SIO ZENGWE: Wakati wa kupumzisha akili umefika, tujuane baadaye

WAKATI fulani nilimshangaa bosi wangu mmoja kukataa kutenga muda na mtu ambaye amekuwa naye kwa kipindi kirefu.

Siku hiyo bosi alikuwa anaingia ofisini na mtu mmoja aliyekuwa nje ya ofisi akamsalimu na kumwambia angependa amuone waongee kidogo, bila ya kujali muda gani. Lakini bosi wangu akawa muungwana sana akamwambia “wewe na mimi kwa sasa ni salamu tu hadi haya mambo yaishe”.

Sikuamini ilikuwa ni kali thabiti na hakumtengea muda huo wa kuambiwa suala dogo. Nilipofika ofisini, nilimuuliza ilikuwaje akakataa kutenga muda wa mazungumzo na mtu ambaye ni wa karibu sana, tena ndiye wakati mwingine hufanya siku yake kuwa bora kutokana na mazungumzo na ucheshi wake.

Bosi wangu akaniambia kama nilimsikiliza jioni ya siku iliyotangulia, ningemuelewa kirahisi. Jioni hiyo, mtu huyo alikuwa amemponda sana bosi wangu, akisema hafai na anatakiwa aondoke ili akili mpya iingie ofisini kwake. Usingetegemea yeye aliyekuwa anaomba muda wa maongezi na mtu aliyemponda kwa nguvu siku moja iliyokuwa imepita.

Bosi wangu aliniambia kuwa wakati wa uchaguzi ni wakati ambao watu hupumzisha akili zao na kuacha ujinga ufanye kazi.

Na ndivyo ilivyo, wakati huu ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaelekea kufanya uchaguzi wa viongozi wake, akili chache sana zitafanya kazi. Akili nyingi zitakuwa zikizungumza mambo usiyotarajia kutoka kwa watu uliozoea kusikia wakizungumza mambo mazuri kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Hao ni wale wanaonufaika na watu waliopo madarakani kwa sasa, wanaotarajia kunufaika iwapo watu fulani wataingia madarakani na wakati mwingine ni wale wanaotarajia kuingia madarakani.

Huu ni wakati ambao si ajabu kurushiwa tusi zito, si ajabu kupakaziwa jambo zito lisilo na miguu wala kichwa, si ajabu kubambikiwa mafanikio ambayo hukuyaanzisha, si ajabu kukumbushiwa rekodi ambayo haina uhusiano na wewe, si ajabu kwa vipindi vya televisheni na redio kugeuka majukwaa ya watu fulafulani, si ajabu magazeti kusifu, kutukana au kumpigia kampeni mgombea mmoja na mambo mengi.

Lakini usidhani kuwa hao watakaotoa maneno hayo au kuropoka, hawana akili nzuri, la hasha. Wameamua kupumsiasha akili kwa sababu wimbi la uchaguzi linapita na baada ya hapo akili zitarudi. Na hurudi pale mambo yanapoonekana kuanza kuharibika. Ambao ndio baadhi hujuta kwamba ilikuwaje wakapumzisha akili wakati muhimu wa kufanya uamuzi bora kwa ajili ya maendeleo ya michezo yetu. Wengi tuliwasikia huko nyuma wakisifu wagombea fulani kuwa ndio majembe na ndio wadau wakubwa wanaoweza kuokoa mpira, ambao hata hivyo haukuwa hatarini.

Hawa walitutafuta baadaye ili watuombe radhi, lakini shughuli za kutafuta riziki zilibana muda na hivyo haikuwa rahisi kusikia majuto yao.

Si vizuri kusubiri kipindi cha kujuta. Ni muhimu kufanya uamuzi sahihi sasa. Watalaamu wanasema kesho yako ni leo. Kile unachofanya leo ndio kinaamua kesho yako. Hakuna kesho inayojitegemea, kesho inayosubiri ifike ndipo ianze kujitengeneza. Bali ipo kesho inayotengenezwa leo. Ukiwa na Sh100,000 ambazo unatumia leo, na ukaamua kuhifadhi Sh20,000 kati ya hizo, unakuwa umeanzisha kesho yako vizuri.

Lakini ukizitumia zote, maana yake kesho utaanza moja na hiyo haitakuwa kesho tena. Ni muhimu sana kwa watu wa mpira kuacha hayo mazoea ya kupumzisha akili wakati wa kufanya maamuzi muhimu kuhusu mchezo huu. Watu wa mpira wanapofanya uamuzi sahihi leo, wanaijenga kesho bora. Wakipumzisha akili zao leo, wanajenga kesho mbovu itakayofanana na jana mbaya.

Wakati nazungumzia mabadiliko ya katiba, sikueleweka. Lakini yameijenga kesho ya leo iliyo mbaya Zaidi. Wachache walihoji malengo ya mabadiliko hayo, lakini wengi wakapumzisha akili. Leo hii kuna tatizo katika kutafuta udhamini kwa wagombea urais baada ya kanuni kutaka kila mgombea apate mikoa mitano au wanachama shiriki.

Maana yake, kukiwa na wagombea kumi, kila mmoja atatakiwa awe na mikoa mitano na hivyo jumla ni 50. Lakini idadi ya mikoa ya TFF na vyama shiriki ni 31 tu. Wengine watano watapata wapi wadhamini. KIhalisia haiwezekani. Lakini labda ndio utamaduni wa mpira wa miguu Tanzania kwamba uchaguzi unapofika, ni muhimu kupumzisha akili na kwenda na wimbi la ujinga. Tupumzishe akili na tujuane baadaye.