Simba wako tayari kwa kocha wa La Liga?

Wednesday November 17 2021
simba pic

SIMBA wamemtangaza Pablo Franco Martin kuwa mrithi wa Didier Gomes kama mkuu wa benchi lao la ufundi.

Pablo Franco au Paulo Frank kwa Kihispaniola, ni kocha wa daraja fulani hivi kwa mujibu wa wasifu wake japo kila alikokuwa aliishia kutimuliwa.

Amefundisha katika klabu ya Ligi Kuu ya Hispania, Getafe, japo kwa miezi mitatu, lakini ndo kafundisha.

Na bahati nzuri ni kwamba aliifundisha katika kipindi cha misukosuko kweli kweli kwa sababu alikalia kiti kuanzia mwishoni mwa Februari 2015 akiwa kocha wa tatu ndani ya msimu mmoja.

Katika misukosuko kama hiyo hofu ilikuwa endapo wangenusurika kushuka, lakini bwana Paulo aliwanusuru na kikombe cha kushuka daraja...lakini wenyewe wakamshukuru na kumtakia kila la heri.

Baadaye akaenda kuwa msaidizi wa Julen Lopetegui klabuni Real Madrid, baada ya kuondoka kwa Zinedine Zidane 2018.

Advertisement

Napo hawakukaa sana, waliingia Juni wakatoka Oktoba, baada ya kile kipigo cha 5-1 kutoka FC Barcelona dimbani Camp Nou.


WAKO TAYARI?

Kama ilivyo kauli mbiu ya Azam TV, soka letu kivyetu vyetu, Simba kama klabu nyingine zote za Tanzania ina kasumba ya kutofuata taratibu za kiweledi katika kusimamia na kuendesha soka.

Watu wengi waliozizunguka hizi klabu zetu, wana tatizo kubwa sana hasa linapokuja suala la utawala.

Katika klabu kama Simba, makocha wengi wazungu wamekuja na kuondoka wakilalamikia kukosekana kwa weledi kwa baadhi ya viongozi wenye sauti ndani ya klabu.

Leo ukiambiwa Pablo amefundisha Getafe, timu ya Ligi Kuu ya Hispania, unaweza kuelewa yuko kwenye kiwango gani cha weledi, na anatarajia akute kiwango gani cha weledi hapa kwetu.

Sasa kwa soka letu kivyetu vyetu, kiwango hicho kipo?

Atakuja hapa na kuona kikosi chake halafu atasema anaomba avumiliwe kwa miezi 6 atengeneze timu.

Kumbuka miezi sita ni michache sana, Klopp aliomba miaka minne Liverpool.

Simba wanayo hiyo miezi sita ya kumpa huyu kocha?

Itakuja mechi ya Simba na Yanga, mambo ya wenye timu yao kutaka kukiona mapema kikosi kitakachoanza ili kipelekwe kwa mtaalamu...kocha atakubali?

Mtaalamu akisema leo Kagere asianze kwa sababu hana nyota, kocha ataelewa kweli?

Kufundisha La Liga maana yake unakutana na wachezaji wa daraja la juu ambao wanajua kufuata maelekezo ya mwalimu kwa asilimia zote.

Pablo hana uzoefu za soka la Afrika kwa sababu hajawahi kufundisha soka kwenye bara hili.

Shida kubwa ya wachezaji wa Kiafrika ni kwamba hufuata maelekezo ya mwalimu kwa asilimia chini ya 40 kwenye mechi...zaidi ya asilimia 60 ni vipaji vyao.

Kwa kukosa kwake uzoefu na wachezaji wa kiafrika, Pablo ataweza kweli kuhimili presha ya kuona wachezaji wanafanya wanavyotaka wao kwa asilimia 60 na kuyaacha Yale waliyoyafanyia mazoezi?


IMEANDIKWA NA MZEE WA UPUPU

Advertisement