Tanzanite Queens bado kidogo fainali za Kombe la Dunia U20
Muktasari:
- Tanzanite ni moja kati ya timu mbili kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zilizopenya hatua hiyo ya mwisho, ikiwa sambamba na majirani zao wa Uganda, zote zikisaka nafasi nne za uwakilishi wa Afrika katika fainali hizo zitakazofanyika Septemba mwaka huu huko Poland.
USHINDI wa bao 1-0 iliyopata timu ya taifa ya Tanzania ya Wanawake wenye umri chini ya miaka 20, Tanzanite Queens umeiwezesha kuanza kunusa ushiriki wa Fainali za Kombe la Dunia U20 2026, kwani sasa imesaliwa na mechi ya raundi ya mwisho dhidi ya Cameroon, ikitoboa hapo freshi!
Tanzanite ni moja kati ya timu mbili kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zilizopenya hatua hiyo ya mwisho, ikiwa sambamba na majirani zao wa Uganda, zote zikisaka nafasi nne za uwakilishi wa Afrika katika fainali hizo zitakazofanyika Septemba mwaka huu huko Poland.
Bao pekee la Winfrida Hubert ndani ya dakika 90 za kawaida liliiwezesha Tanzania kulipa kisasi kwa Wakenya ambao walishinda pia kwa bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza na kulazimisha mshindi wa jumla apatikane kwa matuta mwenyeji akisonga mbele kwa penalti 3-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex juzi Jumamosi, wenyeji Tanzania walishuka uwanjani na presha ya kusaka bao la kusawazisha kabla ya kuwaza mengine ya kuwabeba, lakini Kenya ilikuwa macho, licha ya kuruhusu bao hilo la Winfrida na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Lakini huko Ndola, Zambia kwenye Uwanja wa Mwanawasa, timu ya Uganda, Queen Cranes iliwashtua wenyeji kwa ushindi wa bao 1-0, huku Mary Kantono akifunga bao mapema katika dakika ya 7 na kuifanya Uganda ifuzu kwa jumla ya mabao 2-1, kwani mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya 1-1.
“Tuna furaha sana kwamba timu imecheza kwa moyo wote na kushinda mechi ugenini. Sasa tunahitaji kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo ya mwisho ya mchujo,” alisema kocha mkuu wa Uganda, Sheryl Botes.
Uganda sasa itamenyana na Ghana, huku Tanzania ikitarajiwa kukabiliana na Cameroon katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake U-20 la mwaka 2026.
Bara la Afrika litawakilishwa na timu nne bora zitakazojiunga na timu nyingine 20 kutoka mabara mbalimbali katika Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 la FIFA 2026, litakalofanyika Poland baadaye mwaka huu. Michuano hiyo itafanyika kati ya Septemba 5-27 mwaka huu.
SAFARI YA TANZANITE
Tanzanite Queens, ilianzia raundi ya pili ya michuano hiyo kwa kuvaana na Angola na kupata ushindi wa jumla ya mabao 7-0 baada ya awali kushinda 4-0 kisha kumalizia kwa 3-0 na kupangwa kukutana na Kenya.
Katika mechi ya kwanza ugenini ililala bao 1-0 kisha juzi kupindua meza ikiwa nyumbani na kusonga kwa penalti 3-1 na sasa inakabiliana na mfupa mgumu wa Cameroon iliyoing'oa Botswana kwa jumla ya mabao 5-1, ili kukata tiketi ya kwenda Poland.
Mechi dhidi ya Cameroon zinatarajiwa kupigwa kati ya Mei 1-8, Tanzanite ikianza ugenini na kumalizia nyumbani, huku ratiba nyingine za mechi hizo za raundi ya nne na ya mwisho inaonyesha Ghana itavaana na Uganda, Ivory Coast dhidi ya Benin na Nigeria kumalizana na Malawi.
Washindi wa mechi hizo nne ndizo zitakazofuzu fainali hizo, huku Tanzania ikisaka ushiriki wa mara ya kwanza kwa timu hiyo ya U20.
Tanzania ilishiriki fainali za Kombe la Dunia za U17 za mwaka 2022 zilizofanyika miaka michache iliyopita kule India na kutolewa hatua ya robo fainali na Colombia ilipofungwa kwa mabao 3-0 na sasa ni zamu ya Tanzanite kuisaka tiketi ya michuano hiyo mikubwa duniani.
Safari ya Tanzanite Queens ilipoanza ilikuwa ni ya kujenga misingi ya soka la wanawake kwa ngazi ya vijana Tanzania. Katika miaka ya hivi karibuni, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, limewekeza kikamilifu katika programu za vijana, ikijumuisha kambi za mazoezi, ligi za vijana na klabu zinazokuza vipaji vya soka la wanawake. Mkakati huu ulilenga kuwawezesha wachezaji kuingia katika daraja la ushindani la kimataifa.
Kwa miaka kadhaa kabla ya ushindi dhidi ya Kenya, Tanzanite Queens U20 ilizidi kubadilika kutoka timu yenye nguvu ndogo, bila uzoefu wa kimataifa, hadi kuwa kikosi kilicho na nidhamu, mbinu za kisasa na mfumo imara wa ushindani. Mchezo wao wa kwanza wa kimataifa ukawa kama kioo cha kuona nguvu na upungufu iliokuwa nao, nafasi ya kujifunza, kurekebisha makosa na kujenga nafasi ya kushindana kwa mafanikio mbele.
UKUAJI WA KIKOSI
Mfumo wa uchezaji na mafanikio ya Tanzanite Queens sasa hauwezi kutajwa bila kuashiria mchango mkubwa wa kocha mkuu, Bakar Shime 'Mchawi Mweusi'.
Shime anasifika kwa ufanisi wa kuzisimamia timu za soka za wanawake bila kujali mazingira ya changamoto, akisimamia mazoezi ya kimwili na kiufundi kwa undani mkubwa, huku akisisitiza si tu uchezaji wa haraka wala mbinu za ushambuliaji, bali mafanikio yanachangiwa pia na nidhamu ya kimaadili, umakini kwenye mazoezi ya kujipanga kimkakati na ustadi wa kushindana kimfumo dhidi ya timu za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Shime huwa anaamini kuwa mafanikio ya timu hutokana na uelewa wa wachezaji kuhusu nafasi zao, jukumu la kila mmoja na umuhimu wa msimamo thabiti wa kazi katika kila mechi.
NDOTO KUBWA
Kufuzu hatua inayofuata ya Kombe la Dunia U20 ni mafanikio makubwa kwa Tanzania, lakini kwa wachezaji na kocha Shime, hii ni hatua tu ya mwanzo. Safari ya kwenda fainali za dunia mara kwa mara inahitaji maandalizi zaidi makini, ikijumuisha mechi za kirafiki za kimataifa, mazoezi ya kimkakati dhidi ya timu zenye uzoefu wa dunia, na kuendelea kuboresha ustadi wa kila mchezaji.
Kocha Shime amesisitiza, kazi haiishi kwenye ushindi huo pekee, bali inalenga kuhakikisha timu inajenga mfumo wa ushindani wa kudumu. Hii ni pamoja na kuwatambua wachezaji vijana wenye vipaji vya juu na kuwapa mwanga wa mazoezi endelevu, pamoja na kueneza ari ya ushindani wa hali ya juu ndani ya ligi ya wanawake nchini Tanzania.
Kwa sasa, malengo makubwa ni kuona timu hiyo ikisonga mbele kwenda kuing'oa Cameroon na kuandika historia nyingine ya Tanzania kushiriki fainali za Kombe la Dunia baada ya zile za mwaka 2022 kule India.
Dhamira ni kuendelea kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Dunia U20, kushindana na timu zinazochukuliwa kuwa bora duniani, na hatimaye kuwa kati ya timu zinazofuzu fainali za Kombe la Dunia kwa ngazi kubwa zaidi. Hii sio ndoto ndogo kwa taifa letu, bali ni ahadi inayotekelezwa polepole kwa nguvu, ujuzi na uzalendo. Ngoja tuone itakuwaje!