Simba, Yanga kanyaga twende kimataifa

NI hesabu tu!! Wawakilishi wa Tanzania, Simba na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika wapo kwenye hekaheka za kutupa karata zao za kwanza katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Kimataifa.

Vigogo hao wa soka la Tanzania, wataanzia ugenini, Jumamosi ya Februari 11, Simba iliyopo kundi C kwenye Ligi ya Mabingwa itakuwa Conakry, Guinea kwenye Uwanja wa General Lansana Conte kuanza safari ya kuvuka hatua ya makundi dhidi ya wenyeji wao, Horoya Athletic Club.

Siku inayofuata, Jumapili ya Februari 12, Wananchi nao watatupa karata yao ya kwanza kwenye Uwanja wa Stade Olympique Hamadi Agrebi, uliokuwa ukiitwa Stade 7 Novemba uliopo Rades, Tunis, Tunisia takriban kilomita 10 Kusini-Mashariki mwa jiji la Tunis, katikati mwa Jiji la Olimpiki kucheza dhidi ya US Monastir.

Hesabu za michezo hiyo, zimeiva kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwani walishatanguliza watu kwa ajili ya kuweka mambo sawa juu ya sehemu ambayo watafikia, chakula ambacho watakula ili kukwepa mitego ya wapinzani wao.

Makocha wa timu zote mbili, Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze na Mbrazil, Roberto Oliveira 'Robertinho' na Juma Mgunda watakuwa wanaumiza kichwa kwa kufanyia kazi mbinu ambazo zitawaletea matokeo chanya kwenye michezo hiyo ambayo huchezwa kwa hesabu kubwa ndani na nje ya uwanja.
Kulingana na ubora na madhaifu yao kwenye michezo yao ya hivi karibuni, hawa ndio wapinzani wa Simba na Yanga kwenye michezo yao ya kwanza ya makundi.

Horoya
Wakati Simba ikiwa imepoteza mchezo mmoja kwenye ligi ya ndani, wapinzani wao, Horoya kwenye ligi ya kwao ambayo ni maarufu kama Ligue 1, wamepoteza mara mbili, wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 29 kwenye michezo 13 ya mzunguko wa kwanza.
Wababe hao ambao wanashikilia rekodi ya kutwaa Ligue 1 mara nyingi zaidi (20), michezo ambayo walipoteza ilikuwa mfululizo ndani ya michezo mitatu iliyopita hivyo Simba inaweza kufanya uchambuzi wa namna ambavyo walipoteza.

Kabla ya kupoteza michezo hiyo mfululizo mwanzoni mwa mwaka huu dhidi ya Hafia (1-0) na Renaissance (1-0), walifunga mwaka jana kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kaloum Star, hivyo ndani ya michezo hiyo mitatu walidondosha pointi nane.
Horoya ilikuja kuzinduka Januari 21, baada ya mwenendo huo mbovu kwa kuishushia mvua ya mabao 4-0, Sequence ambao wanashika nafasi 10 kwenye msimamo wa timu 14.

Miongoni mwa wachezaji hatari wa Horoya ni pamoja na Mohamed Lamine Fofana na Pape Abdou Ndiaye ambao waliivusha timu hiyo kwenye raundi ya pili wakati wa kupigania nafasi ya kutinga hatua ya makundi, walifanya hivyo dhidi ya miamba ya Ivory Coast,  ASEC Mimosas kwenye mchezo wa ugenini (0-1) na nyumbani (1-1).

Hii ni mara ya 13 kwa Horoya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa na katika misimu yao mitano iliyopita, wametinga hatua ya makundi mara nne hivyo inaonyesha kuwa timu yenye uzoefu wa kutosha kwenye michuano hiyo.
Wekundu wa Msimbazi nao hawapo nyuma kwani ndani ya misimu mitano iliyopita wametinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili, itakuwa vita ya timu zenye kuyajua vilivyo mashindano hayo makubwa zaidi ngazi ya klabu Afrika.

Simba ligi ya mabingwa hivi karibuni
2002 - Raundi ya Kwanza
2003 - Hatua ya Makundi (8 Bora)
2004 - Hatua ya Awali
2005 - Raundi ya Kwanza
2008 - Raundi ya Kwanza
2011 - Mchujo maalum kwa hatua ya Makundi
2013 - Hatua ya Awali
2018–19 – Robo fainali
2019–20 - hatua ya Awali
2020–21 - Robo fainali
2021–22 – Raundi ya Pili

US Monastir
Kwa mara nyingine tena, Nabi anarejea nyumbani kwao Tunisia ambako mara ya mwisho alifanya maajabu na kuifanya Yanga itinge hatua ya makundi Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga bao 1-0 Club Africain nchini humo.

Safari hii Yanga itakuwa na kibarua cha kucheza dhidi ya timu ambayo inaongoza msimamo wa Kundi B, kwenye ligi ya Tunisia wakiwa na pointi 25 walizovuna kwenye michezo 11, ikumbukwe kuwa Wananchi nao ni vinara wa Ligi Kuu Bara.

Wakati Yanga ikiwa imepoteza mchezo mmoja, Monastir imepoteza mara mbili huku wakionekana kuwa kwenye kiwango bora kwani ndani ya michezo yao mitano iliyopita wamepoteza mara moja na kushinda michezo minne.
Youssef Oumarou mwenye mabao matano kwenye ligi, ni miongoni mwa wachezaji hatari wa kikosi hicho ambacho huu ni msimu wake wa pili kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika tofauti na Yanga ambao ni wazoefu na michuano hiyo.
 

Yanga shirikisho
2007 - Raundi ya Kati
2008 - Raundi ya Kwanza
2011 - Hatua  ya Awali
2016 - Hatua ya Makundi (8 Bora)
2018 - Hatua ya Makundi (16 Bora).