Rekodi tamu za Ligi Kuu Wanawake Bara 2022/2023

MSIMU wa mwaka 2022/23 Ligi Kuu ya Wanawake Bara umehitimishwa Mei 17, kwa timu zote kucheza michezo yao ya mwisho huku JKT Queens ikitwaa ubingwa kwa rekodi ya bila kupoteza mchezo.

JKT Queens imetwaa ubingwa huo ikishinda mechi 14 na sare nne huku kikosi chake kikiwa na wachezaji wazawa pekee ambapo timu hiyo ilizifunga timu zote 10.

Mkwawa Queens ya Iringa na The Tigers Queens ya Arusha zimeshuka daraja kwenda la Ligi Daraja la Kwanza, Bunda Queens ya Mara na Geita Gold Queens ya Geita zikipanda kuziba nafasi ya timu hizo.

Mshambuliaji wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa ameibuka mfungaji bora wa ligi hiyo akifunga mabao 17 akicheza mechi 15, akifuatiwa na Donisia Minja wa JKT Queens (15) na Winfrida Charles wa Alliance Girls na Stumai Abdallah (JKT) mabao 13.

Mwanaspoti limefanya tathmini ya ligi hiyo na kukuletea baadhi ya rekodi za kipekee ambazo zimewekwa msimu huu hususani kwenye ufungaji mabao. Zifuatazo ni sehemu ya rekodi hizo...


HAT-TRICK 11

Jumla ya hat-trick 11 zimefungwa msimu huu na wachezaji saba huku JKT Queens ikiongoza kwa kufunga hat-trick tano zilizofungwa na wachezaji wawili pekee, Donisia (3) na Stumai (2).

Timu zote zilizomaliza nafasi tano za juu zimefunga walau hat-trick moja msimu huu, ambazo ni JKT Queens (5), Alliance Girls (2), Simba Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess hat-trick moja kila mmoja.

Mshambuliaji wa Ceassia Queens ya Iringa ni mchezaji pekee nje ya timu zilizomaliza nafasi tano za juu ambaye amefunga hat-trick, ambapo alifanya hivyo dhidi ya The Tigers Queens.

Wachezaji waliofunga hat-trick msimu huu ni Donisia, Stumai, Winfrida Charles (2), Joanitha Ainnembabazi, Cynthia Musungu, Blessing Nkor na Jentrix kila mmoja alifunga moja.


JENTRIX

Jentrix ni mchezaji pekee kwenye hiyo ambaye amefunga mabao manne katika mchezo mmoja. Alifanya hivyo dhidi ya Alliance Girls kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza Februari Mosi, 2023.

Ambapo Simba Queens ilishinda mabao 4-0 akiyafunga yote akifanya hivyo dakika ya nane, 25, 43 na 64.


WINFRIDA, DONISIA

Mshambuliaji wa Alliance Girls, Winfrida Charles na Donisia ni wachezaji pekee kwenye Ligi hiyo ambao wamefunga hat-trick mbili dhidi ya timu moja.

Wachezaji hao wamefunga hat-trick mbili kila mmoja dhidi ya Mkwawa Queens katika mechi zote mbili nyumbani na ugenini.


REKODI YA SIMBA

Rekodi ya Simba Queens iliyowekwa msimu uliopita ya kufunga hat-trick nne katika mchezo mmoja imeshindwa kuvunjwa wala kufikiwa na timu yoyote msimu huu.

Msimu uliopita, Simba Queens iliichapa Ruvuma Queens mabao 15-0 huku wachezaji wake wanne, Oppah Clement, Asha Djafari, Zena Khamis na Jackline Albert wakifunga mabao matatu kila mmoja.

Simba Queens imeambulia hat-trick moja tu msimu huu iliyofungwa na Jentrix dhidi ya Alliance Girls ikiwa ni tofauti na msimu uliopita ambapo ilifunga hat-trick sita, huku nne zikifungwa katika mchezo mmoja dhidi ya Ruvuma Queens walioshinda mabao 15-0.


OPPAH, CYNTHIA

Washambuliaji, Oppah na Cynthia wa Fountain Gate Princess licha ya kucheza mechi tisa tu za kwanza na kutimkia Ulaya lakini wamemaliza na mabao tisa na kumaliza nafasi ya tano kwenye vinara wa mabao wa ligi hiyo.

Oppah na Cynthia walikuwa moto wa kuotea mbali kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo (mechi tisa) lakini wakapata ofa ambapo Oppah alisajiliwa Beskitas ya Uturuki huku Cynthia akienda zake Kryvbas ya Ligi Kuu nchini Ukraine.

Hadi mzunguko wa mwisho ni wachezaji wanne pekee waliowazidi mabao, Jentrix (17), Donisia (15), Stumai na Winfrida (13) waliowazidi mabao.


ASHA DJAFARI

Msimu uliopita aliibuka kinara wa mabao akitupia kambani mabao 27 katika mechi 22, lakini msimu huu ameshindwa kutetea kiatu chake huku akifunga mabao nane pekee katika mechi 18 na kuishia kukamata nafasi ya nane kwenye orodha ya vinara wa mabao msimu huu.

Pia katika timu yake msimu huu amekosa uhakika wa namba akianzia benchi ama kuishia kukalia mbao. Hata hivyo, amekamata nafasi ya tatu kwa wafungaji bora wa timu yake ya Simba Queens (8) nyuma ya kinara, Jentrix (17) na Oppah (9).


MFUNGAJI BORA AKWAMA

Ni mara ya kwanza katika misimu sita tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo, mfungaji bora kutofikisha mabao 20 jambo linaloashiria kuimarika kwa timu na ushindani mkubwa katika michuano hiyo.

Misimu miwili mfululizo akiwa mfungaji bora, Fatuma Mustapha wa JKT Queens alifunga mabao zaidi ya 25 huku msimu wa 2018/19 akifunga mabao zaidi ya 30.

Msimu wa mwaka 2020/2021, mshambuliaji wa Yanga Princess, Aisha Masaka akiwa kinara wa mabao wa ligi alifunga 35, lakini msimu uliopita (2021/22), Asha Djafari wa Simba Queens aliongoza akifunga mabao 27.

Lakini msimu huu, kinara wa mabao, Jentrix Shikangwa wa Simba Queens amemaliza na mabao 20 pekee huku ikitajwa kupungua kwa timu za ligi kuu kuwa sababu, kwani msimu huu umeshirikisha timu 10 wakati misimu ya nyuma zilikuwa timu 12.


DONISIA, STUMAI

Stumai na Donisia ni wachezaji pekee msimu huu ambao wamefunga mabao matatu kila mmoja kwa pamoja katika michezo miwili tofauti.

Wachezaji hao walifunga hattrick kwa pamoja katika mchezo dhidi ya Mkwawa Queens ya Iringa na wakafanya hivyo tena dhidi ya The Tigers Queens ya Arusha.


MKWAWA, TIGERS KIBOKO

Katika ligi hiyo jumla ya hat-trick 11 zimefungwa na wachezaji mbalimbali, huku 10 kati ya hizo zikifungwa timu za Mkwawa Queens ya Iringa na The Tigers Queens ya Arusha na hattrick ikifungwa Alliance Girls.

Mkwawa Queens imefungwa hat-trick tano ambazo zimefungwa na Donisia (2), Winfrida (2) na Stumai huku The Tigers Queens nayo ikiruhusu hat-trick tano zilizofungwa na Stumai, Donisia, Joanitha (Ceassia), Blessing Nkor (Yanga) na Cynthia (Fountain).