Prime
Simba ikiamua itajibeba hivi...
KWA wale wapenzi wa somo la hesabu bila ya shaka bado wanakumbuka zile hesabu za Magazijuto. Hii ni kati ya topiki tamu za somo la hesabu ambazo mwanafunzi mjanja akizingatia na kuelewa kanuni hiyo ya Magazijuto, ni lazima atoboe kiulaini darasani.
Inawezekana neno Magazijuto kwa watoto wa 2000 ikawasumbua, ila hii ni kanuni ambayo kwa wenzetu Wapogoro wameipa jina la 'BODMAS Rule' na wengine wameikuza na kuita PEMDAS.
Bodmas ni kifupi cha maneno ya Bracket, Order, Division, Multiplication, Addition and Subtraction ambayo waswahili wakaamua kuirahisisha ili hata Wandengereko nao waelewe ndio wakaipa jina la MAGAZIJUTO.
Neno hilo la Magazijuto ni kifupi cha maneno; Mabano (Bracket), Gawanya (Division), Zidisha (Multiplication), Jumlisha (Addition) na Toa (Subtraction), ikiwa moja ya topiki ya hesabu zilizokuwa zikiwavutia wanafunzi darasani.
Hesabu zake ni rahisi kama utazingatia kanuni hiyo ya Magazijuto ambapo kwa mfano ukipewa swali kama hili la (40-3x6+4), ni lazima kwanza utoe mabano kisha kucheki kama kuna ishu ya kugawanya, kama haipo utahamia katika kuzidisha, kisha yanayofuata na mwishowe utapata jibu.
Kanuni hii haina njia ya mkato katika kupata jibu la swali lako na kuna wakati hata namba ziwe nyingi kiasi gani zikijumuisha alama hizo za namba, bado wajibu ni kwenda na kanuni ya kushughulikia mabao, kugawanya, kuzidisha kujumlisha na kisha kutoa, vinginevyo utafeli.
Hivi ndivyo ambavyo Simba inaweza kutumia kanuni hii kama kweli inataka kufikia nchi ya ahadi.
Huu ni msimu wa tano Simba inaendelea kujitafuta katika soka la Tanzania ikisaka ubingwa katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), kwani misimu minne mfululizo imetoka kapa mbele ya watani wao, Yanga iliyotawala na kuwanyima raha mashabiki na wapenzi wa Msimbazi.
KWANINI?
Kuna dhana kwamba Simba inayumba kwa sababu ya kukosa viongozi vijana wabunifu wenye mawazo mapya yanayoweza kuipeleka timu mbele.
Wanaoiegemea dhana hiyo wanarejea namna Yanga inavyoendeshwa na sura mpya za vijana kuanzia Rais Injinia Hersi Said, Makamu wa Rais, Arafat Haji hadi Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na hata wanaosimamia Sekretarieti ya klabu hiyo.
Wanaoiona Simba inaongozwa na viongozi wazee hususani wale wale waliokuwapo miaka nenda rudi na hata wale wapya waliochaguliwa au kuteuliwa kuwapiga tafu viongozi wa juu bado wachache wao wenye kuamini katika soka la kisasa. Hata hivyo, kiuhalisi hili halina ukweli.
Pia wapo wanaoamini Simba inayumbishwa kutokana na badilibadili ya makocha isiyoisha ndani ya vipindi vifupi na kuchanganya wachezaji washike lipi, kwani kabla hawajazoea falsafa za kocha aliyepo wanajikuta wakiletewa mwingine na kuanza upya wakati huo wapinzani vita inaendelea.
Wanatolea mfano ndani ya msimu huu pekee Simba imefundishwa na makocha watano tofautu akianza Fadlu Davids aliyekuwapo tangu msimu uliopita, kisha timu ikaachwa kwa Seleman Matola na Hemed Suleiman 'Morocco', baadaye akaletwa Dimitar Pantev kabla ya ujio wa Steve Barker.
Lakini kuna wanaoamini Simba inaangushwa na wachezaji ambao wamekuwa wakiingia na kutoka kila msimu ndani ya misimu mitano sasa, huku wengi wa wanaosajiliwa wakionekana kuwa na viwango duni kulinganisha na mahitaji ya klabu hiyo kongwe nchini.
Baadhi ya wadau wanaoamini katika hilo wanadai usajili umekuwa ukifanywa kama dili na wanaousimamia kwa mtindo wa '10 parcent' kwa kuleta watu wao bila kujali hitaji la benchi la ufundi na mahitaji ya timu na mwishowe wanatemwa ndani ya kipindi kifupi na kuletwa wengine.
Pia ipo dhana kwamba wachezaji wanaosajiliwa hawajui ukubwa na uzito wa jezi ya Simba, hivyo kushindwa kujitoa kwa ufanisi kama inavyotarajiwa, lakini lawama zote zikienda kwa wanaofanya usajili huo kwamba hawazingatii vigezo na masharti ila kuangalia matumbo yao.
UHALISIA ULIVYO
Kwa wanaokumbuka misimu minne nyuma kabla ya Yanga kuteka soka la Tanzania, Simba ndio iliyokuwa Wafalme wa soka na walikimbiza ndani na nje ya nchi kiasi cha kupewa sifa lukuki.
Katika misimu hiyo minne mfululizo, Simba ilibeba kila taji lililokuwa likishindaniwa hapa nchini kwa maana ya Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA) na Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa Yanga sasa, pia ikitamba katika soka la kimataifa ikicheza mechi za robo fainali mfululizo.
Lakini kinachosahauliwa na wengi ni kwamba kabla ya Simba kuwa mfalme wa soka Tanzania, timu hiyo ilisota karibu misimu mitano mfululizo ikiwa wanyonge mbele ya Yanga na Azam FC zilizokuwa zikipokezana nafasi mbili za Ligi Kuu Bara.
Ndio, mara baada ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2011-2012 kwa kishindo kwa kuifumua Yanga kwa mabao 5-0, haikutwaa tena taji hilo wala kushiriki michuano ya kimataifa kwa misimu karibu sita mfululizo, kwani 2012-2013 Yanga iliinyang'anya taji kabla ya Azam kubeba 2013-2014, kisha Yanga kurejesha taji hilo na kulishikilia kwa misimu mitatu mfululizo hadi 2016-2017.
Kipindi hicho Simba ilikuwa ikitegemea zaidi wachezaji iliowazalisha wenyewe kupitia timu ya Vijana ya U20 sambamba na nyota wa kigeni wa bei rahisi na waliozeeka huko watokako na ikavurugwa na jeuri ya fedha za Yusuf Manji kwa Yanga na utajiri wa siku zote wa Azam FC.
Hata hivyo, Simba ilikaa chini na kufanya mageuzi msimu wa 2017-2018 kwa kusajili mashine za maana akiwamo Emmanuel Okwi aliyerejea kutoka Denmark, Meddie Kagere 'MK 14' na kuwabeba nyota walioifanya Azam FC itishe kama Aishi Manula, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na John Bocco na matunda yalionekana kwa timu hiyo kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huo.
Sio kubeba ubingwa tu, lakini kikosi hicho kilipita katika mikono na makocha wa maana na wenye majina makubwa sambamba na kufanya usajili wa kishindo uliotokana zaidi na 'kufulia' kwa watani wao, Yanga iliyokuwa ikipitia kipindi kigumu baada ya Manji kuwekewa mizengwe na kukumbana na changamoto za kisiasa.
Kipindi hicho, Yanga ilifikia hatua ya kuwa ombaomba kwa staili ya aina yake ya kutembeza bakuli walilolibatiza jina la 'Kubwa Kuliko'.
Muasisi wa bakuli hilo unaweza kumtaja ni kocha Mwinyi Zahera aliyekuwa akiisaidia timu kwa fedha zake mwenyewe za mfukoni na kushirikisha mashabiki na wapenzi kuichangia kabla ya uongozi wa Dk Mshindo Msolla na wenzake kuandaa hafla ya 'Kubwa Kuliko' iliyomuibua GSM na Injinia Hersi.
Hafla hiyo ilileta mapinduzi makubwa kwa Yanga, kwani wababe hao walirudi katika mstari wakati huo Simba mambo yakienda harijojo na kwa misimu mitano mfululizo inaendelea kujitafuta bila kujipata na mwishowe sasa kufikia hatua mashabiki kuwashambulia viongozi hadharani.
KITU CHA KUFANYA
Hakuna siri kwamba, kinachoiponza Simba ni kama kile kilichoiponza Yanga misimu minne mfululizo nyuma, kujilinganisha na wapinzani wao. Yanga ilikuwa ikipima mafanikio kwa kutaka kujilinganisha na Simba na kujikuta ikipotea mazima 'porini' kabla ya kuzinduka.
Hata sasa, Wanasimba wamekuwa wakiumia kwa kuiangalia Yanga na mafanikio yao ya ndani na kimataifa kwa kuilinganisha na timu yao, bila kujua Yanga imefanya uwekezaji mkubwa hadi kufika hapo na hata aina ya kikosi kilichopo Jangwani huwezi kulinganisha na kile cha Msimbazi.
Kama Yanga ilivyokaa chini na kuangalia wapi ilipojikwaa kwa kuburuzwa na Simba kwa msimu minne mfululizo kisha kurudi na nguvu mpya ikisajili wachezaji wa kariba ya timu kubwa yenye malengo makubwa, ndivyo Simba inavyopaswa kufanya sasa.
Na hapo ndipo kanuni ya Magazijuto inapopaswa kutumiwa na viongozi waliopo sasa badala ya kuendelea kujidanganya kwamba kwa mwenendo walionao sasa wanaweza kuikuta Yanga ambayo imeshanogewa na mafanikio na haitaki kurudi kule ilipokuwa ikitegemea kikosi cha kina Ditram Nchimbi, Yassin Mustafa, Michael Sarpong, Yikpe na Klaus Kindoki.
Huwezi kuwa na wachezaji kama Djigui Diara, Pacome Zouzoua au Allan Okello na Aurelio Laurindo 'Depu', kama hutii hela. Huwezi kuwa na timu ya kutaka kuwania ubingwa wa Afrika kama una wachezaji wanaoshinda mitandaoni kucheza bongofleva, huku uwanjani wakiwa hawana njaa ya mafanikio wala kujituma kwa jasho na damu kuipigania timu yao. Tia hela.
Bahati nzuri ni kama vile, Simba imejishtukia na kurudi katika kanuni ya magazijuto, japo kwa kuchelewa baada ya kuleta mashine za maana kama kipa Gibrilla Kassalli, Libasse Gueye, Clatous Chama, Ismael Toure, Anicet Oura na Inno Jopsin Loemba walioanza kuonyesha njaa waliyonayo.
Wasimamie hapo hapo na kumpa muda kocha Steve Barker kufanya kazi yake kwa ufanisi ili kuona msimu huu wanatoboa vipi baada ya awali kuchemsha katika Ngao ya Jamii ilipopasuka mbele ya Yanga kikiwa ni kipigo cha sita mfululizo cha Kariakoo Derby.
Barker akiachwa kufanya kazi na kutimiziwa mahitaji yake ya wachezaji wenye uwezo, Simba ina nafasi kubwa ya kurejesha makali yake na hizi kelele kwamba sijui Murtaza Mangungu ndiye tatizo, mara sijui Simba ina viongozi wale wale kwa miaka mingi hivyo hawana maajabu, zitaisha.
Hata Yanga, kwa misimu miwili mfululizo imenolewa na makocha lukuki, ilianza na Miguel Gamondi, kisha Sead Ramovic kabla ya Miloud Hamdi na baadaye kumleta Romain Folz aliyekaa muda mchache kabla ya kuja Pedro Goncalves, lakini wote wamebebwa na wachezaji wenye uwezo.
Wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu na kuzoeana kiasi kwamba kocha mpya hapati kazi kumwaga falsafa na mbinu zake kwao na kumbeba kama ilivyotokea kwa makocha waliopita tangu Nasreddine Nabi hadi Pedro, licha ya kuchemsha kwenye sajili zao kadhaa ikiwamo dirisha lililopita.
Hayo yakifanyika na wanasimba wakawa na umoja na mshikamano kama kauli mbinu ya klabu hiyo isemayo Nguvu Moja, ni wazi Simba itarejesha makali yake na kufukuzana na wapinzani wao wengine katika Ligi Kuu Bara na michuano mingine, ila ikitaka njia ya mkato ijue itachemsha tu!