SAGALA: Uvivu chanzo cha kufulia kwa wazawa

KATIKA toleo la jana tulianza makala ya nyota wa zamani wa CDA na Simba, Eric Sagala akielezea safari yake ya soka na maisha kwa ujumla enzi akicheza na hata sasa akiwa amestaafu soka.

Tuliona namna jinsi alivyosajiliwa Simba na pia jinsi anavyopoteza simu za mkononil kiasi safari za kwenda polisi kuripoti kila mara...Leo mkali huyo wa zamani anamalizia mahojiano yake na Mwanaspoti na kufunga mambo kibao. Ebu endelea naye...!

MFUMO WA WACHEZAJI

Mfumo wa maisha kwa wachezaji wa soka la Tanzania, unaweza kubadilika kama wao watakuwa na dira ya maisha na kutaka waendelee na kufika mbali kama wafanyavyo wachezaji wengine.

Asilimia kubwa ya wachezaji nchini hasa wanaotoka timu kubwa zikiwemo Simba na Yanga, wamekuwa wakisajiliwa kwa pesa nyingi na hivyo kama wakiweka malengo na kuachana na mambo ya starehe pengine wangeweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo na kuwa na matamanio ya kufika mbali kisoka .

Sagala ambaye aliwahi kucheza timu ya Simba miaka ya nyuma anashangazwa kuona wenzao wanacheza soka na kuvuna pesa nyingi lakini baadhi yao wanakosa mwelekeo.

Anasema kipindi cha nyuma walicheza mpira kwa ajili ya sifa , kujulikana na zaidi ilikuwa ni mapenzi ya timu tofauti na sasa ambapo kabla ya kuanza kucheza lazima mchezaji asajiliwe kwa makubaliano ya fedha .

Nguli huyu wa soka na Tanzania na nje anasema kama siku zingerudi nyuma katika nyakati zao, huenda kusingekuwa na mahangaiko ambayo wanayapata nguli wa soka wengi hivi sasa.

Anasema kama vijana wangekuwa wanajiwekea malengo yao, huenda kila mmoja angekuwa anastaafu soka akiwa na nyumba siyo chini ya tano au zaidi.

“Wachezaji wa siku hizi wanapewa udhamini mkubwa na timu zao kuanzia jezi, afya na fedha tofauti na sisi tulivyokuwa tunacheza enzi zetu hata jezi ikichanika hakuna anayekununulia nyingine kwa hiyo wanapaswa kuitumia nafasi hii vyema,” anasema Sagala.

WACHEZAJI WAZAWA

Sagala anataka mambo mengi yanayofanya soka la Tanzania lisiendelee akifananisha na mataifa mengine lakini kikubwa analia na wachezaji wazawa akisema hawawezi kuendelea katika kusakata gozi la ng’ombe kama wataendelea na alichokiita ‘uvivu’ wa mazoezi.

“Hivi wachezaji wenye maumbo mazuri kama (anamtaja jina) hawaitwi kwenye timu ya Taifa unafikiri inatokana na nini, ni uvivu wa mazoezi tu jamani, huyu nimemtaja mmoja lakini wako wengi hata wanashindwa kudumu katika kikosi cha kwanza,” anasema.

Anasema katika muda aliodumu kwenye soka kunavitu vingi ameviona ambavyo kama vingerekebishwa, hadi sasa Tanzania ingekuwa wachezaji wengi nje ya nchi akitaja wachache walioko huko kwamba juhudi zao binafsi ziliwafikisha katika soka la kulipwa.

Kuhusu timu za Tanzania anaona bado zinafanya udanganyifu ili zisipoteze mchezo jambo ambalo wanazidi kujilemaza na kushuka ubora wao pale wanapokutana na timu za nje zilizojiandaa vema.

Kwa mujibu wa Sagala, makocha wa timu kubwa wamekuwa wakifanya udanganyifu pale wanapokutana na timu ndogo waonekane kuwa na uwezo mkubwa wa kutokupoteza mchezo lakini wakicheza na timu za nje wanapwaya kwani wanakutana na watu ambao wanapesa zao, hawadanganyiki na wanalifahamu soka.

“Mfano mzuri ni kipindi tunacheza na timu Sigara, kocha wa Simba alivyoona tunaweza kupoteza mchezo aliamua kuongea vizuri na timu pinzani ili kuzuia kushuka daraja na ni zaidi ya mara tano kwa msimu ule Simba ilinusurika kushuka kama isingekuwa ujanja basi tungeshuka,” anasema Sagala.

Kwa mujibu wa mkongwe huyo, timu nyingi zinashindwa kuingia kiwango cha kimataifa kutokana na kutaka kuonekana wao ni bora zaidi kitaifa na si kimataifa hivyo wanazuia uwezo wa timu ndogo kwa ushawishi .

Sagala anasema timu nyingi na viongozi wao hawashauriki na ndio maana wanaacha wachezaji wazuri na kusajili wachezaji wenye kiwango cha chini kwa maslahi yao na alichokiita 10 percent.

“Tumejionea katika mchezo tuliocheza na Uganda na kutupiga magoli manne tena mbele ya Waziri Mkuu, sasa hii ni aibu inabidi tubadilike,” anasema.

Anashauri kuwepo na mabadiliko na wachezaji wa ndani wajitume na kuongeza juhudi zaidi ili waweze kuonyesha uwezo wao na kuzisaidia timu kufuzu lakini timu ndogo zikatae kuwa madaraja ya kupandia kwa timu kubwa.

USHAURI WAKE

Anasema wachezaji wengi bado ni vijana na uchezaji ni kipaji, ambacho hakiwezi kudumu hadi uzeeni hivyo wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuwa imara kisoka kwa kipindi hiki ambacho bado wana nguvu za kuwekeza katika maendeleo.

Sagala anamtolea mfano mchezaji Mbwana Samatta ambaye baada ya kuchukuliwa kwenda kucheza Uingereza alionyesha juhudi zake na kuendelea kununuliwa na timu kubwa nchini humo ikiwemo Aston Villa ambayo anasema ingemsajili kwa wakati huu, Mtanzania huyo angeweza kung’ara zaidi kuliko kipindi kile ambacho timu ilishachoka.

Anawashauri wachezaji chipukizi kuwa, wanapopata mechi na timu za nje watambue hiyo ndio nafasi kwao ya kujitangaza na kukuza soka la Tanzania na si kufanya uzembe unaojitokeza.

“Nashangaa hawa wachezaji naenda kucheza mechi za nje lakini baada ya wiki moja au mbili wanakuwa tayari wamerudi badala ya kutumia nafasi hiyo kujitangaza kisoka.”

“….mimi nilienda Botswana na si kwamba nilikuwa na timu ila nilienda kujitangaza ili nipate timu ya kucheza na nilifanikiwa kwa kuwaonyesha kipaji changu, lakini hawa vijana wetu wanapata nafasi za kwenda nchi za mbali na kudhaminiwa na timu zao kwa kila kitu lakini asilimia kubwa hawaitendei haki nafasi wanayopata,” anasema Sagara.

Kutokana na kuwa watu wengi wamewekeza katika soka, anaona ni wakati muafaka kwa wazawa kuitumia fursa hii kwa kuendelea na kuonyesha uwezo wao ili wadhamini wa timu wawaone na kuwasajili.

Jina: Eric Sagala ‘Cantona’

Kuzaliwa: 1958

Uraia: Tanzania

Nafasi: Winga

Timu alizochezea: CDA, Simba, Township Roller’s, BDFnchini Marekani

Kwa sasa: Shughuli binafsi.


Imeandikwa na HABEL CHIDAWALI NA EDA LAJU (DMC)