Sababu ya maji viwanja vya gofu

UMEWAHI kujiuliza mashimo ya maji (water hazard) kwenye viwanja vya gofu yana kazi gani? Unaambiwa viwanja vikubwa ambavyo ni standadi katika mashimo 18, matatu pekee ndiyo yatakosa eneo lenye maji.

Kocha na nyota wa gofu, Rodrick John anasema maji kwenye viwanja vya gofu yamewekwa makusudi ili mchezaji aharibu au kutumia akili kubwa kuvuka eneo hilo.

Anasema katika mashimo 18 unaweza kucheza mashimo tisa kutokana na muda, na viwanja vingi lazima viwe na eneo lenye maji.

“Vile vya kimataifa utakuta vitatu kati ya 18, ndivyo havina eneo lenye maji. Maji hayo yanakuwa na kina kirefu kidogo na yamewekwa makusudi ili uharibu.

“Inahitajika akili kubwa ili uyavuke yale maji mpira usiingie huko, ukiingia kwanza unapata hasara ya kuupoteza, pia ni kama faulo, badala ya kupiga shoti tatu, utalazimika kupiga nne na ukicheza hadi shoti sita ni mbaya zaidi kwenye matokeo.

Mpira ukiingia kwenye maji inaitwa ‘droping zone’, hivyo badala ya kupiga shoti mbili ili ya tatu uingize kwenye shimo utalazimika kupiga tatu na wapo ambao watapiga ‘line off’, hivyo itamlazimu kupiga nne na mwisho wa shoti ni tano, ukipiga sita inakuwa ni mbaya kwa mchezaji na katika gofu mwenye shoti chache ndiye mshindi.

“Mchezaji mzuri akipiga mara moja mpira utafika juu ya kiwanja, shoti ya pili anasogeza na ya tatu anaingiza kwenye shim. Wapo wanaopiga shoti moja au mbili, mfano kwenye mashindano makubwa wanaweka hadi zawadi ya gari kwa wanaopiga shoti moja na kuingiza kwenye shimo, Woods (Tiger nyota wa dunia) amefanya mara kadhaa hivyo.

“Ila ukipiga moja na haujafika juu ya uwanja maana yake shoti ya pili ndio utafikisha uwanjani na ya tatu utasogeza ya nne utaingiza kwenye shimo, usipoweza mwisho kabisa huwa ni shoti tano ambayo si nzuri na ukifikisha sita ni mbaya maana yake umeharibu, ili ucheze vizuri, angalau upige chini ya shoti nne.”