Simba, Yanga wapewa mchongo CAF

Hakuna namna, lazima kushinda na tusifungwe, ni kauli za makocha na wachezaji wa zamani wakiueleza mchezo wa kesho wa Simba na Wydad na ule wa Yanga dhidi ya Medeama keshokutwa.

Mechi hizo ni nafasi ya mwisho wa vigogo hao wa soka nchini kuamua hatma yao ya kufuzu robo fainali kwenye mashindano ya kimataifa au la!.

Yanga ni ya mwisho kwenye kundi D ikiwa na pointi mbili ilizovuna kwe mechi tatu ilizocheza hadi sasa na kupata sare mbili na kufungwa, katika mechi hizo imepachika mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara matano.

Kinara wa kundi hilo ni Al Ahly yenye pointi tano, ilizovuna kwenye mechi tatu, ikishinda moja, sare mbili huku ikipachika mabao manne na kufungwa bao moja.

CR Belouizdad ni ya pili kwenye kundi ikiwa na pointi nne baada kushinda mechi moja, sare moja na kufungwa mara moja, yenyewe imepachika mabao manne na kufungwa mawili.

Medeama ya Ghana ni ya tatu baada ya kuvuna pointi nne pia kwa matokeo ya sare moja, imeshinda na kufungwa mara moja, ina mabao matatu ya kufunga na matano ya kufungwa.

Simba iliyo kundi B pia ni ya mwisho ikiwa na pointi mbili kwenye mechi tatu, ikipoteza moja na kutoka sare mara mbili, katika mechi hizo imefunga bao moja na kufungwa mawili.

Mchezo huo ni wa mwisho, ukitajwa na baadhi ya makocha kuonyesha njia kwa timu hizo kufufua matumaini ya kusonga kwenye mashindano ya kimataifa.

Baadhi ya makocha walisema hakuna namna nyingine kwa Yanga na Simba kuwa na matumaini ya kusonga mbele zaidi ya kushinda mechi hizo.

"Hii ni last chance (nafasi ya mwisho) waitumie kufa na kupona, wakifungwa mechi hizo basi itakuwa hakuns namna," alisema kocha Adolf Rishard.

Kocha huyo na nyota wa zamani wa timu ya Taifa alisema makocha wa timu hizo wana-game plan (mbinu za mchezo) lakini wanapaswa kuwa na mfumo wa tahadhali na kuhakikisha wanapata goli la mapema,"alisema.

Alisema Yanga na Simba lazima washinde na wasifungwe, hicho ndio kitawasaidia.

"Nikiziangali timu hizi mbili na wapinzani wao, naiona Yanga ikiwa na uhakika wanayo sababub hata gemu iliyoisha walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia kulinganisha na Simba ambayo ilitengeneza chache.

"Wydad tekinikali ni wazuri, wanaweza kukufunga kwao au ugenini, wana takitiki nzuri, wanafungua pembeni kifupi ni timu nzuri ina wachezaji wazuri, Simba inapaswa kuchukua tahadhari zaidi.

"Kupata matokeo mazuri inawezekana, lakini kazi ya ziada ifanyike," alisema.

Kocha mwingine, Fred Felix Minziro alisema
Simba na Yanga zina uwezo wa kushinda mechi hizo.

"Hasa kwa Simba ambayo naiona imerudi na kuanza kutengemaa, timu hizi zikijipanga vizuri zitafanya vizuri, ingawa mechi zijazo kwa zote mbili, kama nilivyosema hakuna namna zaidi ya kupata matokeo mazuri kwa kucheza kufa na kupona.

Kocha Charles Mkwassa alisema mambo matatu yanaweza kuzisaidia  timu hizo kupata matokeo mazuri wakati huo huo wakihakikisha wanashambulia lakini wasijiachie.

"Kuna msemo unasema huwezi kwenda kuiba kwa watu wakati mlango wako umeuacha wazi, hivyo ni lazima tufunge lakini tusifungwe," alisema kocha huyo na kuendelea.

"Tukifungwa mechi hizo ni lazima tutakaa kwenye mstari mwekundu,  ingawa chance  (nafasi) za kufanya vizuri na kusonga zipo na timu zetu zimeonyesha tangu mwanzo kuwa zinaweza ni kujipanga tu,".

Alisema njia za kuiweka timu salama ni kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa na ni njia sahihi pia ya kujilinda, vilevile kujilinda kwa kuzuia na kuwanyima nafasi wapinzani kucheza mipira ya kaunta, krosi na mashambulizi mengine.

"Kitu cha tatu ni kupata goli la mapema, ukifunga mapema unacheza kwa kurelax na kuwapa presha wapinzani," alisema.

BENCHIKHA, GAMONDI WANENA

Wakati Watanzania wakihesabu saa kujua hatma za timu hizo mbili, makocha wa timu hizo wameeleza mipango yao na namna walivyojipanga.

Abdelhak Benchikha wa Simba alisema wanaiheshimu Wydad Ac watacheza kwa umakini na tahadhari lakini kwa lengo la kupata pointi tatu.

Alisema kila mchezaji anafahamu hilo, kama timu haijapata matokeo mazuri na kitu pekee ambacho kinaweza kufufua matumaini ni ushindi.

"Hii kwetu ni kama fainali, hatuna kitu kingine ambacho tunasubili zaidi ya kupata pointi tatu, nawaandaa wachezaji kwa lengo la kupata ushindi, mashabiki wetu wajitokeze kutupa sapotii,"alisema Benchikha.

Naye Miguel Gamondi wa Yanga alisema hakuna namna nyingine katika mechi yao ya kesho zaidi ya ushindi.

"Tuna mechi hapa nyumbani kwahiyo tunatakiwa kuzitumia vizuri kupata ushindi ili kuweza kwenda kwenye hatua inayofuata,"alisema Gamondi.

Mfadhili wa Yanga, GSM amenunua tiketi za mzunguko katika mchezo wao ujao dhidi ya Medeama.

TANGU 2020/21 REKODI ZIKO HIVI
Katika misimu mitatu iliyopita, kuanzia wa 2020/21 Simba imekuwa ikifanya vizuri, msimu huo ilifika robo fainali baada ya  kuifunga Plateau United ya Nigeria bao 1-0 ugenini na kutoka nayo suluhu nyumbani,

Kisha  FC Platnum ya Zimbabwe mabao 4-1, ikichapwa ugenini bao 1-0 lakini ikashinda nyumbani mabao 4-0 na kufuzu makundi.

Ilimaliza kinara kwenye kundi A ikiwa na pointi 13 baada ya kuifunga Al Ahly ya Misri nyumbani bao 1-0 licha ya kuchapwa ugenini 1-0.

Simba iliifunga  AS Vita ya DR Congo bao 1-0 ugenini na mabao 4-1 nyumbani. ilisuluhu 0-0  na Al Merrikh ya Sudan  ugenini 3-0 nyumbani, ikafungwa na Al Ahly 1-0 ugenini na ikalipiza kisasi nyumbani ikishinda 1-0 na ilitinga robo fainali.

Simba kwenye robo fainali ilikwaa kisiki baada ya kuchapwa mabao 4-0 ugenini na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini Mei 15, mwaka jana lakini ikashinda mabao 3-0 nyumbani katika mchezo wa marudiano uliofanyika Mei 22 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, ila ikatolewa.

Msimu uliofuatia wa 2021/22 ilishindwa kufurukuta baada ya kutolewa kwenye raundi ya pili ya mashindano hayo kwa bao la ugenini.

Ilianza kwa kushinda ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana mabao 2-0 lakini ikafungwa nyumbani 3-1 na kwenda Kombe la Shirikisho.

Ilicheza hatua ya mtoano dhidi ya Red Arrows ya Zambia na kushinda 4-2 na kutinga hatua ya makundi ambapo ilipangwa kundi moja na RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na USGN ya Nigeria.  

Simba ilishika nafasi ya pili kwenye kundi hilo baada ya kukusanya pointi 10 sawa na Berkane iliyokuwa kinara  na timu zote mbili zilifanikiwa kufuzu robo fainali.

Kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, Simba ilishindwa kufurukuta baada ya kulala kwa penalti 4-3 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini baada ya timu hizo kila moja kushinda kwa bao 1-0 katika uwanja wake wa nyumbani.

Msimu wa 2022/23 Simba kwenye raundi ya kwanza ilimfunga  Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kumfunga 2-0 nyumbani na ugenini 2-0.

Katika raundi ya pili ambayo Simba ilihitaji kwenda kusonga mbele, timu hiyo ilicheza na Petro de Agosto na ilitinga makundi kwa jumla ya mabao 4-1, mchezo wa kwanza ikishinda 3-1 na ugenini 1-1.

Hatua ya makundi walipangwa kundi C  ilimaliza nafasi pili ikiwa na pointi tisa  huku kinara ikiwa Raja CA na kutinga hatua ya robo fainali.

Simba ilitinga robo fainali lakini ilitolewa ilipokutana na  Wydad AC, mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa Mkapa ilishinda 1-0, mchezo uliochezwa nchini Morocco ilifungwa 1-0 kisha kwenye mikwaju ya penalti, Wekundu hao wa Msimbazi walitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Upande wa Yanga, msimu wa 2019/20 ilianza kwenye hatua ya awali na iliifunga Township Rollers kwa jumla ya mabao 2-1. mchezo wa kwanza  1-1 kisha marudiano 1-0.

Yanga ilitolewa raundi ya kwanza na Zesco Utd kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya mechi ya kwanza kutoka 1-1, kisha mchezo wa pili ikafungwa 2-1.

Msimu wa 2021/22 Yanga ilitolewa hatua ya kwanza kwenye  Ligi ya Mabingwa na Rivers United baada kufungwa kwa jumla ya mabao 2-0, ikifungwa 1-0 nyumbani na 1-0 ugenini.

Msimu wa 2022/23 Ligi ya Mabingwa, Yanga ilianzia raundi ya kwanza na kuichapa  Zalan 9-0, kisha ikatinga hatua ya raundi ya pili ikakutana na Al Hilal ya Sudan, mchezo wa kwanza ilitoka sare 1-1, kisha ugenini ikafungwa 1-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.

Yanga baada ya matokeo hayo ikaangukia kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza kinara wa kundi D ikiwa kinara na pointi 13.

Timu hii ilicheza hatua ya robo fainali dhidi ya Rivers Utd na ilishinda 2-0 nyumani na ugenini 2-0 kisha ikatinga hatua ya nusu fainali na kukutana na Marumo Gallants.

Kwenye nusu fainali mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa Mkapa ilishinda 2-0, ugenini ikashinda 2-1 na kufanya matokeo yawe jumla 4-1 na kutinga fainali.

Fainali Yanga ilikutana na USM Alger na mchezo wa kwanza Yanga ilifungwa 2-1, mchezo wa marudiano Yanga ikashinda 1-0 lakini ikamaliza mshindi wa pili na Alger ikachukua ubingwa.

MECHI NYINGINE ZA MAKUNDI SIMBA NA YANGA

ASEC vs Simba (Februari 23)
Simba vs Jwaneng Galaxy (1 Machi)
Yanga vs CR Belouizdad (Februari 23)
Al Ahly vs Yanga (Machi 1)