Sabilo: Kushusha timu ni mkosi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

KILA kazi inafuraha na machungu yake ndio maana kila mtu hutamani kazi anayofanya mwenzake huku ile anayofanya yeye huichukulia poa asijue machungu yake.
Msimu uliomalizika hivi karibuni timu tatu za Ligi Kuu zimeshuka daraja kwenda Ligi ya Championship ambazo ni Mbeya City, Ruvu Shooting na Polisi Tanzania.

Zilizopanda Ligi Kuu kutoka Ligi ya Championship pia zipo tatu, JKT Tanzania, Kitayosce na Mashujaa FC iliyopanda kupitia hatua ya mtoano.

Furaha kubwa kwa zile timu zilizopanda lakini machungu kwa wale walioshuka daraja sababu wengi wao watapoteza ajira zao.
Hata hivyo winga wa Mbeya City, Sixtus Sabilo anasema anaona kama vile mkosi kwenye maisha yake ya soka.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Sabilo anasema haamini kilichotokea timu yake kushuka daraja.

Mbeya City ni moja ya timu iliyoanza vyema Ligi Kuu hadi inamaliza mzunguko wa kwanza ilikuwa 'top four' kwenye msimamo wa ligi hiyo lakini matokeo yakawa tofauti mzunguko wa pili ulipoanza.

Sabilo anasema; "Timu ilikuwa kwenye morali kubwa kila mmoja alikua anajituma kupambania timu ndio maana uliiona ikiwa nafasi za juu na kila mpinzani alikuwa akituhofia.

"Ghafla mambo yakaanza kubadilika taratibu tukiwa tunapata sare nyingi kuliko kushinda, unajua kwenye soka bora upoteze mbili lakini ushinde tatu kuliko upate sare tano."
Sabilo anasema matokeo yale yalianza kuidhoofisha timu na morali kwa wachezaji ikaanza kushuka taratibu kadri siku zilivyokuwa zinasogea.
"Unajua siku zote ushindi unakufanya kupambana zaidi lakini ukipoteza inakufanya uonekane mnyonge zaidi ya ulivyo ndio maana timu ikiwa inashinda siku zote inaendelea kushinda." anasema


MALENGO YAKE
"Sijui nianze na lipi kueleza sababu kila mmoja anakuwa na lengo lake pale msimu unapoanza sasa kwangu sijui niseme malengo yangu yamefanikiwa kwa asilimia ngapi.
"Unajua malengo ya wengi siku zote ndio yanathaminisha malengo ya mtu, mfano hata kama malengo yangu hayakutimia halafu timu ikamaliza nafasi tano za juu hapo hata thamani ya mchezaji inapanda.

"Malengo ya mchezaji siku zote yanaambatana na malengo ya timu, hivyo kama timu imeshindwa kutimiza lengo basi hata lengo langu halijafanikiwa." anasema

Nyota huyo aliyemaliza msimu na mabao tisa anasema katika uchezaji wake soka hajawahi kucheza timu ikashuka daraja hivyo msimu huu ndio umekuwa wa kwanza kwake.

"Hakuna kitu kibaya kama kushuka daraja haya maumivu ndio naona sasa namna wenzangu huko nyuma wakishuka nilikuwa nawashuhudia lakini sikuwahi kujua maumivu yake.
"Hii ni historia mbaya kwangu kwenye soka sababu moja ya malengo ni kuona timu ikifanya vyema hivyo kushuka daraja kwa Mbeya City hata yale malengo yangu nikisema yametimia haina maana yoyote."


ANAKWENDA WAPI
Anasema licha ya kupata ofa ya nane kutoka timu za Ligi Kuu lakini anasubiri kupata baraka za mabosi wa Mbeya City hivyo muda wowote anasaini dili jipya na timu nyingine ya Ligi Kuu.
Sabilo alisajiliwa Mbeya City kutoka Namungo kwa mkataba wa miaka miwili lakini ameitumikia timu hiyo msimu mmoja na timu kushuka daraja na sasa inajiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Championship.
"Soka ndio kazi yangu lakini sijazungumza biashara na timu yeyote sababu ya maumivu niliyokuwa nayo moyoni kuhusu Mbeya City lakini kuanzia sasa nitafungua milango baada ya kumalizana na uongozi wa Mbeya City."
Sabilo hakuweza kuweka wazi juu ya dili lake la kutakiwa na Geita Gold pamoja na JKT Tanzania japo alieleza kati ya timu nane zilizotuma ofa nazo ni miongoni.


ALIKOPITA
Timu nyingine alizowahi kuzitumikia nyota huyo mbali ya Mbeya City na Namungo ni Polisi Tanzania, Stand United na KMC.
Msimu wa kwanza ikiwa Ligi Kuu, Polisi Tanzania ilimaliza nafasi ya tano ikiwa na alama 55 msimu uliopita akiwa Namungo FC timu hiyo imemaliza nafasi ya tano kwa alama 41 na msimu huu akiwa Mbeya City timu imeshuka.
Anasema kila timu aliyokuwa anacheza aliondoka ikiwa nafasi nzuri ambayo ilizidi kumweka kwenye viwango vizuri.
Alianza soka kijijini kwao Kasahunga, Bunda, Mara akiwa anasoma shule ya Msingi Kasahunga na baada ya kumaliza 2007 akagundua kipaji chake akiwa shule ya Sekondari Nyeruma.

"Nilipokuwa sekondari nilipata nafasi ya kushiriki michezo ya Umisseta na kuchaguliwa timu ya Kanda ya Ziwa mashindano yaliyofanyika Kibaha, Pwani baada ya hapo nikacheza timu yangu ya mtaani Town Star Bunda ndipo nikaonekana na Polisi Mara (Biashara United).
Alitua kwenye kikosi hicho kwa ada ya usajili  Sh 80,000 lakini alipewa Sh 50,000 na msimu wa 2013/2014 akacheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na timu hiyo.


NDONDO YAMTOA
"Kulikuwa na mshindano ya mbunge, Ester Bulaya jimbo la Bunda Mjini ndio nikawa nacheza ndondo kutoka kijijini na hapo wakaniona viongozi wa Bulyanhulu FC.
"Jacob Massawe aliniona kwenye mashindano hayo, akaniambia niende nikafanye majaribio Stand United, Shinyanga na hatimaye nikafanikiwa msimu wa 2016/17 nikacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza." anasema Sabilo

Aliitumikia Stand United kwa miaka miaka miwili na miezi sita kisha 2018 wakati wa dirisha dogo la usajili akatua KMC kwa mkataba wa mwaka mmoja

"KMC nilicheza miezi sita wakanitoa kwa mkopo Polisi Tanzania kwa miezi sita iliyokuwa imebaki na nilipomaliza msimu uongozi wa Polisi ukanisajili kama mchezaji huru."