Simba si ya kuhangaikia viungo kutoka nje
KATIKA maeneo ya uchezaji soka ambayo nchi imekuwa na utajiri nayo sana, basi ni hili la wachezaji wa kati, yaani viungo. Ni eneo ambalo kwa matakwa ya mpira wa sasa, wachezaji wake wamejikuta wakiongezewa majukumu na kugawanywa.
Hapa utawakuta viungo wazuiaji (wakabaji), viungo wachezesha timu na viungo washambuliaji.
Si sasa tu, tangu enzi hizo nchi yetu imebahatika kuwa na wachezaji wa eneo hili wenye vipaji vya hali ya juu, ndio maana imekuwa nadra kuona wachezaji kutoka nje wakija nchini na kucheza maeneo haya ya kati.
Kuna mchezaji mmoja tu ambaye alikuja nchini na kucheza katika nafasi ya kiungo na kutamba akiwa na Simba na Azam FC kwa nyakati tofauti, si mwingine, bali ni marehemu Patric Mutesa Mafisango.
Lakini siku zote tumezoea kupata wachezaji wa nafasi nyingine kwenye soka kama walinda milango, ambapo tangu enzi za Mackenzie Ramadhani wa Simba hadi sasa, kuna kina Razak Abarola wa na wengine.
Kutoka enzi za mabeki kutoka nje kina Constantine Kimanda wa Yanga hadi hawa kina Asante Kwasi, Yussuf Ndikumana na wengineo.
Haikuwa rahisi kipindi hicho kumuona mchezaji wa nafasi ya kati akija nchini na kuchukua namba kirahisi mbele ya kina Ramadhani Lenny, Athumani China, Hussein Marsha, Method Mogella, Ally Maumba, Kassa Mussa, Yussuf Macho na Stephen Mussa.
Tanzania ilikukuwa na hazina ya wachezaji wa idara hiyo na hakukuwa na haja ya kuchukua kutoka nje ya nchi. Walikuwapo wengine kina Hussein Marsha, Khalfan Ngassa, Hamis Thobias ‘Gaga’, Willy Kiango, Idd Selemani ‘Meya’ Idrisa Ngulungu, Carlos Mwinyimkuu na wengineo wengi wa kizazi cha kati na hadi cha juzi cha kina Selemani Matola na Athuman idd Chuji. Haikuwa rahisi.
Ni kwa sababu kizazi hicho vipaji vilikuwa vya hali ya juu na bado wengine wa nafasi hizo ilibidi wahamishiwe kwenda kucheza katika maeneo kama ilivyokuwa kwa Said Mwamba ‘Kizota’, Issa Athumani Mgaya waliohamishiwa eneo la ushambuliaji, au Ali Mayai, Nico Bambaga, Method Mogela waliohamishiwa kwa muda fulani nafasi za ulinzi.
Bado kipindi hicho hakukuwa na jina la kiungo mshambuliaji badala yake tulikuwa na washambuliaji wa pembeni au mawinga ambapo nchi ilijaaliwa kuwa na wachezaji wengi mno wenye vipaji.
Wakumbuke kina Edibily Lunyamila, Justine Simfukwe, Thomas Kipese, Celestine ‘Sikinde’ Mbunga, Beya Simba na wenzao, hivyo haikuwa rahisi kumleta kiungo kutoka nje kuchukua nafasi za viungo asilia.
Bado nafasi hiyo kwa imeendelea kuwa na wachezaji wengi katika kizazi hiki wenye vipaji vikubwa.
Bado nchi haihangaiki kutafuta wachezaji wa eneo hilo. Ukizingatia kuwa kizazi cha sasa kinakosa wachezaji wenye miili mikubwa, wachezaji wapambanaji wengi ni waoga wa kupambana hivyo wanakimbilia eneo hilo.
Unaweza usiamini kabisa kuwa moja kati ya timu zenye wachezaji wengi wenye vipaji katika eneo hilo ni Simba. Kwa miaka mingi, Simba imekuwa na hazina kubwa ya wachezaji wa eneo la kati ambao uwezo wao bado ukiwalinganisha na wanaopatikana kwenye timu nyingine, wao wapo juu zaidi.
Simba ina viungo wazuri kina Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na hata Erasto Nyoni ni kiungo pia, hao ni wazawa.
Kisha waweke wageni; James Kotei, Haruna Niyonzima na Nicholas Gyan, unaiona Simba ikiwa tajiri kabisa kwa wachezaji wa kati walio na uwezo mkubwa wa kuisaidia timu muda mrefu.
Katika hali hiyo, unasikia fununu za kusajili wachezaji wa eneo hilo kina Hassan Dilunga au huyu mgeni Kakulu Mugheni Fabrice, unajiuliza nini shida ya Simba kipindi hiki?
Huku ni kujaza nafasi au kuangalia mapungufu ya timu na kusajili? Au kuongeza ushindani ndani ya timu utakaoleta tija! Hata kama Simba inataka kuwa na kikosi kipana si kwa stahili hii.
Lakini unaongeza ushindani katika maeneo ambayo yapo vizuri `strong` au maeneo ambayo hayana ushindani kama angalau ya washambuliaji na mabeki?
Siamini kabisa kama Simba inamhitaji Dilunga kuingia kuongeza nguvu zaidi ya walivyofanya kina Niyonzima, Kichuya na Ndemla.
Unamuhitaji Kakule tena toka nje ya nchi huku unao Mkude, Kotei, Nyoni na Asante Kwasi wanaoweza kucheza eneo la chini kwa ufasaha mkubwa.
Sidhani, nina imani Simba inatakiwa kuwa na utulivu kwenye usajili wake. Kwa jicho langu tangu wanamaliza ligi ya msimu uliopita, nilitegemea waongeze wachezaji wachache kwenye nafasi sahihi za kuiletea timu ufanisi bila hiyo tamaa ya kusajili kila wanayemfikiria, itawaletea tabu huko baadaye.