SIO ZENGWE: Edo amesema kweli kuhusu wachambuzi

SIO ZENGWE: Edo amesema kweli kuhusu wachambuzi

WIKI iliyopita Edo Kumwembe alitoa maoni katika akaunti yake binafsi ya Instagram kuhusu uchambuzi, akisema wachambuzi wa sasa inabidi wajikite katika dakika tisini za mchezo na hayo mambo mengine waachie wenye uzoefu nayo.

Alikuwa ameongeza kiungo katika mboga ambayo ilishaanza kuchemka. Hivi sasa, kila siku mitandaoni, wachambuzi wamekuwa wakishambuliwa zaidi kuliko kusifiwa.

Baadhi wakituhumiwa kuwa chawa au watu wanaotumiwa kushusha upande mmoja na baadhi wanaonekana wameshajenga misimamo kuhusu mambo yanayohusu genge fulani na hivyo hata itokee nini, watapinga tu au kukosoa kwa jinsi ya kuunufaisha genge jingine.

Wapo ambao wamegeuka kuwa wasambaza habari zinazovuja na baadaye haohao kuhusika kuzichambua na kuweka misimamo, ikiwa ni pamoja na kuapa eti ikiwa tofauti wako tayari wafanyiwe kitu, na wapo wenye maslahi na hizo habari kutokana na shughuli zao za kipato nje ya uchambuzi.

Hivi sasa kukuta kejeli dhidi ya uchambuzi au mchambuzi ni kawaida na kwa jinsi hali inavyokwenda suala hilo linaweza kupoteza thamani na maana ya uchambuzi.

Wachambuzi sasa wanajua kila kitu. Likiibuka suala la uamuzi, wao ndio wa kwanza kutuma video mitandaoni na baadaye kujadili kwenye vipindi, huku wakiweka misimamo yao kwamba “lilikuwa goli halali”, “ilikuwa offside”, “mpira ulishatoka”, “ulikuwa mchezo wa hatari na hivyo ni kadi nyekundu” na mambo mengine mengi. Ni kama wamegeuka V.A.R ya kuonyesha uhalisia wa tukio. Wanasahau kanuni kuu ya soka kwamba refa ndiye mwenye uamuzi wa mwisho. Na hii ni mbaya kwa sababu inajenga chuki dhidi ya waamuzi na inaweza kusababisha hatari kwa marefa.

Kama ni mikataba ya udhamini, wao ndio wajuzi wanaoeleza kila kitu bila ya hata kuweka sentensi ya kujikinga na kueleza kwamba mkataba huo ni mbovu, hauko wazi, kana kwamba hawajui kuwa si rahisi mkataba wa kibiashara kuwekwa hadharani.

Likizuka suala la uongozi, pia wako mstari wa mbele kukosoa kuweka misimamo yao, na yule atakayetofautiana nao humchukulia kuwa hajui lolote. Vivyo hivyo katika mambo mengine mengi.

Tumeona jinsi masuala kama ya Twisila Kisinda, Juma Mgunda, Stephane Aziz Ki, mkataba wa GSM na TFF yalivyoibua maneno kwa wachambuzi. Pia jinsi baadhi yao walivyopoteza muda kujadili kuwa Fiston Mayele ni mchezaji wa kawaida, kama ilivyo sasa kwa Aziz Ki ambaye ameanza kujadiliwa kuwa ni wa kawaida. Achilia mbali hayo, wako walioanza kuhoji nani ni bora kati ya Aziz Ki na Clatous Chama. Yote hayo yanageuka kero kwa wasikilizaji na wa mitandaoni.

Kiasilia neno wachambuzi kwa wenzetu walioendelea lilitokana na neno la Kihindi la pandit (likakogeshwa jimbo na Waingereza na kuwa pundit), likimaanisha walimu na viongozi ambao walikuwa wakiheshimika sana India. Huonyesha heshima kwa mtu mwenye busara na ambalo asili yake ni Sanskrit pandita, likimaanisha mtu aliyeelimika kama wale wanasheria wanaojiita learned brothers. Wazungumzaji Kiingereza wakaanza kulitumia kwa kurejea maana ya Kihindi na baadaye likatumika kumaanisha watu wenye ujuzi wa mambo ambao jamii inasikiliza maoni yao. Watu hao ni kama wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi, fedha na wenye safu magazetini.

Baadaye michezo imechukua dhana hiyo na hivyo kutumia watu waliocheza soka katika ngazi ya kulipwa kuwa ndio watu wenye ujuzi ambao maoni yao yanaweza kuaminiwa na umma au mashabiki wa michezo.

Ndio maana redio na televisheni zote duniani hutumia wanamichezo wastaafu kuchambua michezo yao kutokana na ufahamu wao wa mchezo walioupata kwa kucheza na kufundishwa na makocha tofauti. Hujua undani wa kile anachofanya mchezaji, mazingira ya uwanjani, maelekezo anayoweza kuwa amepewa na hali ya timu kwa ujumla.

Ni kweli kwamba katika wachambuzi kumi bora wa Uingereza, wanasoka wa zamani ni wachache, lakini hiyo haiwezi kutufanya tusizingatie mwelekeo wa uchambuzi duniani ambao sasa unajikita zaidi kwa wanamichezo wastaafu. Lakini huku kwetu tumechukua njia yetu ambayo si mbaya, bali inatakiwa iboreshwe kwa mijadala kama hii.

Wachambuzi kama kina Jamie Gallagher, Ray Hudson, Clive Tydesley, Michael Owen au Martin Tyler ni wazuri sana kuchambua mechi, lakini inapofikia masuala ya udhamini, huwezi kuwasikia tena. Hapo wataitwa wachumi, viongozi wa zamani na wataalamu wa sheria au biashara kuzungumzia uzoefu wao au ufahamu wa masuala ya udhamini.

Hii husaidia kuwapa wasikilizaji na watazamaji elimu zaidi kuhusu huo udhamini na hivyo kuelewa kinachoendelea.

Hivyo hivyo, katika masuala ya uongozi na mengine mengi kunatakiwa wenye uzoefu au ujuzi wa maeneo hayo. Pengine wasikilizaji na watazamaji televisheni wanaona karaha kusikia watu walewale wakichambua kila kitu, ndio maana hizi kejeli mitandaoni zinazidi, hasa katika nchi iliyogawanyika kishabiki kama Tanzania.

Uchambuzi ni suala muhimu sana katika maendeleo ya soka kwa kuwa linasaidia kuongeza thamani katika matangazo ya moja kwa moja na kusaidia watu kuelewa kwa mapana na marefu yale yanayotokea wakati wa mechi au katika masuala ya kiungozi, kifedha au mikataba. Husaidia mashabiki kuwaelewa wachezaji wao na hata mikakati na mipango ya makocha na hivyo kujenga subira na matumaini.

Lakini umuhimu huo utakuja pale tu uchambuzi utakapofanywa kwa usahihi na watu sahihi katika maeneo sahihi na kuondoa kero ambazo zinalalamikiwa sasa na kusababisha baadhi kutukanana.

Licha ya kwamba baadhi wameanza kutupa maneno kwa Edo kuhusu maoni yake, bado alichosema kinaishi na ni muhimu wakati huu ambao uchambuzi unazidi kukua nchini. Tusipochukua tahadhari sasa, uchambuzi utapoteza thamani na hao wamiliki wa vyombo vya habari hawataona tena umuhimu wa kuwa na lundo la watu studio kuchambua matukio, huku wasikilizaji wakikerwa na kupungua.

Nafasi ya uchambuzi katika maendeleo ya michezo ni muhimu, lakini isitumiwe vibaya kwa kusakama watu au kikundi, kufanikisha maslahi binafsi, kushabikia, kuchambua bila ya kuwa na ujuzi au namna yoyote ile mbaya isiyonufaisha michezo.

Bravo Dogo Edo!