Timu za VPL ziendelee kutoa nafasi kwa wachezaji vijana

Muktasari:

Ni wazi kwamba msimu huu, ushindani umekuwa mkubwa kuliko msimu uliopita. Timu nyingi zimejiandaa vizuri kwa msimu huu wa mashindano kuliko msimu uliopita.

LIGI Kuu Bara inaendelea kushika kasi kila siku. Mpaka sasa imefikia mzunguko wa 10 huku Simba ikiongoza kwa alama 22.

Ni wazi kwamba msimu huu, ushindani umekuwa mkubwa kuliko msimu uliopita. Timu nyingi zimejiandaa vizuri kwa msimu huu wa mashindano kuliko msimu uliopita.

Maandalizi haya yalianzia katika usajili, kisha mazoezi makali kabla ya msimu pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki. Karibu kila timu ya Ligi Kuu ina ubavu wa maana msimu huu.

Ukiachana na Ruvu Shooting iliyolazimika kucheza mizunguko 10 ndipo ipate ushindi wa kwanza, timu nyingi zimeonekana kuwa na kitu cha tofauti.

Ushindani umekuwa ni mkubwa katika nafasi za juu hadi chini. Katika nafasi za juu, timu tano za Simba, Azam, Yanga, Mtibwa Sugar na Singida United zinaonekana kupambana vikali. Mpaka sasa tofauti ya alama kati ya anayeongoza ligi na aliyeko nafasi ya tano ni alama tano tu.

Ni tofauti na ligi nyingine ambazo vinara wa ligi wanaongoza kwa alama nyingi. Mfano kwenye Ligi ya England, vinara Manchester City wameachana alama 12 na Liverpool iliyoko nafasi ya tano. Vivo hivyo kwa Hispania, Barcelona iliyoko nafasi ya kwanza imepishana alama 12 na Sevilla iliyoko nafasi ya tano.

Kwa VPL, inathibitisha kwamba kuna kitu kimeongezeka msimu huu. Timu zinapata wakati mgumu kushinda mechi zao nyumbani na hata ugenini. Mfano, Mtibwa ilikubali kipigo nyumbani kutoka kwa Kagera Sugar juzi Jumapili. Inastaajabisha kidogo.

Pamoja na ushindani huo, tunaendelea kutoa rai kwa timu za Ligi Kuu kuwatumia wachezaji vijana zilizowasajili na siyo kila mchezo kujaza wakongwe tu.

Kikanuni kila timu inatakiwa kusajili vijana watano katika kikosi chake cha wachezaji 30, japo pia inaruhusiwa kuwatumia vijana wengine waliopo katika kikosi chao vijana chini ya miaka 20.

Imekuwa ni utamaduni kwa misimu kadhaa sasa timu hizo kushindwa kuwapa vijana hao nafasi hata kama wana vipaji vikubwa.

Tatizo kubwa limekuwa kwa timu za Simba na Yanga ambazo zinacheza kwa presha kubwa kila mchezo hivyo kutoa fursa ndogo kwa vijana.

Msimu huu, si Simba wala Yanga ambayo imetoa kipaumbele kwa vijana.

Licha ya Simba kujitahidi kuwatoa vijana kadhaa kipindi cha nyuma, awamu hii wameacha kabisa kuwatumia.

Yanga bado imeendelea kumtumia Yusuf Mhilu kama kijana kutoka timu yao ya B lakini kiuhalisia ni kama ameshavuka umri huo.

Azam kwa upande mwingine imejitahidi katika kutoa nafasi hiyo. Tumeona wachezaji kama; Yahya Zayd, Paul Peter, Swalehe Abdallah na wengineo wakipata nafasi katika kikosi chao.

Lipuli ya Iringa imekuwa mfano mzuri kwa kutoa nafasi kwa mchezaji mdogo zaidi. Karibu kila mchezo Lipuli imekuwa ikimpanga, Zuberi Ada ambaye mwaka huu alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Ada bado hajatimiza miaka 18 lakini amekuwa na mwendelezo mzuri kila mchezo kutokana na kocha Selemani Matola kamwamini na kampa nafasi.

Hakuna shaka kwamba katika miaka miwili ijayo, Ada atakuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars.

Siku zote hakuna ujanja katika soka. Wachezaji vijana ndiyo msingi wa nchi na wanatakiwa kusaidiwa.

Tunafahamu kwamba haiwezekani kwa timu kuwapanga vijana wote kwa pamoja, lakini itapendeza kama watatoa nafasi kwa mchezaji mmoja ama wawili ili kuwainua.

Tunapenda kuzikumbusha timu za Ligi Kuu kwamba mastaa wa baadaye wa nchi hii wapo mikononi mwao, hivyo waendelee kuwapa nafasi vijana hao na matunda yake yataonekana.

Hakuna mafanikio ya soka kama hakuna eneo la vijana.

Bado tunauangalia mchezo wa juzi wa Yanga na Mbeya City, wachezaji wengi vijana waliachiwa dimba, pamoja na kasoro za Mbeya City, lakini walionyesha wanaweza.

Wachezaji na wao wanatakiwa kujituma kuonyesha kuwa wanaweza. Haiwezekani mchezaji unapewa nafasi, lakini unashindwa kuonyesha kuwa walikuona na matokeo yake kocha anashindwa kukuamini katika kikosi cha kwanza. Mafanikio hayaji kama mvua, mchezaji kujituma.