Kinachosubiriwa ni ndoa ya Foden na Rebecca
Muktasari:
- Foden ameendelea kungara ndani ya uwanja kwa kuonyesha kiwango kizuri lakini maisha yake nje ya soka akiwa na Rebecca nayo yamekuwa yakivuta hisia za mashabiki wengi duniani.
KIUNGO wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Phil Foden (25), ana simulizi nzuri kuhusu safari yake ya uhusiano na mpenzi wake Rebecca Cooke (24) hadi kuwa baba wa watoto watatu akiwa bado kijana.
Foden ameendelea kungara ndani ya uwanja kwa kuonyesha kiwango kizuri lakini maisha yake nje ya soka akiwa na Rebecca nayo yamekuwa yakivuta hisia za mashabiki wengi duniani.
Wawili hao ni wapenzi wa muda mrefu waliokutana tangu wakiwa shuleni hivyo uhusiano wao umedumu kwa miaka mingi licha ya changamoto mbalimbali zinazowakumba watu maarufu hasa vijana. Tofauti na mastaa wengi, Rebecca amechagua kuishi maisha ya faragha na kuepuka drama zinazoweza kuletwa na vyombo vya habari na mitandao inayosaka udaku kutoka kwa watu wenye ushawishi.
Hii ndiyo sababu hata mitandao yake ya kijamii ikiwemo Instagram ameifunga (private account) ili isifikiwe na mashabiki, jambo linaloonyesha namna anavyothamini maisha yake binafsi.
Pamoja na ukimya wake Rebecca ameonekana mara kadhaa akimuunga mkono Foden katika mashindano makubwa kama UEFA Euro 2024 na Kombe la Dunia 2022 akijiunga na kundi la wake na wapenzi wa wachezaji maarufu (WAGs).
Uhusiano wao umezaa matunda makubwa kwani wawili hao tayari wana watoto watatu ambapo mtoto wao wa kwanza Ronnie alizaliwa Januari 22, 2019 wakati huo Foden akiwa na umri wa miaka 18 tu.
Akizungumzia kuhusu kuzaliwa kwa mtoto wake huyo wa kwanza Foden aliwahi kusema alishuhudia tukio hilo jambo lililomfanya kutokwa na machozi.
“Nilikuwepo wakati wa kujifungua. Nilitoka kidogo nje nikalia kidogo kisha nikarudi kama hakuna kilichotokea. Mimi si mtu wa kulia mbele ya watu, napenda kuwa peke yangu lakini ilikuwa ni moment ya kipekee,” alisema Foden.
Aliongeza kuwa kutokana na majukumu ya soka kuna mambo hukosa kuyaona katika ukuaji wa mtoto wake kama vile hatua ya kwanza ya kutembea.
Ronnie alipata umaarufu mwishoni mwa msimu wa 2022/2023 baada ya kuonekana akisherehekea mafanikio ya timu ya baba yake (Man City). Kwa sasa ana wafuasi zaidi ya milioni 4.1 katika ukurasa wake wa Instagram unaosimamiwa na wazazi wake.
Kufikia Julai 2021 walijaliwa mtoto wa pili ambaye ni wa kike na walimpa jina la True. Baadaye walitangaza ujauzito wa mtoto wa tatu Aprili 2024 kwa kufanya sherehe ya baby shower.
Mtoto huyo alizaliwa Juni 27, 2024 lakini hadi sasa jina lake halijawekwa hadharani.
Kuzaliwa kwake kulikuwa na uzito mkubwa kiasi kwamba Foden alilazimika kuondoka kambini mwa timu ya taifa ya England wakati wa michuano ya Euro 2024.
Hatua hiyo ilithibitishwa na The Football Association ambayo ilieleza kuwa alirejea nyumbani kutokana na dharura ya kifamilia. Tukio hilo linathibitisha namna Foden anavyothamini familia yake licha ya majukumu makubwa aliyonayo.
Foden pamoja na familia yake wanaishi Bramhall, Manchester katika nyumba yenye thamani ya Pauni 2 milioni (takriban Sh6.4 bilioni).
Licha ya maisha ya kifamilia yenye furaha uhusiano wa Foden na Rebecca haujakosa changamoto. Mwaka 2020 Foden alikumbwa na tuhuma za usaliti baada ya kuripotiwa kuingiza wasichana wawili katika chumba chake cha hoteli.
Mwaka 2022 wawili hao walionekana wakibishana vikali wakiwa mapumzikoni Corfu jambo lililoibua mjadala kuhusu hali ya uhusiano wao. Hata hivyo wameendelea kuwa pamoja na kuonyesha mshikamano.
Novemba 2025 ziliibuka tetesi kuwa wawili hao wapo mbioni kufunga ndoa baada ya kuonekana wakinunua pete katika duka la vito la Empire Fine Jewellers lililopo Wilmslow, Cheshire.
Dukani hapo Foden na Rebecca walikuwa wakitazama pete mbalimbali hali iliyochochea uvumi kuwa huenda harusi iko karibu lakini hadi sasa ndoa bado haijafungwa.
Tetesi hizo zilianza mapema 2025 baada ya Rebecca kuonekana akiwa amevaa pete kubwa ya almasi kwenye kidole chake huko Paris, Ufaransa wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
Chanzo kimoja kililiambia SunSport Februari 2025 kuwa wawili hawa ambao wamekuwa pamoja tangu ujana sasa ni wakati wa kuchumbiana.
“Alimpeleka Paris kwa ajili ya mkesha wa mwaka mpya na waliporudi Rebecca alikuwa na pete ya almasi inayong’ara kwenye kidole chake. Pete hiyo ni kubwa sana, ni almasi kubwa mno. Anaipenda sana na anajivunia kuivaa ingawa hajatangaza rasmi chochote,” chanzo hicho kilieleza na kuongeza:
“Lakini wake na wapenzi wa wachezaji pamoja na wachezaji wote wa Man City wanafahamu kuhusu pete hiyo na kila mtu anasubiri kwa hamu tangazo rasmi labda la uchumba au ndoa.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali familia na marafiki wa karibu wa Foden na Rebecca wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuona wakichukua hatua hiyo kubwa.
Ikiwa ndoa itafungwa inatarajiwa kuwa sherehe kubwa itakayohusisha mastaa wa soka, watu maarufu na marafiki wa karibu.