Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Karia, Mguto watulie kwanza wakati huu

ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Badala yake, Oktoba, 2015 Kamati ya Maadili ikatangaza kumsimamisha uongozi wakati uchunguzi dhidi yake na maofisa wengine ukiendelea, na Desemba mwaka huo Kamati Huru ya Maadili ikaamua kumuondoa madarakani.

WAKATI Rais wa zamani wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Joseph Blatter aliposhtakiwa kwa tuhuma za ufisadi na ubadhilifu wa fedha, Kamati ya Maadili ya chombo hicho haikusubiri shauri hilo liishe mahakamani.

Badala yake, Oktoba, 2015 Kamati ya Maadili ikatangaza kumsimamisha uongozi wakati uchunguzi dhidi yake na maofisa wengine ukiendelea, na Desemba mwaka huo Kamati Huru ya Maadili ikaamua kumuondoa madarakani.

Wakati huo, Blatter alikuwa ametangaza kuachia nafasi yake ya urais ikiwa ni siku chache baada ya kuchaguliwa tena kuendelea na wadhifa wake, lakini alisema angeendelea kukaa madarakani hadi atakapoitisha mkutano wa dharura kwa ajili ya kumchagua rais mwingine. Kamati ya Maadili ikaona hakufaa kuendelea na wadhifa wake na kumuondoa ofisini.

Adhabu ya kufungiwa kwa miaka minane, ilipunguzwa mwaka uliofuata kutokana na kiongozi huyo kukata rufaa, lakini akakutwa tena na makosa mengine yaliyostahili adhabu nyingine ya kufungiwa kwa miaka sita.

ZENG 01

Huo ulikuwa ni mwisho wa enzi za Blatter ambaye alifanikiwa sana kulifanya shirikisho hilo kuwa kubwa tangu alipolipokea kutoka kwa Joao Havelange.

Kwa hiyo, vyombo vya haki vya Fifa havikusubiri mahakama imalize uchunguzi wake na baadaye kesi ndipo navyo vianze uchunguzi wake dhidi ya tuhuma hizo za ufisadi na ubadhilifu dhidi ya Blatter. Wakati uchunguzi wa serikali ukiendelea, Kamati ya Maadili ya Fifa, ambayo ina idara mbili, ile ya uchunguzi na ya mashtaka, navyo vilikuwa vinaendelea na uchunguzi wake ndani ya anga za soka.

Kwa hiyo itakuwa ni ajabu sana hapa kwetu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusema kwa kuwa Yanga imechukua hatua mbalimbali kudai haki inazoamini kuwa ni zake baada ya mechi ya Ligi Kuu baina yake na Simba kuahirishwa kiholela, inasubiri hatima ya mashauri hayo ndipo nayo ifanye uchunguzi.

Sakata la kuahirishwa kiholela kwa mechi hiyo bado halijatulia baada ya Yanga kueleza kuwa tarehe mpya iliyopangwa na Bodi ya Ligi imegongana na mwaliko waliopata kutoka serikali ya Rwanda kucheza mechi ya kirafiki siku hiyo ya Juni 15 kwa ajili ya sherehe za kufungua uwanja mpya.

ZENG 02

Ingawa Yanga ilishasema kuwa haitacheza mchezo huo na inadai ipewe pointi tatu za mechi hiyo, mwaliko huo unaweza kuwa mwanzo wa sababu nyingine ya kuhalalisha kugomea mchezo kama Simba walivyotumia sababu ya kuzuiwa kufanya mazoezi Machi 7, kugomea mechi ya kwanza.

Maana yake sakata hilo linachukua sura mpya kila uchao, lakini kinachoharibu zaidi ni matamko ya viongozi wa juu wa Bodi ya Ligi na TFF.

Matamko hayo yanaweza kumaanisha kuwa, Rais Wallace Karia anatoa maagizo kwa vyombo vyake vya uamuzi vishughulikie sakata hilo kwa mtazamo wake. Hali yale matamko ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto yanaweza kuwa, yanamaanisha uamuzi tayari upo kinachosubiriwa ni kutangazwa tu, ndio maana anawaibia watu siri.

Baada ya shauri la Yanga kurejeshwa kutokana na kutoanzia kwenye vyombo vya uamuzi vya nchi, mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto alisema walifurahia suala hilo tangu waliposikia Yanga imeenda Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kwa kuwa walijua wangeshindwa.

ZENG 03

Unajiuliza kama Mnguto angekaa kimya, angeathika vipi hadi anaamua kutoa kauli ambayo inachochea moto uliokuwa kama unaanza kuzimika?

Lakini nimesikia tena kauli kutoka kwa kiongozi wa TFF akisema kuwa hawawezi kuchukua hatua kwa sasa kwa kuwa shauri la Yanga bado halijatolewa uamuzi. Na hatua hizo ni kufanya uchunguzi kujua waliosababisha mechi ya kwanza iahirishwe kiholela na kuwachukulia hatua.

Ni dhahiri kuwa ingekuwa kosa la kumtukana kiongozi wa TFF au kulishambulia shirikisho hilo, tayari watuhumiwa wangeshaitwa Kamati ya Maadili, ambako hakuna anayeonekana hana kosa bali huenda kutimiza utaratibu wa kumfungia hata akajitetee vipi.

Lakini kwa sababu makosa hayo, kwa akili yao haiwaathiri viongozi wa soka au chombo chenyewe, wanasema kirahisi tu kwamba hawawezi kufanya uchunguzi kwa sasa hadi shauri la Yanga litakapoisha.

Unajiuliza, hivi uchunguzi wa sakata hilo unaweza kuathiriwa vipi na shauri la Yanga kupelekwa kwenye vyombo vingine vya haki kwa ajili ya uamuzi? Huoni uhusiano wowote.

ZENG 04

Rais Wallace Karia na Mnguto hawana budi kuelewa kuwa sakata hilo ni kubwa na limeugusa mpira wa miguu pande zote na hivyo haliwezi kupuuzwa eti kwa sababu tu TFF inaweza kupanga tarehe mpya na timu ambayo haitaenda uwanjani, itaadhibiwa.

Sakata hilo ni zaidi ya mazoea hayo. Ni suala ambalo linahitaji uchunguzi wa kina kujua sababu za kuahirisha mechi hiyo katika mazingira tata yaliyotia dosari mpira wa miguu na ambayo yangeweza kusababisha taharuki kwa mashabiki na madhara makubwa kama mashabiki wasingeendeleza Utanzania wa kumaliza mambo kwa amani.

Kama Blatter anavyoshinda kesi za mahakamani, na Kamati ya Maadili Fifa kumuona kuwa ana hatia, ndivyo ambavyo Yanga inaweza kushindwa huko ilikokimbilia, lakini vyombo vya uchunguzi vya TFF vikabaini makosa kwa wahusika wengine na kuchukua hatua stahiki, iwapo uchunguzi wa kweli utafanyika kutafuta chanzo na suluhisho la uamuzi mbovu katika siku za hivi karibuni.

Uchunguzi wa kina na kuwashughulikia wahusika utasaidia kupunguza vitendo vya mazoea ambavyo vinaonekana kuanza kuendelea.

Na cha muhimu ni kwamba Rais Karia hana budi kuviheshimisha vyombo vyake vya utendaji kwa kutotoa matamko yanayoonyesha anatoa maagizo vishughulikie sakata hilo kwa jinsi anavyoona yeye kuwa inafaa.