Siamini kama Adel Amrouche amewaacha Tshabalala, Kapombe

KATIKA mitandao kuna video inasambaa ikiwaonyesha mabeki wawili wa Simba, Mohamed ‘Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe wakimsikiliza kwa makini kocha mpya wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, Adel Amrouche.

Hakuna aliyeweza kunasa mazungumzo hayo. Inawezekana akawa anawaambia jinsi ya kuboresha kiwango chao baada ya kuwaona wakiliongoza jahazi la Simba kuisambaratisha Horoya AC ya Guinea kwa mabao 7-0 juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Inawezekana pia alikuwa akiwaambia jinsi wawili hao walivyo kwenye mipango yake na timu ya taifa ambayo Machi 24 itavaana na Uganda The Cranes kwenye mechi ya kusaka tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), 2023 zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Lakini wawili hao na nyota wengine wazoefu hawamo kwenye kikosi kilichoondoka alfajiri ya jana kwenda Cairo kwa ajili ya mchezo huo muhimu wa Afcon utakaopigwa nchini Misri badala ya Kampala, Uganda kisha kurudiana tena wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

Haijaelezwa sababu za wahusika kuwaacha nyota hao wawili ambao wamekuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kwa muda mrefu. Pengine ni kwa sababu timu yao ilikuwa na mechi hiyo dhidi ya Horoya, lakini kuna muda mrefu wa kupumzika kabla ya mechi hiyo.

Binafsi sitaki kuamini Amrouche ndiye aliyeamua kuwaacha wawili hao kwa sababu zozote zile kwa kuwa hajapata muda mrefu wa kuwaangalia na kama aliwaona haikuwa kwa ajili ya kujua atawatumiaje, ukiachana na mechi ya Jumamosi.

Ni lazima uamuzi wa kuwaacha nyota hao umefanywa na kikundi kingine kilicho karibu na timu hiyo, chenye hoja za kipekee kuhusu kiwango cha wawili hao na wengine.

Katika hali ya kawaida, kocha mpya ambaye hakuwa na uhakika wa kuja nchini kufundisha Stars hadi alipotangazwa rasmi, angeanza na sehemu kubw aya wachezaji waliokuwa wanaunda kikosi cha sasa, akijumuisha wachache wapya aliowaona kwa siku chache alizoanza kufuatilia mpira wetu kwa makini zaidi.

Kadri muda ambavyo ungekwenda ndivyo ambavyo angeendelea kubaki na aliowakuta au kuingiza wachezaji wapya kulingana na mahitaji ya mfumo wake na uwajibikaji wa wachezaji.

Lakini hilo la kuwaacha ghafla wachezaji ambao hawajawahi kusugua benchi tangu waanze kuchezea timu ya taifa, linashangaza wengi na ndio maana limekuwa mjadala mkubwa, hasa kwa wawili hao ingawa wako wengine wengi walioachwa.

Nimejaribu kufikiria lakini sijapata sababu ya maana ya kuwaacha Kapombe na Tshabalala. Nachoona ni kikundi cha watu kilichojenga hoja ambayo si rahisi kueleweka kwa wengi na kuingiza wachezaji wapya. Ndio, hao wapya wanaweza kufanya maajabu, lakini kwa nini tusubiri miujiza? Kama wasipofanya vizuri, mashindano hayatatupa nafasi ya kujisahihisha, bali kutumia nguvu kubwa zaidi kuweka mambo sawa wakati nafasi ya kuepuka hilo ilishakuwepo tukacheza kamari.

Hi si mara ya kwanza. Wakati Kim Poulsen alipoondolewa Taifa Stars, kuliibuka kitu kama hiki. Wale wachezaji waliokuwa wanazungumzwa kuwa wameshuka kiwango waliachwa mara moja na ilikuwa rahisi kusema kuwa Kocha Mzambia aliyepewa majukumu ya Stars kwa muda, ndiye aliyefanya uamuzi huo. Binafsi nikapinga.

Wakati mechi dhidi ya Uganda ikikaribia, mtangazaji mmoja wa kituo cha redio alinipigia simu kuniulizia kitendo cha kuchelewesha kumtangaza kocha mpya kina maana gani. Moja kwa moja nilimjibu kinamanisha kuna watu wanataka kwanza wateue wachezaji ambao wao wanaona wanafaa ili apewe huyo kocha atakayetangazwa.

Ilipita kama wiki mbili ndipo kocha mpya alipotangazwa na siku chache baadaye kikatangazwa kikosi ambacho hakiakisi sura na falsafa za Amrouche, kama kocha mtaalamu anayejua wajibu wake kwenye timu yoyote ya taifa ni kunganisha vipaji vilivyo tayari na si kufundisha wachezaji jinsi ya kucheza au kuwakuza.

Timu yoyote ya taifa huundwa na kikosi cha wachezaji waliokamilika na walio tayari kwa mechi za mashindano ya nyumbani na ugenini. Ndio maana hata kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuhusu kuruhusu wachezaji wa kimataifa zinatoa siku tatu au nne tu kwa wachezaji kutoka klabu zao. Kama mchezaji anatoka ndani ya bara husika, hupewa siku tatu na yule anayetoka bara jingine hupewa siku zaidi.


Kwa hiyo siku za maandalizi za timu za taifa huwa hazizidi tatu au nne kwa kuwa huundwa na wachezaji walio kamili na tayari kwa mechi. Hivyo, wajibu wa makocha ni kuhakikisha wanaita wachezaji walio kamili na tayari kwa mechi na si wale wa kwenda kuanza kuwajenga utimamu wa mwili na baadaye kuwafundisha mpira kwa kuwa mambo hayo huhitaji muda mrefu zaidi.

Katika hili, sidhani kama kuna kocha angewaacha Tshabalala na Kampombe, ambao klabu yao bado iko katika mashindano ya kimataifa na imefikia hatua za juu ambako wawili hao na wenzao wanazidi kuongeza uzoefu unaotakiwa kuwa hazina kwa taifa hili.

Na uzoefu wao ni muhimu kwa ajili ya mechi ya Uganda na nyingin e zinazofuata. Unaposikia wameachwa, unashikwa na butwaa. Kwa sababu zipi hasa? Kwamba wameshuka kiwango? Kwamba hawaingii kwenye mfumo wa Amrouche? Kwamba wakati umefika wawapishe wengine? Kwamba wamepoteza utimamu wa mwili? Kwamba nafasi zao zina ushindani mkubwa kiasi kwamba walikuwa ama wanacheza ama wanasugua benchi? Kwanini hasa?

Katika hali ya kawaida, makocha huzungumza na wachezaji ambao ni tegemeo na ambao hawatajumuishwa kwenye kikosi kinachocheza mechi inayofuata na kuwaambia sababu. Ndivyo inavyofanyika duniani kote. Hii ni tofauti na hali inavyokuwa kwa mchezaji ambaye amekuwa akiitwa na kuachwa kwa nyakati tofauti.

Na hii hujenga taswira nzuri kwa wengine kwamba “kumbe wanathaminiwa” na hivyo timu ya taifa kuheshimiwa si tu na wachezaji pekee, bali hata mashabiki ambao ni sehemu kubwa ya timu inapotafuta ushindi.

Wakati mwingine ni muhimu kutengeneza sera au utamaduni wa jinsi ya kushughulika na magwiji wetu kwenye timu ya taifa. Hata kama kocha mpya atakuja na mawazo tofauti, ni muhimu kuwe na mwongozo wa jinsi ya kuachana na wachezaji waliotoa huduma kwa taifa kwa kujituma na kwa kipindi kirefu.

Kocha atalazimika kufuata utamaduni huo badala ya kusubiri kila kocha aje na taratribu zake na kutuacha hatujui nini cha kufanya pale anapotimuliwa.

Yako mataifa ambayo mchezaji wake nyota anapoumia, huchukua jukumu la kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida kuanzia anapomaliza matibabu hadi anaporudi uwanjani.

Si lazima sera au utamaduni huu uwepo vitabuni, bali kuujenga ili kujenga heshima kwa timu ya taifa na kuwafanya makocha wajue kuwa taifa hili linaheshimu timu ya taifa na wachezaji wake na hivyo kufanya kazi kwa nidhamu iliyowekwa-- hapa simaanishi kuwa Amrouche ndiye aliyewaacha Tshabalala na Kapombe kwa kuwa hakuna utamaduni kama huo. Bado naamini kabisa kuwa Amrouche hakuhusika kuwaacha nyota hao.

Ninaamni kabisa kwamba Tshabalala na Kapombe watarejeshwa muda si mrefu kuendelea kulitumikia taifa lao. Lakini hapa ndipo pa kuanzia kujenga utamaduni wa uteuzi wa wachezaji wa timu za taifa na kuheshimu michango ya wachezaji waliotoa huduma yao kwa muda mrefu kwa kwa kujitoa kwa nguvu zote.

Utamaduni huo utaepusha makocha kujifanyia mambo kiholela eti kwa sababu wao ndio watalaamu na ndio wanaobeba lawama timu ikifungwa.

Tunahitaji kuwa na kitu chetu na hao tunaowaajiri, watumie utalaamu wao ndani ya misingi tuliyoijenga. Mbona Barcelona, Real Madrid au Bayern zimefanikiwa kujenga hadi utamaduni wa kusajili wachezaji hata kama kocha aliyepo hakumtaka nyota Fulani.

Tunahitaji kitu chetu!