SAJENTI BACCA: ‘Ukakamavu’ askari hadi beki Stars, Yanga ijipange

Muktasari:
- Ilikuwa Novemba 19, 2024 na beki huyo wa kati alimficha mshambuliaji huyo hatari wa Guinea kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Taifa Stars ikijikatia tiketi ya kwenda Morocco kwenye fainali zijazo za mataifa ya Afrika.
KUTOKA kuwa Koplo hadi Sajenti. Huyu ndiye Ibrahim Hamad 'Bacca'. Beki mkakamavu wa Yanga, ambaye alimfanya mshambuliaji hatari wa Borussia Dortmund, Serhou Guirassy kushindwa kupiga hata shuti moja lililolenga lango la Taifa Stars.
Ilikuwa Novemba 19, 2024 na beki huyo wa kati alimficha mshambuliaji huyo hatari wa Guinea kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Taifa Stars ikijikatia tiketi ya kwenda Morocco kwenye fainali zijazo za mataifa ya Afrika.
Mbali na makubwa aliyoyafanya akiwa na Yanga ikiwemo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, matatu ya kombe la FA, Ngao ya Jamii mara tatu na kuifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2023, alichokifanya mwaka jana kwa Mkapa kilichochea Mkuu wa Jeshi la Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Komodoo Azana Hassan Msingiri kufanya maamuzi hayo.
Bacca amekuwa mmoja wa wachezaji kipenzi cha mashabiki wa Yanga na Mwanaspoti linakuletea vitu vinavyombeba na kumpa heshima katika kikosi hicho.

KIWANGO BORA
Bacca alianza kucheza soka la ushindani Jang'ombe Boys mwaka 2017–2019, kisha Malindi 2019–2021, ndipo akajiunga na KMKM 2021–2022 msimu ambao alishinda ubingwa wa Lig Kuu Zanzibar, kabla ya kutua Yanga dirisha dogo la usajili mwaka 2022.
Hakuibuka tu na kuwa mmoja wa mabeki bora wa kati, miaka minne iliyopita alianza kwa kuwa chaguo la pili nyuma ya Yannick Bangala aliyekuwa anaaminiwa zaidi akitumika kama beki ya kati na kiungo mkabaji sambamba na Dickson Job, hata hivyo upepo wa mambo ulibadilika na Bacca kuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi hicho na kwa wakati huo kilikuwa chini ya Nasreddine Nabi.
Msimu wake wa kwanza Yanga (2021/22), alicheza mechi tano kwa dakika 282, huku Bangala akiongoza kwa kucheza dakika nyingi eneo hilo (2074) katika mechi 24.
Msimu uliofuata 2022/23 pia hakuwa na namba kubwa, hii ni kutokana na uwepo wa Bangala aliyecheza michezo 20 kwa dakika 1526 na ukawa msimu wake wa mwisho, huku Bacca akicheza michezo 12 kwa dakika 851.
Bacca amekuwa akionyesha kiwango bora na nidhamu na ni ngumu kumkosa katika mazoezi ya klabu yake na timu za Taifa, labda kwa sababu maalumu. Pia ni mtu wa kujituma jambo linalowashawishi makocha na hivyo kuzidi kumweka katika ubora na hilo limemfanya kuwa muhimu kikosini na amekuwa akikosekana kwa nadra, labda kwa sababu ya kadi au majeraha.

AITEKA BEKI YANGA/STARS
Msimu wa 2023/24 ndiyo ulikuwa bora zaidi kwake na hilo lilithibitishwa pia na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo lilimtangaza kuwa beki bora wa msimu huo na alicheza mechi 22 kwa dakika 1762 na aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wake wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Licha ya kutokuwa na misimu bora miwili ya mwanzo, hakukata tamaa na alipambana kuhakikisha anakuwa bora katika kikosi hicho na timu ya Taifa, Taifa Stars. Pia hakuingiwa kiburi kutokana na mafanikio ya msimu huo, na msimu huu ameendeleza ubora wake, licha ya makosa madogo madogo.
Bacca amekuwa akiwakosha mashabiki na makocha waliopita Yanga akiwamo Miguel Gamondi, Saed Ramovic na sasa Miloud Hamdi na wote wamekuwa wakimwamini katika safu ya beki na amekuwa akiitendea haki.
Msimu huu hadi sasa, Yanga ikiwa imecheza michezo 22 ikiongoza ligi, Bacca amecheza mechi 19 kwa dakika 1533. Ameonyeshwa kadi moja nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Tabora United timu yake ikikubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani.

NIDHAMU NJE, NDANI
Pamoja na kucheza kwa kiwango bora, Bacca amekuwa muumini wa nidhamu ndani na nje ya Uwanja na katika kuthibitisha hilo, ni matukio yake awapo uwanjani na amekuwa akicheza kwa umakini sana.
Pia inaelezwa Bacca sio mtu wa matukio nje ya uwanja na licha ya kufanya starehe zake lakini siyo kwa kiwango cha kushusha heshima yake na kuharibu kipaji chake kama meneja wa timu hiyo anavyoeleza;
“Bacca sio mtu wa mchezo awapo uwanjani. Nje ya uwanja ni miyeyusho sana, ni mtu wa maneno mengi utekelezaji mdogo sana kama ilivyo kwa Mwamnyeto. Ni mtu mwenye nidhamu ya hali ya juu kwenye kazi yake.”
Bacca pia sio mzungumzaji sana ni mtu wa vitendo na mara zote anaamini katika kumuomba Mungu ili mambo yake yaweze kwenda kama anavyotaka.
Amekuwa akiongea maneno machache sana hata anapohojiwa na vyombo vya habari ikiwamo kuongelea mchezo ujao au kutoa dukuduku kutokana na kile kinachozungumzwa kuhusu timu yake.

ANAIBEBA YANGA, STARS
Ubora wake unabebwa na uwezo wa kutengeneza mashambulizi, kukaba na ni mwepesi wa kupanda na kushuka na si mwoga katika kufanya maamuzi akicheza sambamba na nahodha wake msaidizi Dickson Job.
Hii ndiyo sababu hadi sasa msimu huu amefunga mabao manne kwani inapotokea nafasi ya kushambulia hupanda na kutengeneza nafasi au kufunga.
Pia Bacca ni beki wa kati mwenye nguvu na uwezo wa kusoma mchezo vizuri, ana sifa ya kuwa na uwezo wa kuzuia mashambulizi ya wapinzani kwa umakini, kushinda mipira ya juu na kutoa msaada kwa mabeki wenzake.
Stars imekuwa ikiwatumia mabeki wawili kutoka Yanga, sio tu kwa sababu wanacheza pamoja muda mrefu, bali ni kutokana na ubora wao huku nyota kutoka Simba Abdurazack Hamza akisubiri benchi.

YANGA IJIPANGE
Aliyewahi kuwa kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche alimtaja Bacca ni beki bora Afrika kwa sasa kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha na anamwona mbali zaidi.
"Ubora wa Bacca alionao sasa na nidhamu yake ya mchezo anazidi kuwa mchezaji mkubwa na mimi namwona mbali sana, kwa sasa ukiniambia nikutajie beki bora Afrika jina la kwanza ni Bacca ni beki mzuri," anasema Amrouche.
Hii dhihirisho la ubora wa Bacca na Yanga ina kazi kubwa ya kuhakikisha inamtunza kwani kiwango chake kimekuwa kikipanda kila msimu na itawalazimu kutuliza akili na kuandaa fungu la maana ingawa tayari ana mkataba wa muda mrefu na klabu yake hiyo hadi 2027, ingawa bado kuna haja ya kufanya naye mazungumzo zaidi ili kumlinda kwani ni beki wa viwango kutokana na umbile lake na makubwa anayoendelea kuyafanya.
Tayari kuna ofa kutoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo ambaye kwa sasa anainoa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Nasreddine Nabi na alionyesha nia ya kumuhitaji beki huyo lakini Yanga haikutaka kufanya biashara hiyo kutokana na kutokuwa na mtu sahihi wa kuvaa viatu vyake.
MIAKA MITATU, MATAJI MATATU
Hadi sasa beki huyo ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na mawili ya Kombe la FA akiwa na Yanga, huku akiwemo kwenye kikosi kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kuondoka na medali.
REKODI ZAKE
2021/22
Mechi 5 dakika 282
2022/23
Mechi 12 dakika 851
2023/24
Mechi 22 dakika 1762
2024/25
Mechi 19 dakika 1533 amefunga mabao manne.