Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI DOKTA: Mashabiki wazingatie haya Dabi ya Kariakoo

Muktasari:

  • Hii ni mechi kali ya watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara ikiwa ni marudiano baada ya awali kupigwa Oktoba 19, mwaka jana na Yanga kushinda 1-0.

NAAM kumekucha! Zimebaki siku mbili tu kabla ya Dabi ya Kariakoo kupigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hii ni mechi kali ya watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara ikiwa ni marudiano baada ya awali kupigwa Oktoba 19, mwaka jana na Yanga kushinda 1-0.

Mechi hiyo ambayo ni maarufu Afrika yenye kuvutia maelfu ya mashabiki itachezwa kuanzia saa 1:15 usiku.

Mara nyingi ni mechoi inayobeba hisia za wapenzi wa soka ambazo hazipimiki kiasi kwamba wengine hugeuziana kibao kama maadui na si watani wa jadi.

Kutakuwa na mashabiki na wachezaji walio katika mfungo wa Ramadhan na habari nzuri ni kuwa mechi  itachezwa saa moja usiku muda ambao wengi watakuwa wameshafuturu.

Katika mechi hiyo jicho la kitabibu litatoa ufahamu kuhusu mambo muhimu ya kiafya kuyazingatia unapokwenda kuitazama.


UKIHISI KUZIMIA FANYA HIVI

Kutokana na kubeba upinzani wa jadi ambao ndani yake una hisia za maelfu ya mashabiki wa soka kindakindaki mechi hiyo ni moja ya vitu vinavyoleta mpasuko wa hisia kwa mashabiki na huwa  na matukio ya kushtukiza ikiwamo kufungwa pasipo kutarajia. Hapa mtu anaweza akapatwa na mstuko na kupoteza fahamu. Kumbuka katika msongamano wowote kuna mnyang’anyano wa hewa safi na huku pia kukiwa na hewa chafu inayokuweka katika hatari ya kukosa hewa hatimaye kupoteza fahamu.

Kuzimia katika mchezo wenye msongamano mkubwa huwa ni kawaida katika mechi kubwa yenye wingi wa watu. Ni hali ya muda mfupi isiyozidi dakika moja ambayo inasababishwa na damu pungufu katika ubongo au kupata damu yenye hewa ndogo ya oksijeni. Inapodumu kwa muda mrefu ni ishara kuwa kuna tatizo zaidi, hivyo kuhitaji huduma za dharura.

Dalili za awali ni kuanza kuona giza, pumzi kukatika, kichwa kuuma, kichefuchefu na kuishiwa nguvu.

Ukipata dalili hizo lala au kaa chini ili kupunguza uwezekano wa kuzimia na kuanguka. Usiinuke haraka. Weka kichwa chako katikati ya magoti yako, kaa kitako na tulia kisha omba msaada kwa ishara.


MFANYIE HIVI ALIYEZIMIA

Kwa kuwa uwanjani upo msaada wa huduma ya kwanza ni muhimu walio jirani na mtu aliyekumbwa na hilo kuomba msaada haraka ili watu wa huduma ya kwanza watoe msaada. Wakati msaada unasubiriwa unaweza kumlaza chali kama hana majeraha na anapumua. Inua miguu ya mhusika juu kuzidi kifua kama inchi 12 (sentimita 30). Fungua mikanda, kola au nguo zenye kubana.

Ili kupunguza uwezekano wa kuzirai tena, usimwinue mtu huyo haraka. Ikiwa mtu hatapata fahamu ndani ya dakika moja endelea kuomba msaada wa huduma ya kwanza.

Angalia tena kama anapumua, angalia mapigo ya moyo na tazama kama kuna mkwamo njia ya hewa. Ikiwa mtu hapumui anza huduma ya utomasaji wa moyo kifupi CPR kama tu una ufahamu wa kutoa huduma hiyo. Endelea CPR hadi usaidizi ufike au mtu aanze kupumua.

Waliopo jirani waendelee kuita huduma ya kwanza ya afya ya kwanza ambayo katika mchezo kama huo ipo.

Ikiwa mtu alijeruhiwa wakati anaanguka na kuzimia, hudumia majeraha kama ya mchaniko na michubuko kwa kudhibiti kutokwa na damu kwa kuweka shinikizo la moja kwa moja katika jeraha.

Vilevile walio jirani ni vizuri kumpa nafasi aweze kupata hewa safi na muhimu kuepuka kumzunguka na kumtazama tu.


KUEPUKA KUZIMIA

Hakikisha unawahi mapema uwanjani ili kuepuka kusongamana na kusimama muda mrefu katika foleni.

Pata mapumziko ya kutosha na lala angalau saa nane katika usiku mmoja kabla ya mechi hiyo. Hakikisha umekula vizuri na umekunywa maji ya kutosha angala glasi 10 kwa siku au lita 1.5-2. Hali ya hewa ya Dar ni joto, hakikisha unakunywa maji ya kutosha siku tatu kabla ya mechi.

Ikumbukwe kutokuwa na maji mwilini ya kutosha ni moja ya sababu inayosababisha watu kudondoka na kupoteza fahamu.

Vilevile maji yanakusaidia umalize kuutazama mchezo ukiwa na maji mengi hata kama umeyapoteza kwa njia ya jasho.

Pamoja na kuwa wapo baadhi ya wanaofunga watakuwepo katika mchezo huo ni muhimu na wao kuzingatia kunywa maji mengi mara tu wanapofungua na kula mlo mwepesi wa kuwapa nguvu.

Kama ni mgonjwa wa magonjwa ya moyo na kisukari na umri umekwenda ni vizuri kuhakikisha unazingatia ushauri wa daktari ikibidi tazama mechi hiyo nyumbani.

Kama uwezo unaruhusu ukiwa ni mtu mzima ambaye umri umekwenda vizuri kukaa eneo la V.I.P kwani eneo hilo lina mazingira yenye nafasi yasiyo na msongamano wa watu, basi fanya hivyo.

Mechi hiyo itachezwa saa 1:15usiku hii ina maana itakuwa faida kwa mashabiki na wachezaji kwani wanaupukana na jua ambalo lingezidisha makali ya joto.


KUEPUKA AJALI

Mechi hiyo inawashika watu kila kona nchini, hivyo husafiri hapa na pale kwa kutumia vyombo vya moto. Fanya ukaguzi wa gari mnayotumia kwa wale wanaosafiri kutoka mikoani.

Hakikisha kuwa dereva anayeendesha chombo cha moto hatumii pombe au kilevi cha aina yoyote na asiwe mwenye uchovu wa mwili.

Katika mechi hizo ni kawaida mashabiki kuwa makundi na kukaa baa za jirani wakibugia pombe za kutosha. Unywaji huwa ni kabla na baada ya mchezo, ilhali wengine huwa na furaha iliyopita kiasi au huzuni kali, hivyo hujipoza au kujipongeza kwa kunywa pombe. 

Hakikisha kama unatumia bodaboda uvae kofia ngumu hii ni kwa dereva na abiria. Siku hiyo barabara nyingi zinakuwa na hekaheka nyingi ambazo hatari ya kutokea ajali ni kubwa.


MENGINE YA KUZINGATIA

Vaa mavazi ambayo yatakuwa rafiki na hali ya hewa ya joto ikiwamo nguo ambazo ni rahisi kuvutika na kunyonya jasho la mwili na miguuni ukivaa raba isiyo laini wala ngumu sana.

Usikae katika maeneo ambayo wanakaa mashabiki wakereketwa ambao wana hisia kali na timu zao kwani unaweza kuwakwaza wakalipuka. Kama wewe ni shabiki kindakindaki kaa eneo ambalo ndilo linalojulikana rasmi kwa ajili yenu. Hii itakupunguzia hatari ya kuingia katika migogoro.

Kufanya hivi kunakuepusha na mifarakano na mashabiki wengine na pia kukuepusha kuumia kihisia kwani ukifungwa na wewe watakukejeli hatimaye utaumia kihisia.

Siku hiyo inakuwa na mambo mengi ikiwamo uchafuzi wa kelele ambao unaweza kuwa kero au baadaye kukuletea shida ya kichwa kuuma, masikio kuuma na mwili kuwa na uchovu. Kama unakwenda na watoto ni vizuri kuwahi mapema na kuhakisha unawalinda na mambo yote hatarishi kwa afya zao ikiwamo msongamano.