SIO ZENGWE: Chama, Morrison wanazishusha hadhi Simba, Yanga

MOJA ya mijadala ambayo huibuka na kupotea ni ule unaozungumzia ukubwa wa klabu za Simba na Yanga, si tu katika soka la Tanzania, bali hata barani Afrika.

Wapo wanaozungumzia mwenendo wa sasa wa Simba katika michuano ya Afrika ambao umeifanya hadi ifikiriwe kushiriki michuano mipya ya Super League ya Afrika na wapo wanaojadili rekodi za kutwaa makombe. Kila mmoja anaeleza moja ya hizo hoja ndizo zinaifanya klabu kuwa kubwa.

Huu mjadala huibuka kulingana na mazingira ya wakati huo na kupotea bila ya sababu za msingi. Pande zote zinaweza kuwa sahihi, lakini usahihi huo hautakuwa na maana kama klabu hizo mbili zinafanya vitendo ambavyo klabu kubwa haziwezi kuvifanya.

Katika moja ya vipindi vya Kona ya Mwanaspoti vinavyorushwa na YouTube ya Mwanapoti kila Ijumaa na Jumatatu, niliwahi kuzungumzia tafsiri ya klabu za Simba na Yanga kumgombania mchezaji mwenye vituko kama Bernard Morrison.

Katika kipindi hicho nilieleza kuwa kama kuna vitu vinazifanya Yanga na Simba ziendelee kuonekana kuwa ni klabu ndogo, basi ni jinsi zilivyoingia kwenye mgogoro wa Mghana huyo kiasi cha kufikishana Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS) na kupokonyana mchezaji huyo, ambaye sasa amerudi Yanga.

Kitendo cha mchezaji kwenda Shirikisho la Soka (TFF) kudai amesikia Yanga wana mkataba wa miaka miwili zaidi na kweli TFF ikagundua mkataba ulikuwepo ila una kasoro, kilitosha kuifanya Yanga igundue kuwa kuna tatizo kwa Morrison, hivyo kuachana kabisa na biashara yake.

Lakini katika kutotaka kushindwa na Simba, ambayo baadaye ilimsajili Morrison, Yanga ikapambana kumrudisha. Hata Simba hakuondoka vizuri. Kulianza msuguano wa chinichini na baadaye kuachana nayo.

Mashabiki wa Yanga walishangilia kurejea kwa Morrison kama ambavyo mashabiki wa Simba walishangilia kurejea kwa Cloutus Chama kutoka RS Berkane baada ya kuondoka klabu hiyo katikati ya mgogoro ulioanza kukua baina yake na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji kuhusu sakata la Haji Manara.

Leo hii, Yanga hawaelewi ni kwa jinsi gani uongozi wa Yanga unashughulika na Morrison ambaye amerejea mwishoni mwa wiki iliyopita akitokea mapumzikoni kwao nchini Ghana.

Uongozi umeshindwa kueleza bayana nini kilitokea hadi akawa na ruhusa maalum tofauti na wachezaji wenzake, huku Kocha Nasreddine Nabi akiendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi ngumu za kumalizia msimu na zile za michuano ya Kombe la Shirikisho, ambazo ni mtihani mkubwa kwa Mtunisia huyo.

Bila shaka kuna usumbufu unaofanywa na Mghana huyo ambao ukiwekwa bayana itakuwa ni aibu kwa uongozi. Lakini kosa lilishafanyika katika kuhangaika naye ili kumrudisha Jangwani licha ya vituko ambavyo si rahisi kufanywa katika dunia ya sasa ya soka, achilia rekodi yake ya jinai inayomfanya asiruhusiwe kuingia Afrika Kusini.

Kwa wenzetu hata kumpiga paka wako tu ni kosa linaloweza kuathiri mkataba wako, achilia mbali mikataba binafsi ya chapa za kampuni mbalimbali.

Wiki iliyopita kulikuwa sakata la Chama kufanyiwa mabadiliko dakika ya 30 ya mchezo baina ya Simba na Mbeya City, ambao vijana hao wa Mbeya walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, hasa katika kiungo.

Uwanja ulitoa mguno usio wa kawaida kuona kiungo huyo Mzambia anatolewa hata kabla ya kipindi cha kwanza kuisha, akiwa ndio kwanza ametoka kutoa pasi ya bao lililofungwa na Said Ntibanzokiza.

Kwa jicho la kimpira, Chama hakuwa anaisaidia timu katika kiungo, hasa upande wa kulia ambako Salum Kihimbwa alionekana kutawala na kumsumbua beki Shomari Kapombe, ambaye hakuwa anapata msaada wa kutosha kutoka kwa Chama aliyekuwa akicheza upande wa kulia wa kiungo.

Mashabiki walishangaa na kumrushia maneno Robertinho, kiasi cha kudiriki kusema hata kama timu inaongoza Chama hatakiwi kupumzishwa—ni maneno ya mashabiki lakini unaweza kuona tafsiri yake katika taarifa za uongozi na hata kocha mwenyewe.

Kwanza kocha alishangilia kwa nguvu kiasi cha kupiga magoti, akiwa amegeukia mashabiki baada ya Sakho kufunga bao la tatu. Anaweza kutoa sababu nyingine za shangwe zake, lakini kwa tafsiri ya haraka, aliona kama Sakho amemsaidia kujibu lawama za mashabiki dhidi ya kutolewa kwa Chama. Sakho aliingia kuchukua nafasi ya Chama.

Ni kama lile tukio la kocha wa Misri kumtoa Mido katika mechi ya fainali za Mataifa ya Afrika halafu mbadala wa Mido akafunga bao. Kocha alishangilia akijipigapiga kifua kuonyesha alifanya uamuzi sahihi wa kumbadilisha Mido, ambaye wakati huo alikuwa nyota wa Misri akicheza soka nchini England.

Baadaye Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, alisema kile kilichokuwa kinasemwa na mashabiki, kuwa ‘eti’ kila mtu alishangaa Chama kutolewa, lakini wenye subira walisubiri nini kitatokea mwishoni.

Kuna haja gani kwa viongozi na watendaji wa klabu kushangaa Chama kubadilishwa na baadhi yao kusubiri ambacho kingejiri? Yaani kama Sakho asingefunga bao, nao wangeona kulikuwa na kasoro katika hayo mabadiliko?

Hata ile taarifa iliyosambaa baadaye ikimkariri kocha kuwa anakubali kuwa alifanya makosa, pia ni uthibitisho Chama amekuwa mkubwa kuliko timu na hawezi kuanzia benchi, kupumzishwa au kutopangwa hata kama kocha atamwona mazoezini kuwa ameshuka kiwango au uchezaji wake haulingani na mpinzani wanaetarajia kukutana naye na hivyo hatakiwi kupangwa.

Ni woga dhidi ya mashabiki, ni woga wa kupoteza kibarua, ni ukosefu wa ujasiri na mengine mengi.

Nimesikia hata Yanga wanaeleza jinsi Morrison atakavyofanya vizuri katika mechi za kuelekea mwishoni mwa msimu na zile za Kombe la Shirikisho.

Kwamba Morrison ana mechi zake, kwa hiyo zile za kwenda Mwanza au Ihefu kucheza na wenyeji si zake kama alivyofanya mara ya kwanza alipokuwa akiichezea Yanga, alipogomea safari ya Kanda ya Ziwa na baadaye kupelekwa kwa ndege akiwa na kiongozi wa klabu.

Sidhani kama Simba au Yanga zilitakiwa kutoa taarifa za jinsi ile kuhusu mchezaji mmoja, hasa ikizingatiwa wengine walikuwa watiifu na wako kambini na wanakubaliana na mipango ya mwalimu nani aanze na nani atokee benchi au abadilishwe kwa muda ambao mtaalamu anaona ni sahihi.

Ukiangalia matukio hayo yote, ni dhahiri Simba na Yanga bado ni klabu ndogo na zenye safari ndefu ya kifikia uamuzi wa kumwondoa mchezaji kwa sababu tu amempiga paka wake—hiyo ni hatua kubwa mno!

Kauli za klabu na kocha kuhusu wachezaji wanaoonekana kuwa na tatizo zinaonyesha udogo wa klabu hizi kongwe nchini. Na Fei Toto ameingia katika kundi hilo.

Anaweza kuzifanya ziwe ndogo zaidi ya tunavyoziona sasa!