Stars imevuna ilichopanda, ijipange kwa Afcon 2019

Muktasari:

Sare ya bao 1-1 iliyopata Stars nyumbani wiki iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza katika mechi ya kwanza ndiyo iliyoinufaisha Rwanda na kuifanya isonge mbele dhidi ya Tanzania.

TAIFA Stars chini ya Kocha Mkuu Salum Mayanga imeng’oka katika michuano ya kuwania kushiriki fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan-2018).

Stars ilikuwa mjini Kigali, Rwanda kuvaana na wenyeji wao Amavubi na pambano hilo la marudiano lililochezwa Uwanja wa Nyamirambo, liliisha kwa suluhu, hivyo kutolewa kwa faida ya bao la ugenini lililowabeba wapinzani wao.

Sare ya bao 1-1 iliyopata Stars nyumbani wiki iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza katika mechi ya kwanza ndiyo iliyoinufaisha Rwanda na kuifanya isonge mbele dhidi ya Tanzania.

Kutolewa kwa Stars katika michuano hiyo kunaifanya kwa mara nyingine izikosea fainali hizo zilizopangwa kufanyika mwakani nchi jirani ya Kenya na kunaifanya ibakiwe na michuano ya Kombe la Afrika (Afcon) itakayofanyika Cameroon 2019.

Ilichokipata Stars ni matunda ya kile ilichokipanda nyumbani katika mechi ya mkondo wa kwanza na hakuna sababu ya kuanza kutafuta mchawi, badala yake tusahau ya Chan na kujipanga kwenye michuano iliyopo mbele yetu.

Kung’olewa kwa Stars katika michuano hiyo kumewasikitisha wengi kwa sababu Rwanda haikuwa timu kubwa ya kuikwamisha Tanzania, lakini imeshatokea na sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu kwenye mbio za michuano ya Afcon 2019.

Tanzania imesaliwa na michuano hiyo tu ikiwa Kundi L pamoja na timu za Cape Verde, Uganda na Lesotho ambao tulishacheza nao na kutoshana nao nguvu kwa kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Kabla ya hapo Tanzania ilishapoteza dira katika kuwania fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Russia, hivyo kutolewa tena Chan ni msiba kwa soka la Tanzania katika ushiriki wa michuano ya kimataifa.

Turufu pekee ya kututoa kimasomaso ni Afcon na Machi mwakani tutaifuata Uganda The Cranes nyumbani kwao kabla ya kurudiana nao mwezi huohuo na ni lazima Stars ishinde ili kuweka hai mustakabali wake.

Mpaka kufukia Machi ni muda mrefu ambao kama tutaamua kujipanga upya basi kuna uwezekano wa kurekebisha dosari zilizotugharimu mbele ya Lesotho na kwa Amavubi, kiasi cha kuondoshwa mapema katika mbio za Chan.

Mwanaspoti linaamini Stars bado ina nafasi ya kurekebisha makosa na kuja kufanya vizuri kwenye mechi ya kundi lake, lakini ni kama wadau wa soka wakiwamo viongozi wajao wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wataamua kuelekeza nguvu kubwa katika michuano hiyo ili timu yetu iende Cameroon.

Kama tutaendelea na zile siasa zetu zilizozoeleka na kauli za kujitia moyo bila utekelezaji wa vitendo kwa timu hiyo, ni wazi tutarajie kuwa na mambo magumu mwakani kwani Uganda, Cape Verde na hata Lesotho hawatatuchekea asilani.

Stars ya Mayanga inahitajika kuongezewa nguvu katika idara ya ushambuliaji na eneo la beki wa kati, maeneo hayo yana udhaifu ambao tunaamini kwa muda uliopo kukaribia kwa mechi zijazo za kundi lao unatosha kurekebisha.

Bahati nzuri ni kwamba kabla ya kuvaana na Uganda benchi la ufundi la Stars litakuwa limepata wasaa wa kuangalia nyota wanaofaa kuwa ingizo jipya kwa timu yao kwa sababu Ligi Kuu Bara itakuwa imeshaanza kitambo.

Tunafahamu wazi kikosi kilichocheza Chan hakilingani na kile cha Afcon, lakini vikosi vyote tatizo la idara hizo mbili limeonekana, ndiyo maana tunasisitiza kama kweli tuna nia ya kwenda Cameroon, Mayanga na wenzake wafanye mambo mapema ili kuirahisishia kazi Stars. Bao tuna nafasi ya kusonga mbele.

Kadhalika kama itaonekana kuna ulazima, Mayanga aongezewe nguvu katika benchi lake ikiwezakana hata Mshauri wa Ufundi wa timu ya vijana U17, Kim Paulsen akapelekwa huko ili kuweka mambo sawa kabla ya kuifuata Uganda.

Stars haina namna nyingine ya kutuliza mioyo ya mashabiki wa soka nchini ila kufanya vyema katika mechi zake tano za kundi lake ili kukata tiketi ya Afcon na hasa baada ya mabadiliko yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa timu shiriki za fainali hizo za Cameroon.

Kuongezwa kwa idadi ya timu shiriki za michuano hiyo ni nafasi isiyopaswa kuchezewa na Stars kwa sababu, siku zote bahati huwa haiji mara mbili.

Tujisikie huzuni na aibu kwa kushindwa kushiriki fainali za Afrika tangu tulivyofanya hivyo mara ya kwanza na mwisho miaka 37 iliyopita tulipokwenda Nigeria mwaka 1980.

Miaka yote tumekuwa tu wasindikizaji bila ya kujiuliza tutakuwa hivyo hadi lini? Ni wazi kila kitu kinawezekana, Stars inaweza kucheza mashindano yoyote kama tu ikiandaliwa vyema.