Prime
Mpanzu wa jana, leo na kesho
KUNA nyakati ngumu anazopitia kiungo mshambuliaji wa Simba, Ellie Mpanzu ndani ya kikosi hicho. Hakuna shabiki wala kiongozi wa klabu hiyo anayekubaliana na kiwango cha sasa cha staa huyo, ambaye alikuwa mtu hatari ndani ya kikosi cha wekundu hao msimu uliopita.
Simba wanapata wasiwasi mkubwa juu ya kiungo huyo kutokana na kiwango chake, na hatua hiyo imeibua tuhuma mbalimbali ambazo kama hazitatatuliwa haraka, haitashitua kuona anapotea kabisa ndani ya wekundu kwa namna mambo yanavyokwenda.
Miezi sita ya kwanza Mpanzu ndani ya Simba alipoanza kazi dirisha dogo la usajili msimu uliopita 2024-2025, alikuwa hatari mbele ya uso wa lango la mpinzani, ilikuwa rahisi kuona anafunga kuliko sasa ambapo ni rahisi kuona anapoteza nafasi, lakini pia amekuwa akionekana anakabika kwa wepesi huku hata mbinu zake zikitabirika.
Kutabirika kunamfanya ajikute akikosolewa kwa kupoteza mipira kirahisi.
Kumbuka nyota huyo alitua Simba Oktoba 2024 akisaini mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika mwisho wa msimu huu. Licha ya kutua kipindi hicho, lakini alianza kucheza lilipofunguliwa dirisha dogo la usajili kwani alifika wakati dirisha kubwa likiwa limefungwa.
Swali ambalo mashabiki wengi wanajiuliza ni kipi kimemkumba staa huyu wa zamani wa AS Vita Club ya DR Congo?
MABADILIKO YA MAKOCHA
Kitu cha kwanza ambacho mashabiki wa Simba na hata viongozi wa klabu hiyo wanatakiwa kufahamu ni kwamba klabu yao imepitia mabadiliko makubwa ya falsafa za makocha watatu tofauti wakiwa na Mpanzu.
Mpanzu aling’ara akiwa na Fadlu Davids ambaye ukweli ni kwamba alikuwa na kikosi cha kawaida, lakini ubora wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini ndio uliwabeba wachezaji wengi, si Mkongomani huyo peke yake.
Fadlu aliletwa Simba na benchi lake na alikuwa na hesabu nzuri za kuwapa ubora wachezaji wengi, ndio maana alifanya makubwa. Bahati mbaya sana aliondoka klabuni hapo kwa kushtukiza tena msimu ukiwa umeanza, hatua hiyo haiwezi kuwa iliwashangaza mashabiki na viongozi pekee, inaweza kuwa ni mtikisiko hata kwa wachezaji.
Baada ya Fadlu kutimka, akatua Dimitar Pantev ambaye hakumaliza hata miezi miwili akaondoka, wakati ambao wachezaji walikuwa wanajaribu kutafuta kumwelewa, akatimka, baada ya hapo sasa amekuja Steve Barker.
Unaweza kumuangalia Mpanzu pekee, lakini uhalisia ni kwamba ukitulia utaona si Mkongomani huyo tu, wachezaji wengi ambao walikuwa bora wamepoteza ubora wao uliokuwepo awali na kuonekana wachezaji wa kawaida zaidi. Hii ni kutokana na kupitia mabadiliko ya haraka ya falsafa tofauti kutokana na mabadiliko ya makocha, na hili ni muhimu kuzingatiwa kwani limewaathiri.
MAANDALIZI YA MSIMU
Mpanzu alichelewa kujiunga na kambi ya Simba ya kujiandaa na msimu huu, na hili lina sababu nyingi zikiwemo kutomalizana sawasawa na mabosi wa Simba juu ya fedha zake. Haya ni makubaliano ya kimkataba na itakumbukwa winga huyo zilizuka taarifa kwamba anawindwa na Yanga.
Kukosa maandalizi haya ni lazima yangemuathiri, kwa kuwa timu yenye ukamilifu ndani ya msimu inaanzia hapo, ambako yeye alikosa hatua hiyo muhimu.
Hakuna anayejua umuhimu wa maslahi yake binafsi zaidi ya muhusika. Mpanzu alisimamia maslahi yake, lakini kukosa uwajibikaji kwa wahusika ndio sababu ya mchezaji huyu kutokwenda kwa wakati kutokana na kutotimizwa kwa makubaliano.
Ikumbukwe baada ya Mpanzu kujiunga na Simba kule Misri kisha kurejea hapa nchini, nyota huyo aligundua kuna kitu kwake hakipo sawa, akamfuata kocha Mohamed Mrishona maarufu Kocha Xavi, yule fundi wa mazoezi binafsi, na kuamua kujiongezea dozi ili awe daraja sawa na wenzake.
TAARIFA ZA YANGA
Ndani ya maisha hayo ya kujitafuta kwa Mpanzu, zinavuma taarifa nyingi kutoka nje kwamba staa huyo anatakiwa na wapinzani wa Simba ambao ni Yanga. Hapa simu zilikuwa nyingi kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo kwenda kwa viongozi wao na wao kumrukia mchezaji husika, mwisho wanakuta hakuna kitu.
Hata hivyo, bado shaka ipo kwa mashabiki kwamba huyu mchezaji anaweza kuwa anataka kuwakimbia kweli. Hili lazima limechangia kutetereka kwa winga huyo ambaye alihitaji watu wa saikolojia kumweka sawa na kuachana na taarifa za nje.
TUHUMA NDANI YA SIMBA
Hajakaa sawa zikavuma taarifa nyingine mbaya tena kutoka ndani ya klabu kwamba winga huyo anatumika vibaya kuififisha Simba, tena kutoka kwa wakubwa ndani ya klabu hiyo.
Bosi mmoja anayetuhumiwa, aliwahi kumwonyesha mwandishi vitu ambavyo vilishtua kwamba mara ya mwisho anawasiliana na winga huyo alikuwa anamlaumu kwanini hajacheza vizuri.
Unajiuliza hizi taarifa za kutumika zinatoka wapi, lakini ukitulia unakumbuka kwamba ni kasumba ya soka letu kwamba mchezaji anaweza kutuhumiwa kwa mambo ambayo hayana ukweli, na kama ukweli usipozingatiwa ni rahisi kumpoteza mchezaji yeyote.
PRESHA YA MASHABIKI
Wakati Mpanzu akiyapitia haya, anakutana na presha ya mashabiki wake ambao wanaona staa ambaye wanamtegemea hafanyi vizuri, wakati ambao timu yao kiujumla haifanyi vizuri. Anajikuta kila kitu anakifanya kwa presha kubwa na kumpotezea utulivu wa kufanya mambo kwa usahihi na ubunifu mkubwa.
MABADILIKO YA KIKOSI
Tukumbuke wakati Mpanzu anatamba msimu uliopita alikuwa anacheza na watu bora zaidi. Akiwa winga wa kushoto, nyuma yake kulikuwa na mkongwe beki na aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, walikuwa wakielewana vizuri.
Pale katikati Mpanzu alikuwa anapata huduma nzuri kutoka kwa mkongwe, Fabrice Ngoma, pembeni yake kuna Yusuf Kagoma ambaye alikuwa anazima hesabu zote za wapinzani. Usisahau kulikuwa na kiungo wa kimbinu, Jean Charles Ahoua.
Uwepo wa mastaa hawa ulimpa wepesi Mpanzu na kujikuta anafanya mambo kwa utulivu. Msimu huu mambo yalianza kwa utofauti mkubwa, Tshabalala ameondoka na Ngoma, Ahoua yakamgeukia na kuwa wa benchi mpaka akatimka. Anajikuta anaanza maisha mapya na watu wapya kama Antony Mligo na Naby Keita ambao inahitaji muda kuzoeana kiuchezaji.
UJIO WA OURA
Kuna hesabu za ndani sana kwamba ujio wa kiungo Anicet Oura ni kama Simba imeanza kujiandaa na maisha bila Mpanzu, kwamba wakubwa hawaridhishwi na kiwango chake wakiamua kulikimbia tatizo kwa kushindwa kukaa na kutafuta suluhisho la kupata utulivu wa winga huyo na bdala yake kumtafutia mtu mwingine.
Inawezekana ikawa ni njia rahisi ili washindanie nafasi, lakini haitakiwi kumuangamiza Mpanzu, badala yake Oura amuimarishe kiushindani Mkongomani huyo na Simba inufaike bila kumuangamiza mwingine, kwa kuwa kuna mengi amepitia staa huyo.
TAZAMA HAPA
Takwimu zinaonyesha msimu huu Mpanzu katika mechi nane za Ligi ya Mabingwa Afrika alizocheza kwa dakika 646, amefunga bao moja dhidi ya Gaborone United wakati Simba ikishinda 1-0 ugenini hatua ya awali. Hana asisti.
Katika mechi hizo nane, saba alimaliza dakika zote tisini, huku moja dhidi ya Esperance iliyomalizika kwa sare ya 2-2, aliingia akitokea benchini kuchukua nafasi ya Libasse Gueye na kucheza kwa dakika 16 tu.
Msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho Afrika, Mpanzu alicheza mechi tisa kuanzia hatua ya makundi akiziwahi zile tatu za mwisho.
Katika mechi tisa, alihusika kwenye mabao matatu, akifunga moja na asisti mbili ikiwamo ile ya fainali dhidi ya RS Berkane iliyomalizika kwa sare ya 1-1 ambapo Joshua Mutale ndiye aliifungia Simba, hata hivyo, wekundu hao wa Msimbazi walipoteza kwa jumla ya mabao 3-1 kufuatia ugenini kufungwa 2-0.
Msimu huu katika Ligi Kuu Bara, amefunga bao moja na asisti tatu wakati Simba ikicheza mechi saba na kupachika mabao 14.
Kwa msimu uliopita, Mpanzu alipoanza kazi dirisha dogo, alimaliza na mchango wa mabao kumi katika ligi, akifunga manne huku akitoa asisti sita.
NINI KIFANYIKE
Simba inatakiwa kutuliza presha kwa Mpanzu, ikiwezekana ichukue mikanda yake ya nyuma, kisha kocha Barker aanze kwa kukaa na Mkongomani huyo wazungumze na kuamua safari mpya, kwani bado Mpanzu anaweza kuwa na siku nyingine bora mbele yake kama ilivyokuwa huko nyuma.