Tausi FC ilivyokuja na mipango tofauti Ligi Kuu ya Wanawake
Muktasari:
- Tausi FC imeamua kubadili mwelekeo wa soka la wanawake nchini kwa kuweka nguvu kubwa katika ukuzaji wa wachezaji na badala ya kuwekeza fedha nyingi katika kusajili nyota waliokwisha tengenezwa, imeamua kuwekeza katika kuwanoa chipukizi na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
WAKATI vigogo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Simba Queens, Yanga Princess na JKT Queens zikiwania nafasi ya kuchukua ubingwa, Tausi FC iliyopo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi yenyewe imejikita katika kukuza na kuuza vipaji vya wachezaji.
Tausi FC imeamua kubadili mwelekeo wa soka la wanawake nchini kwa kuweka nguvu kubwa katika ukuzaji wa wachezaji na badala ya kuwekeza fedha nyingi katika kusajili nyota waliokwisha tengenezwa, imeamua kuwekeza katika kuwanoa chipukizi na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
Lengo kuu la mkakati wao ni ni kuzalisha wachezaji watakaouzwa katika masoko ya kimataifa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa halijazoeleka katika soka la wanawake Tanzania.
Ikumbukwe huu ni msimu wa kwanza wa timu hiyo kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake ikipanda daraja kutoka ligi ya mkoa na ilikuwa mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza baada ya kuichapa Bilo Queens mabao 3-0 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana Mwanza.
Kwenye michuano hiyo, Tausi zamani ikiitwa Ukerewe Queens iliandika rekodi ya kutopoteza mechi hata moja na ikiwa timu pekee iliyokuwa na kocha wa kigeni na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Mwanaspoti limekuchambulia mikakati ya timu hiyo, namna itakavyonufaika na changamoto zake kama haitakuwa na muendelezo mzuri.
MKAKATI ULIOPO
Taarifa zinaeleza Tausi FC ipo kwenye mchakato wa mwisho wa kuingia makubaliano na moja ya klabu kutoka Hispania na endapo yatakamilika, yatafungua milango kwa wachezaji wa klabu hiyo kupata nafasi ya kucheza katika ligi za Ulaya.
Kutokana na mkakati huo wa muda mrefu, Tausi FC haionekani kuweka kipaumbele kikubwa katika mbio za ubingwa wa WPL na tayari imemuuza nyota wa Burkina Faso, Adama Congo mwanzoni mwa msimu huu kwenda Dux Lugrono ya Hispania, timu aaliyowahi kukipiga Mtanzania Clara Luvanga kabla ya kutimkia Al Nassr ya Saudia.
“Sisi tunalenga mustakabali wa wachezaji kimataifa kwa sababu siyo kwamba Tanzania hatuna vipaji, vipo na hao ndio wanapaswa kwenda nje kuleta changamoto na unaona tumesajili wachezaji kisha tukawauza,” anasema Amos Mlandali kutoka Idara ya habari ya timu hiyo.
Kitaalamu, mkakati huo una maana kubwa. Katika soka la kisasa, hasa Ulaya na Amerika Kusini, klabu nyingi zinaingiza mkwanja mkubwa kutokana na biashara ya wachezaji. Klabu kama hizi huwekeza katika akademi, huendeleza vipaji na hatimaye huwauza kwa bei kubwa.
Faida ya mkakati huo ni nyingi. Kwanza, unawapa wachezaji motisha ya ziada. Mchezaji anapojua kuwa klabu yake ina mtandao wa kumfikisha kimataifa, anakuwa na sababu kubwa ya kujituma zaidi mazoezini na kwenye mechi.
Pili, mkakati huo unaweza kusaidia kuongeza ushindani katika timu, kwani kila mchezaji atapambana kuonyesha uwezo wake ili kupata nafasi ya kuonekana na mawakala au klabu za nje.
Faida nyingine ni kuwa msaada kwa timu ya Taifa, kwani watakaopata nafasi ya kucheza nje watajifunza mbinu mpya, nidhamu na uzoefu wa kimataifa ambao utasaidia timu ya wanawake (Twiga Stars) kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa. Hivyo, ingawa Tausi FC inaweza isishinde ubingwa lakini mchango wake unaweza kuonekana kwenye mafanikio ya taifa.
CHANGAMOTO
Moja ya changamoto kubwa ni udhibiti wa kikosi. Ikiwa klabu itakuwa inauza wachezaji wake bora mara kwa mara, inaweza kushindwa kujenga timu imara ya ushindani katika ligi. Hali hii inaweza kuathiri matokeo ya timu.
Mfano katika msimu mmoja, timu hiyo imeuza wachezaji wawili muhimu kipa Ruth Aturo aliyetimkia Simba Queens na Adama Congo ambao wote walikuwa wachezaji muhimu kwani ndio walioipandisha timu hadi ligi kuu.
Pia, kuna changamoto ya kifedha na kiutawala. Kufanikisha mpango wa kupeleka wachezaji nje kunahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu, mafunzo bora na usimamizi wa kitaalamu.
“Ndiyo maana hapa tuna makocha kutoka nchi mbalimbali, lengo ni kuhakikisha wachezaji wanapata mafunzo na mbinu mpya kutoka kwa makocha walioendelea kisoka duniani.”
Kwa upande mwingine, mkakati huu unaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika soka la wanawake Tanzania. Ikiwa utafanikiwa, klabu nyingine zinaweza kuanza kufuata njia hiyo na kuunda mfumo imara wa uzalishaji wa vipaji nchini. Hii inaweza kuongeza thamani ya soka la wanawake, kuvutia wawekezaji na hata kuongeza mapato kutokana na mauzo ya wachezaji.
Tausi FC imekuja na falsafa mpya WPL, falsafa inayotazama zaidi kesho kuliko leo. Ingawa inaweza isiwafurahishe baadhi ya mashabiki lakini ina msingi wa kujenga mfumo endelevu wa maendeleo ya soka.