Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Ubora ni uwanjani, si katika makaratasi

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Na mjadala ukajikita zaidi katika orodha ya ubora wa klabu inayochakatwa na CAF ambayo huzingatia jinsi timu zinavyosonga mbele katika mashindano yake mawili, Ligi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho.

TANGU Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) litangaze kuanzisha Ligi ya Mpira wa Miguu Afrika (AFL) kumekuwa na mijadala mingi kuhusu vigezo vinavyotumika kupata timu shiriki.

Na mjadala ukajikita zaidi katika orodha ya ubora wa klabu inayochakatwa na CAF ambayo huzingatia jinsi timu zinavyosonga mbele katika mashindano yake mawili, Ligi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Timu ambazo huingia makundi na kusonga mbele hadi fainali, hukusanya pointi nyingi zaidi ya zile zinazofanya hivyo katika Kombe la Shirikisho. Na kikubwa zaidi, pointi hizo hujumlishwa katika kipindi cha miaka mitano ili kutengeneza orodha hiyo.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kwa mfumo huo, hata timu ambayo ilifanya vizuri sana katika kipindi cha miaka mitano, lakini ikashindwa kutwaa ubingwa wa nchi yake na hata kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, itaweza kupata nafasi ya kushiriki AFL kwa kigezo cha ubora wake wa miaka mitano iliyopita.

Viongozi wa klabu, kama Zamalek walihoji sababu za CAF kutumia mfumo huo, wakisema haushirikishi timu zilizo na ubora kwa wakati huo na hivyo kusababisha mashindano ya ubingwa ya nchi yasiwe na maana kwa CAF.

Hata hivyo, CAF, ambayo inaelekea kuwa inasukumwa na rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) katika mpango huo, imeendelea na utaratibu huo na msisimko wa ligi hiyo hauonekani kuwa mkubwa kama wa Ligi ya Mabingwa, huku mechi kadhaa za awamu ya kwanza iliyoshirikisha timu nane, zikihudhuriwa na mashabiki walioruhusiwa kuingia bure uwanjani.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Suala hilo la ubora limeendelea kuwa gumzo katika mijadala mbalimbali nchini, huku baadhi wakionekana kukubaliana na CAF na wengine kupinga. Lakini kwa mukhtadha wa soka la Tanzania, mijadala hiyo ni kati ya mashabiki wa Yanga na Simba na baadhi ya wachambuzi walioamua kujitoa akili.

Ni lazima taasisi kama CAF iwe na mfumo wake wa kupata timu bora, uwe ni mbovu au mzuri. Ni lazima pia taasisi kama Opta iwe na vigezo vyake vya kupata timu bora, na hali kadhalika taasisi nyingine kama IFFHS ambayo ndio inaaminika na mamlaka mbalimbali za soka duniani.

Kupinga vigezo vya Opta au IFFHS ni kupoteza muda kwa sababu ziko taasisi zinazotumia takwimu zao kuendesha mambo na hakuna anayelazimishwa kuzitumia na hata zikipingwa haziathiriki kiutendaji kwa kuwa ni uamuzi wao kutumia vigezo fulani tofauti na wengine.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kwa wale wanaojua umuhimu wa takwimu huweza kutumia takwimu za taasisi zote kwa nyakati tofauti kulingana na mahitaji ya mradi wao wenye malengo fulani. Kwa hiyo kukataa takwimu za taasisi moja kwa sababu vigezo vyake vinaiweka chini timu ambayo mtu anaishabikia, ni kupoteza muda na kujitekenya ili apate furaha ya bandia isiyodumu.

Ni muhimu kukubaliana na takwimu za taasisi tofauti kulingana na umuhimu wa vigezo tofauti vinavyotumiwa katika mukhtadha fulani.

Kitu cha msingi ambacho kingefaa kuzingatiwa ni ubora wa timu kwa wakati huo. Hata kama ikiwa juu kwenye orodha ya ubora, lakini uwanjani ikawa mbovu, basi furaha hiyo ya kuwa juu ni ya muda na itapotea kadiri timu hiyo itakavyobweteka na ubora huo na kushindwa kurekebisha hali.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kwa muda mrefu, Pyramids ya Misri ilikuwa haishiriki Ligi ya Mabingwa na haikuwa juu sana katika orodha ya ubora, lakini imekuwa ikiimarika kila mwaka na sasa imo kwenye orodha hiyo, ikiwa imefanikiwa kufika hatua ya makundi  kwa msimu wa pili mfululizo, ikiwa imeshika nafasi ya pili Kombe la Shirikisho mwaka 2019.

Ukiiangalia katika orodha hiyo ya ubora ya CAF, Pyramids iko chini ya Petro de Luanda, ambayo imeshindwa kuvuka hatua za awali za Ligi ya Mabingwa, RS Berkane, USM Alger na Zamalek ambazo zinashiriki Kombe la Shirikisho.

Kwa maana nyingine, timu ambayo kwa sasa iko katika ubora (good current performance) ndiyo ambayo kwa mujibu wa vigezo vya CAF, inashika nafasi ya 16 ukilinganisha na hizo timu tatu zilizo katika kumi bora.

Hata hali ya mashabiki wa Pyramids wanapokuwa uwanjani hii leo watakuwa na furaha zaidi kulinganisha na mashabiki wa Petro, RS Berkane, USM Alger na Zamalek kwa kuwa ubora wanaouona uwanjani unawapa ladha halisi ya ubora wa timu yao, sio huo wa kwenye makaratasi ambao hauonekani uwanjani.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kwa maana nyingine, ubora huo wa takwimu unazisaidia taasisi husika katika kupanga ratiba za mashindano yao au vitu vingine kama tuzo, lakini hauakisi ubora wa uwanjani kwa wakati huo.

Kwa hiyo ni vizuri kujua dhana hizo mbili na kwa jinsi gani zinatumika. Kwangu ukiniuliza vigezo vipi ni vizuri, mimi nitaangalia vile vinavyoakisi kiwango cha timu kwa wakati husika kwa sababu ndio ambao nauona kwa macho yangu na si kuufikiria.

Na burudani huletwa na kile unachokishuhudia ubora wake, si ule wa kusikiliza waliokusanya takwimu wamepata nini.

Ubora ni uwanjani, wa makaratasi kwa ajili ya ratiba. Hakuna shabiki ambaye atakwenda uwanjani kushuhudia ubora wa kwenye makaratasi na aridhike akiambiwa timu yake ni bora makaratasini hata kama itakuwa imechezea kichapo siku hiyo!