Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania Prisons tatizo lipo hapa!

Tanzania Prisons tatizo lipo hapa!

MBEYA. STORI kubwa vijiweni kwa sasa kwa wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya ni kuhusu matokeo mabaya iliyonayo Tanzania Prisons kwenye Ligi Kuu, huku kila mmoja akiwa na mawazo yake juu ya hatma ya Wajelajela hao.

Kauli zinapishana baadhi wakiamini timu hiyo kongwe nchini huenda ikaaga Ligi Kuu msimu huu, huku wengine wakiipa nafasi ya kupindua meza kijeshi na kunusurika.

Mbali na mawazo hayo, bado swali kuu linabaki tatizo lililoikumba timu hiyo ambayo ina historia kubwa kwenye soka la hapa nchini ikiwamo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1999 na ushindani iliokuwa nao dhidi ya vigogo.

Maafande hao wa Magereza, msimu huu mambo yake hayajawa mazuri na kuamsha hisia kwa mashabiki wakionekana kuikatia tamaa kwa kiasi fulani.

Mwanaspoti imeiangalia kwa umakini ndani na nje ya uwanja na kukuletea sababu kadhaa zinazoiyumbisha timu hiyo, kinachoweza kuwamaliza au kuwanusuru msimu huu kwenye Ligi Kuu.


Majeruhi

Miongoni mwa mambo yanayoipa wakati mgumu timu hii ni pamoja na kuwakosa baadhi ya nyota wake wenye uwezo binafsi ambao wanasumbuliwa na majeraha.

Pamoja na kwamba wameanza kurejea mmoja mmoja, lakini timu hii ilikuwa na wakati mgumu haswa sehemu ya mabeki ambao kwa muda mrefu walikuwa msaada mkubwa sana.

Wachezaji kama Jumanne Elfadhil, Nurdin Chona, Salum Kimenya, Benjamin Asukile ni kati ya watu wenye msaada mkubwa kwa timu hiyo kutokana na uwezo na uzoefu walionao kikosini.

Kukosekana kwao katika baadhi ya mechi imeonekana kuacha pengo kubwa ambalo limaigharimu timu hiyo hadi kufikia hatua waliyopo kwa sasa kuanza kuhaha namna ya kukwepa kushuka daraja.

Tofauti na misimu ya nyuma kwa vijana hao kumaliza nafasi saba za juu, hivi sasa ndio wanaburuza mkia kwa pointi 13 baada ya mechi 18, hali inayotia wasiwasi.

Ilishuhudiwa maafande hao wakianzia msimu mkoani Rukwa walipokuwa wameweka kambi kabla ya kukimbia hivi karibuni na kurudi Sokoine ambako nako hakijaeleweka bado.


Usajili

Ni wazi timu hii haikufanya usajili mzuri licha ya kuwatema nyota wengi (16) wakati wa dirisha kubwa, lakini hata dirisha dogo haikufanya mabadiliko makubwa na yenye tija kulingana na mahitaji yao.

Katika ongezeko la wachezaji wa dirisha dogo bado hawajaonesha mchango wao wakiwa ni kipa Hussein Abel, Mudathir Said na Aboubakari Malika ambao hawajaweza kuwatoa kwenye nafasi wapinzani wao waliowakuta kikosini.

Pia kuwaruhusu waondoke nyota wao kama Jeremia Kisubi, Aron Kalambo, Gasper Mwaipasi, Shaban William, Kassim Mdoe na Seleman Mangoma nayo imekuwa pigo kwa kikosi hicho kwani nafasi zao hazipata mbadala rasmi.


Mabadiliko uongozi

Tangu kuanza kwa msimu huu, timu hii ya Jeshi la Magereza limekuwa na mabadiliko ya kiutendaji katika nafasi mbalimbali, jambo ambalo kwa kiasi fulani inapunguza ufanisi.

Wakati msimu unaanza, mabosi walifanya mabadiliko walipomtoa aliyekuwa Katibu Mkuu, Ajabu Kifukwe na nafasi yake kujazwa na Ally Mrisho, huku Romlo Kironge akisimama kama meneja wa timu kwa kipindi kifupi.

Katika nafasi ya meneja, msimu uliopita walikuwa ni Simon Meta, Kilian Ngala na Prosper Mzelu ambao kila mmoja alifanya kwa vipindi tofauti kabla ya kubadilishiwa majukumu, huku wakiitumikia nafasi hiyo kwa mafanikio.

Kwa sasa Wajelajela hao wapo chini ya uongozi wa Anthony How ambaye ni Katibu Mkuu na Osward Moris akivaa nafasi ya Meneja ambapo hali si shwari kwa ujumla kutokana na matokeo yalivyo.

Hata hivyo, licha ya hali kuwa mbaya, viongozi hao ni kama wanabebeshwa mzigo wa lawama kutokana na kuikuta timu ikiwa imeshakamilika kila idara hususani kwenye usajili.

Uongozi wa How na Moris haujashiriki kwa lolote katika maandalizi ya kuisuka timu msimu huu, japokuwa hawana budi kukubaliana na kuweka mikakati mipya ya kuivusha timu hiyo.


Makocha nao

Hadi sasa timu hiyo kongwe imeshasimamiwa na makocha wawili, ikianza na Salum Mayanga aliyeikimbia katikati ya msimu na kutimkia Mtibwa Sugar.

Mayanga aliyekuwa nao tangu msimu uliopita, ndiye alikuwa na kikosi tangu mwanzo ikiwamo kupendekeza majina ya nani aitumikie timu hiyo akishirikiana na uongozi uliokuwapo awali.

Hata hivyo, Mayanga hakudumu zaidi alipopata ofa kwa timu yake ya zamani na kuingia mitini na kuwapa jukumu mabosi wa Prisons kuingia sokoni kumsaka Patrick Odhiambo aliyepo sasa aliyekuwa akisaidiwa na Shaaban Kazumba.

Kazumba kwa sasa ameondolewa kwenye timu na nafasi yake kushikwa na Shaaban Mtupa, nyota wa zamani wa timu hiyo aliyekuwa akiinoa timu ya Vijana U20.

Odhiambo hakuhusika kwenye usajili wowote jambo ambalo hata matokeo ni ngumu kumhukumu moja kwa moja kwani katika michezo saba aliyosimamia ameshinda mechi moja ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), sare mbili na kupoteza nne.


Vigogo na matumaini

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Anthony How anasema licha ya matokeo hayo lakini bado wana matumaini na chama hilo kutoshuka daraja akibainisha kuwa mkakati wao ni kuanza na mechi tatu za nyumbani.

Anasema anafahamu ugumu ulivyo kwa sasa, akieleza kuwa kila timu inapambana kwa nafasi yake kuhakikisha wanapata ushindi, akifafanua kuwa pointi tisa zitawaweka pazuri kwenye msimamo.

“Tuna mechi tatu mfululizo hapa nyumbani tukianza na Dodoma Jiji, Coatal Union kisha Polisi Tanzania, tunaweka nguvu zote kuhakikisha hatuachi hata alama moja ambapo itatusaidia kujianasua mkiani,” anasema How.

Anasema kwa sasa wanaendelea kukaa na wachezaji kufanya tathimini lakini pia kuwatuliza na kuwaandaa kisaikolojia kuhakikisha michezo iliyobaki wanapambana kupata matokeo mazuri.


Kocha atuliza

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Odhiambo anasema kipindi wanachopitia ni kigumu na hajafikiria kung’atuka akisema kazi yake ni kufundisha na hawezi kukata tamaa kwani bado ana muda na mechi za kuamua matokeo.

Anasema wanapambana kuhakikisha michezo iliyobaki wanajikongoja kusaka ushindi ili kujinasua mkiani lakini pia kukwepa rungu la kushuka daraja.

Anawaomba wadau na mashabiki wa soka jijini Mbeya kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, akiahidi kuwa kurejea kwao kuutumia Uwanja wa Sokoine kuna maana kubwa kuwapa burudani.

“Ndio mpira ulivyo matokeo ya aina hii hutokea popote lakini bado hatujakata tamaa na sijafikia hatua ya kusema niondoke, naamini tutapambana na faraja itarejea kwa mashabiki,” anasema kocha huyo raia wa Kenya.