Straika anayekiwasha na mtoto uwanjani

Muktasari:

  • Mashindano hayo yalishirikisha timu saba kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro. Lakini kivutio kikubwa katika mashindano hayo alikuwa ni Amchezaji wa Kilosa Queens, Fatma Abdalah Gamba (18) ambaye alikuwa anakuja uwanjani na mtoto wake wa kumzaa (Farhia(miezi 13).

Morogoro: Kuna vitu vinaendelea viwanjani haswa hapa Morogoro vinavutia na kusisimua sana. Mojawapo ni hili lilitokea kwenye Ligi ya soka ya Wanawake Mkoa wa hapa iliyomalizika hivikaribuni na timu ya G.Seven kutawazwa kuwa mabingwa.

Mashindano hayo yalishirikisha timu saba kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro. Lakini kivutio kikubwa katika mashindano hayo alikuwa ni mchezaji wa Kilosa Queens, Fatma Abdalah Gamba (18) ambaye alikuwa anakuja uwanjani na mtoto wake wa kumzaa (Farhia(miezi 13).

Mchezaji huyo ambaye ni kiraka uwanjani, katika mechi zote amekuwa akiingia na mtoto wake na kumuacha jukwaani chini ya uangalizi maalum wa msaidizi wake, lakini ameenda mbali na kusimulia kwamba hata mazoezini miongoni mwa makocha ndiye Yaya(mlezi) wa mwanae.

 Ameelezea safari yake katika soka pamoja na simulizi nzito ya namna alivyofanya mazoezi bila kocha wake kugundua mpaka ujauzito wake mpaka ulipofikisha miezi sita.

Fatma ana miaka miwili tangu aanze kujihusisha na mchezo wa soka, ambapo safari yake ilianza mwaka 2022 wakati akiwa kidato cha nne alipoanza tu kujihusisha na soka badae akajikuta tayari ana ujauzito ambao alikubaliana nao na akajiwekea mazingira ya kuwa salama kiafya.

“Nilipoanza mazoezi ya mchezo wa soka ilinichukua miaka miwili kupata ujauzito na hata nilipogundua nina ujauzito sikumwambia yeyote bali niliendelea na mazoezi mpaka ujauzito ulipofika miezi sita ndio nikaacha,”anasema na kuongeza kwamba mzazi mwenzie siyo mwanasoka lakini hawaishi pamoja kwani bado yupo kwao.


CHANGAMOTO MAZOEZINI

“Wakati nikiwa mjamzito, kama nilivyosema niliendelea tu na mazoezi wakati huo ujauzito una miezi miwili, hali ikawa tofauti kwangu maana nilikua nikifanya mazoezi nachoka sana,sikuwa nataka kocha anitoe kwenye programu zake nilikua naamka naenda, lakini kiukweli hali ilikua mbaya lakini nilijitahidi mpaka ilipofika miezi sita nikaacha, nilishindwa kutokana na hali halisi.”€

Hakuamini kama angeweza kujifungua salama mtoto (Farhia) kutokana na mazoezi magumu ambayo alikua anayafanya kama wachezaji wengine huku Kocha wake akiwa hajui kama ni mjamzito

“Sikujua kama ningejifungua(anainuka na kuanza kulia)  maana nilifanya mazoezi sana na mwili ukachoka, lakini  namshukuru Mungu kwa kujifungua salama maana sikutarajia kama ningejifungua, maana nilifanya mazoezi ya nguvu, nikahisi kwamba mtoto angeharibika tumboni lakini nilijifungua.”

Fatma anasema baada ya kujifungua ilipotimia miezi mitatu akaanza mazoezi na kuanza kucheza mechi, kwa akili zake  alikua akiogopa kwamba Wazazi wake wangemkataza kucheza lakini hali ikawa tofauti.

“Mtoto alipofikisha miezi mitatu nikaanza kwenda mazoezi, maana nilikua siagi nyumbani, nilichukua baadhi ya nguo zangu nikapeleka kwa marafiki zangu nikawa naondoka kama naenda kutembea tu lakini baadae wakagundua Mama na Baba yangu wakaniambia nisiondoke kwa kutoroka badala yake niage na niwe makini na mtoto maana alikua mdogo sana hivyo nashukuru kwa sapoti yao.”


ANATAKA SIMBA,YANGA

“Matarajio yangu katika soka ni kucheza mpira katika timu kubwa hapa nchini, nataka huko mbeleni nicheze timu za Simba na Yanga ili nionekane maana hesabu zangu zote ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ndio maana hata mtoto wangu bado mdogo lakini napambana kuhakikisha natimiza ndoto zangu ili mtoto asome vizuri na kupata mahitaji yake,” anaongeza na kusema


MTOTO AKILIA TU...

“Timu yetu ratiba yake ya kufanya mazoezi kutokana na hali ya hewa ya Kilosa tunaanza saa nne asubuhi, lakini baada ya kujifungua nimekuwa mchelewaji sana kutokana na mtoto wangu hata nikienda mazoezi naenda nae.

“Mwanzo ilikua ngumu lakini sasa wachezaji wenzangu, Makocha wameshaelewa na nina ruhusa maalum kutoka kwa kocha nahata nikifika mazoezini kocha ndiye ananishikia mtoto na inabidi awe mbali maana kama ninaendelea na mazoezi, akilia tu,akili inahama kwahivyo mara nyingi huwa naenda na mdogo wangu huko kunisaidia”€


KIWANGO VIPI

“Kabla sijapata mtoto nilikua nacheza vizuri na uwezo wangu ulikua mkubwa sana uwanjani, lakini baada ya kupata mtoto naona kuna vitu kidogo vimepungua lakini kocha ameniangalia na amenishauri nizidishe mazoezi nitarudi kama mwanzo kiuchezaji na hilo ndio limenisaidia mpaka sasa nategemewa kwenye timu yetu”€

Kocha mkuu wa Kilosa Queens, Christom Kalima anasema wakati mchezaji wake anafanya mazoezi  akiwa na ujauzito alikua hafahamu chochote hadi ujauzito ulipofika miezi sita

“Mimi kama kocha wake alipokua na Mimba aliendelea na mazoezi kama kawaida, sikujua lolote na yeye alinificha, lakini baadae nilianza kuhisi maana hata mazoezi alipunguza lakini baadae nikatambua kama ni mjamzito basi nikamtoa kwenye program zangu ndipo akaenda kusubiri kujifungua.”

KOCHA NI YAYA MAZOEZINI

Kocha Kalima anasema wakati mwingine anapokuja mazoezini analazimika kumsaidia kubeba mtoto ili Fatma afanye mazoezi na wenzake kikamilifu.

“Mimi ni kama Baba mlezi wa Fatma hivyo Farhia Mtoto wa Fatma ni mjukuu wangu hivyo wakati mwingine kama hana msaidizi nalazimika kumsaidia kushika mtoto wakati wa mazoezi mpaka tunapomaliza lengo ni kumsimamia aweze kutimiza ndoto zake”


ELIMU YA SOKA

Kocha Kalima anasema; “Familia ya Fatma kiukweli hawana uwezo wa kumsomesha zaidi Mama wa Farhia (Fatma) ili aweze kutimiza ndoto, kutokana na hali hiyo mimi nimeamua kumsisitiza acheze soka apate kuajiriwa na timu kubwa  amtunze Mtoto wake.