' Eagles itacheza na Geita Academy, Mapinduzi na Nyamongo, Kundi B Singida Cluster itacheza na Kilosa huku Mambali itaikaribisha Kiuluvya.

Huko Kundi C Mbuga itakipiga dhidi ya Navy, Bus Stand itakipiga na Rangers wakati Kundi D Sodeko itacheza na Zamalek huku Hollywood na THB.