Siri ya Katwila kunyoa kipara

KAMA ulikuwa hujui basi ngoja tukujuze. Pamoja na timu ya Mtibwa Sugar kuboronga kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara, hilo halisababishi maisha mengine kutoendelea.

Wengi wanamjua Kocha Zuberi Katwila mwenye leseni A ya CAF kuwa aliwahi kukipiga Mtibwa Sugar enzi zake na ni kocha wa kikosi hicho kwa awamu mbili alizoitumikia kwa takriban miaka minane.

Tangu kocha huyo astaafu kucheza soka 2013 alianza kunyoa kipara huku akivaa miwani yake na kutokelezea kama ilivyo kwa makocha wengine wanavyosimama kwenye msitari wa uwanja (touchline) siku ya mechi wakiwa wameulamba.

 Tumekutana na kinyozi wa kocha huyo ambaye hufunga saluni yake na kisha kuanza safari mpaka nyumbani kwa kocha huyo anayeishi Turiani kwa ajili ya kumnyoa kipara kwa wembe, amezungumza na Mwanaspoti na kufunguka mengi.

Jamaa amejitambulisha kwa jina la Elisha Martine, mzaliwa wa Shinyanga ambaye kwa sasa anaishi Turiani mkoani Morogoro.

Martine anasema kuwa mpaka sasa ana muda mrefu akimnyoa Katwila na anafurahia kumnyoa kwani ni nafasi adhimu ambayo kuipata sio rahisi.


ANAPENDA KUNYOA STAILI GANI?

Martine anasema tangu amfahamu Katwila mara nyingi amekuwa akinyoa kipara na asili ya nywele zake kwa sasa kuna sehemu zimeisha kabisa hivyo hata akinyoa kwa mtindo mwingine bado hatapendeza.

 “Hivyo niliamua kumshauri anyoe upara na yeye akakubali na ndio mtindo wake anaonyoa kila leo na watu wameshamzoea kuona ananyoa hivyo na akinyoa anapendeza,” anasema.

“Kwa sasa Katwila ameshakuwa rafiki yangu, mara nyingi ananisaidia pale ninapokuwa na shida ndogondogo hivyo hii kwa sasa ni kama familia. Lakini nikimnyoa huwa ananilipa mpaka elfu tano maana nikija hapa kwake ninafunga saluni yangu ninafanya kazi kisha narejea eneo langu la kazi.”

UNANYOA WACHEZAJI?

Martine pia huwanyoa wachezaji wa timu hiyo. “Naweza kusema mimi ndiye kinyozi wa kocha Katwila, wachezaji na hata viongozi maana wachezaji walio wengi ninawanyoa tena kwa kuja hapa kambini na hapa mimi peke yangu ndiye ninaingia kwa urahisi kuliko mtu yeyote hivyo ninawanyoa makocha, wachezaji na hata viongozi pia,” anasema.

“Nina saluni yangu iko Madizini hapahapa Turiani, mwanzo walikuwa wanakuja kunyoa kwangu nikiwanyoa wanaona utofauti ndio Kocha katwila akaniita nimnyoe nyumbani kwake. Tangu hapo hata wachezaji nikaanza kuwafuata na sasa nimezoea hivyo kupata hii kazi ilikuwa kama bahati na najivunia kuwa familia ya Mtibwa Sugar.

“Sipati tatizo maana kwa sasa ameshakuwa kama ndugu yangu, kabla sijaanza safari ya kufika hapa huwa ananipigia simu anauliza kama nina nafasi ndio nije, kama nimebanana huwa namweleza ukweli na nikipata muda nakuja namsafisha maana huwa namnyoa kipara kwa wembe pamoja na ndevu zake ambapo namnyoa kwa mashine ya kawaida.”



KUWAPENDEZESHA WACHEZAJI

Martine haishii kuwanyoa pia huwapendezesha nywele mastaa.

“Mara nyingi kabla ya mechi kwa kuwa zinaonyeshwa kwenye televisheni, mimi ndiye ninawanyoa wachezaji. Wapo wale wanaopaka rangi (piko) kwenye nywele hususan beki Geofrey Luseke anapenda kupaka piko kwa hiyo naifanya hii kama kazi yangu rasmi maana inanipa riziki kwa kuwa nikimaliza kumnyoa mchezaji au kocha huwa nalipwa papo hapo,” anasema.


MTIBWA KUFANYA VIBAYA

Juu ya timu ya Mtibwa kufanya vibaya katika Ligi Kuu, ikishika mkia kwa sasa, kinyozi huyo anaumia sawa na mastaa na kocha wa timu hiyo.

“Majanga mzee, tunaumia sana tena kama mimi ninayekuja kambini kwa wachezaji muda wote nikirudi mtaani naulizwa maswali kibao, wanajua pengine nayajua zaidi kumbe hata mimi sjui ila inatuumiza na binafsi huwa napata kazi kuijibia timu (kwa mashabiki),” anasema.

“Huwa tunaongea na Katwila mara nyingi ninasema naye wakati ambao naona kule mtaani kelele zimekuwa nyingi, kwa kuwa naye hapendi hali ya kukosa matokeo itokee huwa anajibu kwa ufupi tu kwamba tutaimarika na kushinda.”


ALIVYOENDA IHEFU

Kuna wakati Katwila alikwenda Ihefu kuifundisha, ambako alikaa kwa miaka mitatu na hapa Matine aliumia.

“Aisee Kocha Katwila alivyohamia Ihefu kiukweli nilipata wakati mgumu maana nilishazoea ananipa riziki kwani kipara chake siku nne nyingi lazima nimnyoe tena, hivyo nilikosa raha. Lakini hata makocha wengine waliokuja kama Mayanga nilikuwa namnyoa na wengine ila huyu nimemzoea sana,” anasema

Anasema kutokana na kazi yake ya kuwa kinyozi alipata bahati ya kumnyoa kiungo mkabaji wa Mtibwa enzi hizo, Mghana James Kotei ambaye aliichezea pia Simba, huku akidai kwamba hata rasta za Baraka Majogolo ndiye alikuwa anazitunza kuhakikisha zinakua kwenye ubora.


KWANINI KIPARA?

Akizungumzia unyoaji wake, Katwila anasema anapenda zaidi kiparana ana sababu ya kufanya hivyo.

“Hii ni staili yangu ninayonyoa kwa sasa maana miaka ya nyuma nilikuwa nina nywele zangu kichwa kizima lakini nilipoingia kwenye masuala ya mipira, tena kuwa kocha ndio nywele zangu zikaanza kupotea baadhi ya maeneo ya kichwa changu, ndiyo maana napenda kunyoa hivi,” anasema kocha huyo

Katwila anaeleza kwamba anapenda fundi wake wa kunyoa amfuate nyumbani kwake kwa kuwa kutembea huwa hapendi na akifuatwa ananyolewa kwa urahisi kuliko akienda kutembea mtaani kusaka saluni ili afanye usafi wa nywele.


 HAPENDI MITINDO

Kocha huyo anasema hata kama ingekuwaje, yeye sio muumini wa mitindo ya nywele.

“Kwa umri wangu wa sasa miaka 51, kunyoa mitindo kwa sasa sio fahari maana umri umeshatupita mitindo tumewaachia wachezaji maana mfano nikinyoa mtindo mchezaji wangu naye nitamwambia nini,” anatania na kucheka kocha huyo akisisitiza kwamba ananyoa kulingana na umri wake.

 “Sipendi kwenda Barbershop kunyoa kama wanavyofanya wengine badala yake huwa ninayoa kwa vinyozi wa kawaida tu maana kwa sasa sitaki mambo mengi.”


KUNYOA NA KIWEMBE

Pamoja na kupenda kunyoa kipara, Katwila ambaye enzi zake pia aliitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa mafanikio makubwa, anaeleza kwani hupendelea kunyolewa nywele kwa kutumia wembe.

“Zamani nilikuwa nanyoa na mashine ikawa inaniotesha upele mwingi, ikafika mahala nikabadilisha nikaanza kunyoa upara wangu kwa wembe sikupata madhara,” anasema na kuongeza:

“Tangu wakati huo natumia wembe kunyoa nywele, lakini ndevu huwa naendelea kunyoa kwa mashine ya kawaida.”

Huyo ndiye Katwila, nyota na kocha aliyeitumikia Mtibwa kwa muda mrefu zaidi katika nafasi zote mbili.