Kifo cha Charles Hillary chawaliza wengi

Muktasari:
- Gwiji huyo wa utangazaji aliyejipatia umaarufu kwa kutangaza mechi za soka, alikumbwa na mauti alfajiri ya leo wakati akiwa njiani kupelekewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tawi la Mloganzila.
MWILI wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hillary aliyefariki dunia alfajiri ya leo, unatarajiwa kuagwa kesho Jumanne kabla ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi, huku msiba huo ukiwa umewashtua wengi wakiwamo wadau wa tasnia ya utangazaji na michezo waliomlilia na kuelezea alivyokuwa enzi za uhai wake.
Gwiji huyo wa utangazaji aliyejipatia umaarufu kwa kutangaza mechi za soka, alikumbwa na mauti alfajiri ya leo wakati akiwa njiani kupelekewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tawi la Mloganzila.
Mapema leo asubuhi, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said, alinukuliwa akithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba wa gwiji huyo wa utangazaji nchini.
Marehemu Charles alizaliwa Zanzibar miaka 66 iliyopita eneo la Jang’ombe na mwaka 1968 alihamia jijini Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Msingi ya Ilala Mchikichini na kuendelea na masomo ya juu kabla ya mwaka 1980 kujiunga na Redio Tanzania (RTD)na kuitumikia hadi 1994 alipojiunga na kituo binafsi cha Radio One Stereo kinachomilikiwa na IPP.
Akiwa Redio One alitamba zaidi na kipindi cha Charanga Time kilichombatiza jina la Mzee wa Macharanga, mbali na kipindi cha Chemsha Bongo, kilichompa jina la Mzee wa Kipusa.
Mwaka 2003 aliondoka nchini na kujiunga na Radio Deusch Welle (DW) nchini Ujerumani, na miaka mitatu baadaye alijiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa Idhaa ya Kiswahili na mwaka 2015 alirejea nchini na kujiunga Azam Media ambako alifanya kazi hadi 2021 akiwa Mkuu wa Idara ya Redio Uhai (UFM) kabla kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar hadi mauti yalipompata leo.

VIGOGO WAMLILIA
Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wa X, alitoa salamu za rambirambi kwa msiba huo mzito kwa kuandika; “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Bw. Charles Hilary, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar kilichotokea leo Mei 11, 2025.
Ninatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, familia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wote wa sekta ya habari nchini kwa msiba huu.
Ndugu Charles Hilary atakumbukwa kwa mchango wake adhimu wa zaidi ya miaka 40 katika kukuza sekta ya habari nchini tangu akiwa redioni hadi kwenye televisheni, pamoja na unasihi kwa wanahabari wachanga.
Namuomba Mwenyezi Mungu aijaalie familia yake uvumilivu na subra katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho ya mpendwa wetu mahala pema.
Hakika sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.”
Viongozi wengio

WASIKIE WATANGAZAJI
Mtangazaji mkongwe Aboubakar Liongo aliyewahi kufanya kazi na gwiji huyo alisema; “Charles Hillary alitupokea RTD mwaka 1991 nikiwa na wenzangu kama marehemu Swedi Mwinyi, Eshe Muhidini na wengine wengi, hakuwa mchoyo alihakikisha tunakuwa watangazaji bora.”
Lyongo alisema walifanya kazi kwa muda na mkongwe huyo RTD kisha wakaibukia Radio One.
“Walikwenda kuanzisha Redio One, wakiwa Charz (Hillary), marehemu Julius Nyaisanga na Mikidadi Mahmoud, kisha walitufuata chuoni mimi na Pascal Mayalla tukawa tunaogopa kwenda kujiunga na hiyo redio, hivyo wakaenda kuzungumza na baba yangu na baada ya kujiunga nao ilibidi ITV ilipe pesa ambayo serikali ilikuwa imenisomesha, lakini zote hizo zilikuwa juhudi zake,” alisema Lyongo na kuongeza;
“Baadaye alikwenda Ujerumani (DW) alipoondoka kwenda BBC nikaenda DW kubadili nafasi yake, kwa kifupi alikuwa mcheshi, ila makini sana kufanya kazi zake, juzi Jumamosi alinipigia simu alikuwa ananiuliza kama nimeishamtafutia bendi Mbaraka ambaye alikuwa mpiga tarumbeta wa bendi ya Sikinde nikamjibu bado akaniambia nilishughulikie hilo kwa uharaka, tulikuwa tunacheka na sikujua kama anaumwa zaidi ya kushtushwa na taarifa zake za kifo.”
Mtangazaji wa Azam na muandaaji wa tamthilia ya Mwaipopo, Baraka Mpenja alisema: “Hillary alikuwa muungwana kati ya vitu vilivyowahi kunishangaza wakati anatoka BBC kuja Azam wengi walimtarajia angekuja kutangaza mpira wa miguu, ajabu akaishia kutangaza mechi mbili ya Simba na Yanga ile ya kampa kampa tena na Real Madrid dhidi FC Barcelona.
“BaaDa ya mechi ya Simba na Yanga akaniuliza Mpenja umeuonaje utangazaji wangu wa leo, nikamjibu umetangaza vizuri sana Anko, akaniambia hapana nimekosea nilikuwa siwezi kuendana na kasi ya picha, kisha akaniambia napenda mtu anayeniambia ukweli na siyo kuniogopa, baada ya mechi na Madrid na Barcelona akarudia kuniuliza swali lile lile nikajibu kama mwanzo akasisitiza hajafanya vizuri hivyo anatuachia vijana ambao tunaweza kwenda na kasi ya picha na matukio.
Mpenja aliongeza kwa kusema; “Pamoja na ukubwa wa jina lake aliishi maisha ya kawaida, mcheshi, mwalimu mzuri, alikosoa kwa haki na kukupa plani B ambayo alikuwa anaifuatilia, ukipatia anakupa moyo na kusisitiza nidhamu na kujituma, kubwa zaidi alisisitiza tufurahie kila sekunde ya uhai wetu bila kujali kama una pesa nyingi au huna.”

WANASOKA NAO
Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema, Hilary alikuwa muungwana, mcheshi na alipenda wengine wafanikiwe, kubwa zaidi alikosoa vitu kwa haki bila kupendelea mtu kutokana na hadhi yake.
“Enzi zetu redio ilikuwa moja ya RTD (sasa TBC Taifa), hivyo tulikuwa tunaongozana naye katika majukumu ya Taifa Stars, alikuwa mbunifu, nidhamu na kupenda wengine wafanikiwe, watangazaji wa sasa licha ya nyakati kubadilika yapo mengi wanapaswa kujifunza kutoka kwake, kitendo cha kupewa nafasi Ikulu waliona nidhamu yake,” alisema Mogella.
Winga wa zamani Majimaji, Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garrincha’ alisema, Hilary alikuwa mwalimu na aliujua vizuri mpira wa miguu katika utangazaji wake hakuwa na upande alifanya vitu kwa haki, kuhakikisha jamii inayomsikiliza inapata taarifa sahihi na zenye kujenga.
“Ili kuthibitisha hilo Ikulu sio kila mtu anaweza akapata nafasi ya usemaji, hilo lilitokana na kuzingatia maadili ya kazi yake ilikuwa na tija katika jamii, angalau ninayeona anaweza akafuata nyayo za Hilary na Mwinyi ni Mpenja pia ana kazi kubwa ya kufanya, ushauri wangu watangazaji waache mihemko, jamii inawategemea katika habari za kweli na siyo upotoshaji,” alisema.
Kwa upande wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Stars,Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema Hillary ndiye aliyempachika jina la utani, ilikuwa mwaka 1987 akiwa African walicheza dhidi ya Miembeni katika mashindano ya CCM Kitaifa.
“Kutokana na kiwango cha juu nilichokionyesha katika mchezo huo ndipo akawa anatangaza kwamba huyo ndiye Mmachinga kwa sababu natokeo Mtwara, alikuwa rafiki yangu, mahiri, mbunifu na utangazaji wake ulikuwa na radha, apumzike kwa amani,” alisema Mmachinga ambaye rekodi yake ya mabao 26 ndani ya msimu mmoja aliyofunga 1999 haijavunjwa hadi sasa.
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini na nyota wa zamani wa Yanga na Stars, Ally Mayay alisema kifo cha gwiji huyo kimemshtua na kwamba taifa limepoteza hazina kubwa.
“Tumempoteza mtu muhimu katika jamii, nakumbuka nikichambua Azam alikuwa anafuatilia neno moja baada ya lingine, nikikosea ananiambia ukweli, alijua vizuri Kiswahili, alikuwa na data za kutosha kitu ambacho kwa zamani haikuwa kitu rahisi,” alisema Mayay.