Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Si viongozi Yanga, wa kulaumiwa ni TFF, TPLB

WAKUBWA Pict

Muktasari:

  • Na mashirika makubwa ni yale yanayotaka kupata soko kubwa zaidi kuzidi mipaka ya taifa yaliyopo na wakati mwingine yasijulikane hata yanatoka wapi.


Mpira wa miguu, kama michezo mingine mikubwa duniani umegeuka kuwa biashara kubwa inayozifanya klabu ziendeshwe kama mashirika makubwa (corporate organisations), kiasi kwamba yanahitaji kudhibitiwa kwa kanuni na sheria maalumu ili yasifanye kazi kuzidi mipaka yake.


Na mashirika makubwa ni yale yanayotaka kupata soko kubwa zaidi kuzidi mipaka ya taifa yaliyopo na wakati mwingine yasijulikane hata yanatoka wapi.

Taarifa zinasema kati ya mashirika makubwa yanayodhamini klabu za Ligi Kuu ya England, yenye ofisi angalau kilomita 10 kutoka makao ya klabu yanayoidhamini au hata ndani ya nchi ya Uingereza, ni machache.

Mengi yanatoka nje ya Uingereza kwa sababu yanajua jinsi klabu za nchi hiyo zilivyojijengea jina ulimwenguni na kuiwezesha Ligi Kuu England kuwa inayofuatiliwa na watu wengi duniani.

Kadiri klabu hizo zinavyozidi kupanua wigo wa mashabiki wake nje ya mipaka, ndivyo zinavyozidi kuvuta kampuni nyingi duniani kuwa washirika wake.

Nchini Hispania, Real Madrid na Barcelona zina wigo mkubwa kulinganisha na klabu nyingine za nchi hiyo ambayo klabu zake zinatamba barani Ulaya.

Wakati Florentino Perez anaelekea kuwania urais wa Real Madrid kwa mara ya kwanza, alitangaza wazi kuwa lengo lake siyo vigogo hao kutamba Hispania na barani Ulaya tu, bali kuwa chapa ya dunia.

Akaingia na sera ya Galacticos ambayo ililenga kukifanya kikosi cha Real Madrid kiundwe na wachezaji nyota duniani katika kila nafasi. Mchezaji ambaye alionekana anafuatiliwa sana barani Asia alinunuliwa kwa pesa aliyotaka. Vivyo hivyo wachezaji waliovutia Amerika Kusini, Afrika na Amerika Kaskazini walisajiliwa na kuiwezesha Real Madrid kuwa chapa ya dunia.

Ukiwaambia Real Madrid na Barcelona kwamba wanaweza kuchezea mechi yao ya Kombe la Mfalme au Ligi Kuu nchini Saudi Arabia au Marekani, hawatanyanyua hata sehemu ndogo ya mdomo wao kujaribu kukupinga. Kwao ni neema na fursa ya kufanikisha ndoto ya kuwa chapa za ulimwengu.

Hata jamaa walipoibuka na wazo la European Super League, wawili hao waliungana kushika bango kuwa hiyo ndiyo ligi sahihi, ingawa Shirikisho la Soka la Hispania, kama ilivyokuwa kwa mashirikisho mengine, halikubaliani na mpango huo kwa sababu ulionekana kuwa ungeua soka la ndani ya nchi za Ulaya.

Kwa hiyo, klabu za soka ni taasisi za kibiashara ambazo ziko tayari wakati wowote kutumia fursa ya masoko mapya popote watakapoona mlango umefunguliwa, ingawa kwetu huku sababu zinaweza kuwa si za kibiashara sana kama miamba hiyo ya soka duniani.

Wiki iliyoisha mjadala mkubwa ulikuwa kuhusu uamuzi wa Yanga kucheza mechi yao ya kwanza dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba kwenye Uwanja wa New Amaan Complex jijini Unguja, uamuzi ambao utaandika historia kwa vigogo hao kukutana mara ya kwanza nje ya Tanzania Bara katika mechi ya ligi.

Wengi wamewalaumu viongozi wa Yanga kwa uamuzi huo wakisema wameamua kutoheshimu mashabiki wao ambao wangesafiri kutoka kila kona ya nchi kuifuata timu yao jijini Dar es Salaam kama ingeamua kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga wameeleza kuwa waliomba kutumia uwanja huo unaochukua watu 60,000 waliokaa, lakini inaonekana utakuwa na shughuli nyingine siku hiyo. Lakini kikubwa, mabadiliko ya kanuni yaliyotangazwa mapema msimu huu, yanawapa mwanya huo wa kutumia Uwanja wa New Amaan wa Zanzibar, ambayo kwa mujibu wa katiba, mambo ya michezo yana wizara yake tofauti na hii ya kwetu inayoongozwa na Paul Makonda.

Ni kweli kwamba suala la mashabiki ni lazima liheshimiwe, hasa klabu inapokuwa nyumbani. Hata hivyo hakuna kanuni inayolazimisha klabu kutumia uwanja iliousajili mwanzoni mwa msimu kuwa utakuwa ndio makao yake. Ukweli kwamba kanuni zinaruhusu kuhamia uwanja mwingine, unafuta ulazima wa timu kutumia uwanja mmoja msimu mzima. Na si kanuni tu, huenda Yanga wameona fursa na manufaa ya kuchezea mechi yao visiwani Zanzibar, ambazo zinaweza kuwa za kibiashara kama ambavyo Real Madrid na Barcelona zinacheza mechi za mtoano nchini Marekani au Saudi Arabia, au masuala mengine ya kijamii.

Mlango ulishafunguliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linawajibika kupitisha kanuni za ligi baada ya kupokea mapendekezo kutoka Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Lakini duniani kote, mpango mkubwa ni kuwalinda mashabiki dhidi ya uamuzi unaoweza kulenga biashara zaidi kuliko utamaduni wa mpira.

European Super League ilikuwa na kasoro hiyo. Na kwa sababu klabu kubwa za barani humo ni mashirika makubwa ya kibiashara ziliona umuhimu wa kutumia fursa hizo, lakini serikali zikaona zikiruhusu hilo, mashabiki wa ndani watakosa burudani, michuano ya ndani itapoteza hamasa na mambo mengine.

Kwa Uingereza hilo lilichangia kuharakisha kuwasilishwa bungeni muswada wa kuanzisha ofisi ya msajili huru ambayo itahusika na mambo yote ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya mashabiki. Moja ya vipengele kwenye muswada huo ni kuzitaka klabu kuwasilisha ushahidi kuwa uamuzi wa kubadili rangi ya jezi za nyumbani ulikubaliwa na mashabi, na si wanachama. Yaani klabu itafute njia ya kuwezesha kushirikisha mashabiki kufikia uamuzi huo.

Ingawa kwa teknolojia ya sasa inawezekana, lakini ni kitu kigumu na kinaonyesha ni kwa kiasi gani sasa mashabiki watakuwa wakilindwa baada ya ofisi hiyo kuanzishwa rasmi. Na hivi ni vitu ambavyo TFF na TPLB wanatakiwa kuanza kufikiria kuvianzisha.

Haiwezekani KMC, timu ya Manispaa ya Kinondoni ihamishe mechi zake kutoka uwanja uliojengwa kwa jasho la wananchi wa wilaya hiyo kwenda mkoa mwingine. Na hata hili la Yanga, inawezekanaje ipuuze mashabiki wake wote wa Tanzania Bara ikapeleka mechi Zanzibar ambako wana ligi yao inayotoa bingwa anayeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika? Mamlaka za Zanzibar zilikubalije mpango kama huo? Hazioni kuwa huko ni kuua unazi kwa klabu za Zanzibar?

Kitendo cha mechi za Ligi Kuu Bara kuhamishwahamishwa kiholela ni cha kupuuza mashabiki kwamba hawana maandalizi yoyote kwa mwaka kuziona klabu wanazopenda. Ina maana kungekuwa na tiketi za msimu ingekuwaje? Yaani umeshanunua tiketi yako ukijua mechi itachezwa Mwanza na ukajipanga kifedha, halafu siku mbili kabla ukaambiwa itachezwa Mtwara?

Uendeshaji klabu kisasa unahitaji kuonekana katika mambo yanayoonekana madogo kama hayo, lakini makubwa kwa wadau wa mpira. Lakini kama nilivyosema awali, mamlaka zimefungua mlango, kwanini viongozi wa klabu wasiutumie kufanikisha malengo yao? Wa kulaumiwa si viongozi wa Yanga, bali mamlaka zilizofungua milango na kutojishughulisha kutengeneza kanuni zitakazolinda mashabiki dhidi ya uamuzi mbovu wa kibiashara wa viongozi wa klabu bila ya kuzingatia utamaduni na mazingira ya mpira wa miguu.