Robbyone: Wanamichezo wawekeze kwenye afya

MATUKIO ya kuanguka na kufariki dunia kwa wachezaji yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara lakini ufumbuzi wake haujapatikana.
Hivi karibuni mchezaji wa kimataifa wa Ghana, Raphael Dwamena alifariki dunia baada ya kudondoka uwanjani kutokana na tatizo la moyo akiwa anaitumikia KF Egnatia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Albania dhidi ya Partizani Novemba 11, mwaka huu.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na mdhamini na mdau wa masuala ya afya kwenye michezo, Robart Mchunguzi ‘Robbyone’ ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya kutatua changamoto ya wachezaji kufariki dunia wakiwa uwanjani.
AFYA MICHEZONI CHANGAMOTO
Ni ngumi pekee mabondia wamekuwa wakifanya vipimo wiki moja au mbili kabla ya pambano na baadae kurudia siku chache kabla ya pambano hilo kwa upande wa soka halipo.
“Afya ni jambo zuri sana kwa wachezaji lakini limekuwa halipewi kipaumbele jambo ambalo limekuwa likisababisha shida viwanjani ikiwamo vifo;
“Nina miaka mitano kwenye maisha ya michezo, sasa nimeamua kuwekeza nguvu kwenye ngumi nikisimamia zaidi sekta ya afya kwa kuhakikisha mabondia wanapata vipimo kabla ya mapambano.” anasema Mchunguzi ambaye ni mdhamini wa ndondi.
AWAONYA MASTAA
Anasema mastaa wa soka wanalipwa pesa nyingi tofauti na mabondia na hivyo wanatakiwa kuwekeza kwenye afya na hata mabondia ambao wanatumia zaidi miili yao kutafuta pesa, wanatakiwa kuwekeza huko ili kuwa na maisha bora.
Pia anawaonya kuhusu maisha ya kawaida na vipato wanavyoingiza wawekeze ili wasiwe ombaomba kwani maisha ya kuwa mwanamichezo ni ya muda mfupi.
“Mabondia licha ya kutokuwa na kipato kikubwa kama ilivyo kwa wachezaji wa soka wanapaswa kuwekeza kimaisha ili muda wao ukifika wa kustaafu waachane na tabia za kugeuka waombaji.
“Tabia hii sio kwa mabondia tu hata kwa wachezaji imekuwa ikijitokeza hivyo ni wakati sahihi kwao, wakati huu wanapata fedha wajiwekeze, napenda kumsifu Mandonga licha ya kudundwa amejitahidi kwenye uwekezaji,” anasema.
MANDONGA NYOTA WA NGUMI
Anataja jina la bondia Karim Mandonga ni miongoni mwa mabondia ambao wameurudisha mchezo kutokana na makeke yake.
“Mandonga karudisha mchezo wa ngumi kwenye piki sasa unazungumzwa na unatajwa sana na watu hii ni kutokana na uchangamfu wake licha ya kupigwa lakini ameleta amsha amsha kwenye mchezo huu;
“Mandonga umaarufu wake pia umeongeza uwekezaji kwenye ngumi, nilikuwa upande wa Miss Tanzania, Big Brother Bingwa na kwenye soka ndio naingia mdogo mdogo kwani nipo kwenye mazungumzo na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ili niweze kusimamia suala la afya kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi,” anasema na kuongeza;
“Kwenye ngumi nimevutiwa na Mandoga ambaye amekuwa akiufanya mchezo huo kuzungumzwa muda mwingi nafurahia kuingia huko kwani licha ya kuto kunufaika, nafurahia kuona vipaji vinaendelezwa nikiwa miongoni mwa watu walio nyuma yao.”
MWAKINYO ANOGESHA MIKATABA
Anazungumzia pia juu ya bondia Hassan Mwakinyo kugoma kucheza pambano lililodaiwa kuandaliwa kwa gharama kubwa kutokana na sababu ya kubadilishiwa bondia.
“Kugoma kwa Mwakinyo kumetufanya sisi kama waandaaji wa mapambano sambamba na chama cha mchezo huo kuboresha mikataba ambayo itawafanya mabondia kuingia gharama kubwa endapo watarudia michezo baada ya kususa;
“Kuahirishiwa bondia sio kitu kigeni huwa kinafanyika kutokana na sababu mbalimbali, mfano kapata shida ya kiafya ghafla au kuumia mazoezini, lazima pambano liahirishwe, pia wao ni binadamu anaweza akapatwa na msiba hilo limekuwa likizungumzwa kama tatizo la ghafla na linaweza kufanya pambano likaahirishwa,” anasema.
Anasema kutokana na sakata hilo mikataba imeboreshwa ili kumlinda mwandaaji, mdhamini, akikiri mabondia wengi hawathamini wanachofanyiwa.
SASA NI ZAMU YA MAJIA
Licha ya kumtaja Mandonga ndiye aliyerudisha mchezo huo kwenye ushindani mwekezaji huyo na mdau wa masuala ya afya anasema Fadhili Majia ni bondia hatari zaidi kwa sasa.
“Kuna mabondia wengi wazuri lakini kwa upande wangu namwona Majia akifika mbali kama atajiweka kwenye ushindani na kuuchukulia mchezo huo kama ajira;
“Ni bondia ambaye anabadilika badilika katika kila raundi na huo ndio uchezaji mzuri tofauti na wengine mwanzo mwisho wamekuwa na aina moja ya uchezaji hao mara nyingi ndio wamekuwa wakipingwa raundi za mapema kutokana na kusomwa na mpinzani,” anasema.
Anawataja Ibrahim Class, Dulla Mbabe, Twaha Kiduku wao pia ni wazuri lakini wamekuwa wakikata pumzi mapema huku akimtaja Majia anaweza kucheza raundi hata 12 akiwa na mifumo tofauti na kumpa mpinzani kazi ya kumsoma.
KINACHOANGUSHA NGUMI
“Ili mchezo wa ngumi ufike mbali kama lilivyo soka la Tanzania kwa sasa ni kutafuta viongozi waliosimama katika maadili na kuuchukulia mchezo huo kama ajira ambayo itaweza kupunguza na kuondoa kabisa mabondia kwenye changamoto ya uchumi mdogo;
“Natamani kuona bondia anapata Sh50, 80 hadi 100 milioni kwa pambano moja, hivi sasa hakuna na hili linawezekana kama tutapata viongozi imara na bora kwani wawekezaji wanaogopa kuja huku kutokana na ubabaishaji,” anasema.
Mchunguzi anasema ameamua kuwekeza kwenye suala la afya zaidi ili kuwaondoa mabondia kwenye hali hatarishi wanapokuwa ulingoni huku akisisitiza hata kwenye soka inawezekana.
AITAMANI YANGA
Wanasoka wamekuwa wakifanya vipimo kipindi cha usajili tu na baada ya hapo wao kazi ni moja tu kufanyia kazi mikataba wanayopewa baada ya vipimo.
“Wachezaji ndio wanaongoza kwa kudondoka uwanjani na baadaye kupoteza maisha, hivyo ni jambo jema kama watawekeza kwenye suala la vipimo kwa wachezaji wao mbali na kupima kabla ya kuwasajili;
“Mimi ni shabiki wa Yanga, nitafanya mazungumzo na viongozi wa timu hiyo ili wanipe dhamana ya kufanya vipimo vya mara kwa mara kwa wachezaji kama ilivyo kwa ndondi.” anasema.
AMCHAMBUA MAXI, MUSONDO
Yanga msimu huu imefanya usajili wa wachezaji wengi lakini mchunguzi amemtaja Maxi Zingeli kuwa ni mchezaji punda ndani ya kikosi cha timu hiyo.
“Maxi akiwa uwanjani huelewi ni kiungo mkabaji, mshambuliaji au winga sehemu zote anaonekana ana jicho la kuona goli anakupa vitu vingi uwanjani, ni aina ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa kutoka nje na kuja kucheza soka la kulipwa Tanzania hata fedha haiumi kumlipa,” anasema na kuongeza;
“Kiungo huyo mshambuliaji amebeba majukumu mengi akimpiku Keneddy Musonda ambaye tulimtegemea kwa mambo makubwa lakini ameshindwa kutuonyesha sisi kama wadau na wanachama wa Yanga.”